Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Moyo
ya Jakaya Kikwete (JKCI) Profesa Mohamed Janabi akiteta jambo na baadhi
ya wafanyakazi wa Taasisi yake alipotembelea Maonesho ya 41 ya
Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam leo. Kushoto ni Afisa Uhusiano wa
Taasisi hiyo Bi. Anna Nkinda.
Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Moyo
wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dkt. Bashir Nyangasa
akielezea namna upasuaji wa moyo unavyofanywa kwa mmoja wa mwananchi
aliyetembelea banda la taasisi hiyo katika Maonesho ya 41 ya Kimataifa
ya Biashara Dar es Salaam (Sabasaba) leo.
Wananchi wakipata huduma ya vipimo
katika banda la Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) wakati wa
Maonesho ya 41 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam (DITF) leo.
Picha na: Frank Shija – MAELEZO.
……………………………….
Frank Mvungi- Maelezo
Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete
imewataka Wananchi kujitokeza kwa wingi kupima afya zao hasa magonjwa
ya moyo katika msimu huu wa maonesho ya Kimataifa ya 41 ya Biashara ya
Dar es Salaam yanayofanyika katika viwanja vya JK Nyerere jijini Dar es
Salaam.
Akizungumza katika viwanja vya
maonesho hayo Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo Prof. Mohamed Janabi
amesema kumekuwa na muitikio mkubwa sana kwa wananchi kutembelea banda
lao ambapo amesema kuwa kwa siku takribani watu 700 wanafika katika
banda hilo kwa ajili ya kupata huduma na ushauri.
“Ni vizuri watanzania wakatumia
fursa hii kufika hapa na watapatiwa baadhi ya vipimo na ushauri bure
katika banda letu lililopo ndani ya viwanja vya sabasaba kwa kuwa
dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuwahudumia wananchi wake kwa
kuhakikisha kuwa wanapata huduma zote za msingi zenye kiwango na ubora,”
Alisisitiza Prof. Janabi
Akifafanua Prof. Janabi amesema
Taasisi hiyo imedhamiria kuwahudumia wananchi wakati wote wa maonesho na
hata baada ya hapo wapo tayari kuwahudumia wale wanaohitaji huduma
katika taasisi hiyo.
Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete
imekuwa ikitoa huduma za upasuaji wa moyo tangu kuanzishwa kwake hali
inayosaidia kupunguza gharama zilizokuwa zinatumika kusafirisha wagonjwa
kwenda nje ya nchi kwa matibabu kwa kipindi kirefu sasa.
No comments :
Post a Comment