Mkuu
wa Oparesheni Maalumu za Polisi, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Liberatus Sabas
(Kushoto) na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Rufiji, Kamishna Msaidizi
Mwandamizi wa Polisi (SACP) Onesmo Lyanga wakionyesha kwa Waandishi wa habari
silaha mbili zilizopatikana baada ya mapambano katika msitu wa Ngomboroni Tarafa
ya Ikwiriri ambapo katika tukio hilo
waliuwawa wahalifu wawili wanaojihusisha na mauaji katika wilaya ya Mkuranga, Kibiti na Rufiji. (PICHA NA
FRANK GEOFRAY-JESHI LA POLISI)
NA
FRANK GEOFRAY -JESHI LA POLISI.
Jeshi la
Polisi nchini limefanikiwa kuwaua wahalifu wawili ambao ni miongoni mwa
wahalifu wanaoendesha mauaji katika Kanda maalumu ya Polisi Rufiji
kufuatia operesheni kali inayoendelea katika Wilaya ya Mkuranga,
Kibiti na Rufiji mkoani Pwani.
Akielezea
tukio hilo, Mkuu wa Operesheni Maalum za Jeshi la Polisi,
Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Liberatus Sabas alisema tukio hilo lilitokea
siku ya Jumatano Julai 5 majira ya saa nne usiku katika msitu wa
Ngomboroni kata ya Ikwiriri, Wilaya ya Ikwiriri Kanda maalumu ya Rufiji
ambapo askari wa operesheni maalum wakiwa katika doria za ufuatiliaji
wahalifu sugu wanaojihusisha na mauaji yanayoendelea katika Kanda hiyo ya
kipolisi.
Sabas
alisema Askari wakiwa na mtuhumiwa mmoja muhimu anayeshiriki katika
mauaji hayo ambaye alikuwa amekamatwa na baada ya mahojiano alikubali
kwenda kuwaonesha Polisi mahali ambapo ni maficho ya wenzake.
Sabas alieleza kuwa, baada ya kufika eneo la msitu wa
Ngomboroni kikundi cha watu wanaokadiriwa kufikia watano
walikurupuka kutoka kwenye kichaka na kuanza kukimbia ndipo askari Polisi
kwa tahadhari kubwa walianzisha mashambulizi na kufanikiwa kumjeruhi mhalifu
mmoja kwa risasi, katika mashambulizi hayo mtuhumiwa aliyekuwa
mkononi mwa polisi naye alijaribu kutoroka na hivyo kupelekea
kumjeruhi kwa risasi hivyo idadi yao kufikia wawili.
Majeruhi hao wawili walifariki dunia njiani wakati
wakipelekwa hospitali kwa matibabu kutokana na kuvuja damu nyingi
iliyosababishwa na majeraha ya risasi waliyoyapata. Miili ya marehemu
imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili.
“Katika tukio hilo tumefanikiwa kupata silaha mbili
aina ya SMG na shot gun moja pamoja na risasi tisa za SMG
zilizokuwa kwenye Magazine.” Alisema Sabas.
Aidha, mkuu huyo wa Operesheni maalum za Jeshi
la Polisi Naibu kamishina Sabas ameendelea kuwasisitiza
wananchi kutoa taarifa zitakazowezesha kupatikana kwa wahalifu wengine
waliosalia na kwamba zawadi nono bado ipo pale pale na itatolewa
kwa mtu yeyote atakayetoa taarifa sahihi kuhusiana na wahalifu
wanaojihusisha na mauaji katika kanda maalumu ya Rufiji.
No comments :
Post a Comment