![]() |
| Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Jijini Tanga (TANGA UWASA) Mhandisi Joshua Mgeyekwa akifafanua jambo wakati akizungumza na waandishi wa habari |
NA ISMAIL NGAYONGA, MAELEZO
TAARIFA ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 2004 inaonesha kuwa ifikapo mwaka 2025, nchi za Bara la Afrika hususani zilizopo kusini ya jangwa la Sahara, zitakumbwa na upungufu mkubwa wa maji kutokana na ongezeko la watu na matumizi ya maji yasiyo endelevu.
TAARIFA ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 2004 inaonesha kuwa ifikapo mwaka 2025, nchi za Bara la Afrika hususani zilizopo kusini ya jangwa la Sahara, zitakumbwa na upungufu mkubwa wa maji kutokana na ongezeko la watu na matumizi ya maji yasiyo endelevu.
Aidha inakadiriwa kuwa upatikanaji wa maji kwa kila mtu kwa mwaka
utapungua toka mita za ujazo 2,300 za sasa hadi 1,500 ifikapo 2025 kutokana
tatizo la kuharibika na kupotea kwa vyanzo vya maji.
Pamoja na umuhimu wa maji kueleweka na kila mwananchi, taarifa zinaonyesha
kuwa vyanzo vingi vya maji nchini vimeendelea kuharibika kwa kasi na
kusababisha maji kupungua katika mito na maziwa mengi.
Ili kukabiliana na hali hiyo, Serikali inatekeleza Programu ya
Maendeleo ya Sekta ya Maji 2006-2025 inayolenga katika kuhimiza na kusisitiza
usawa na utashi katika utunzaji na usimamizi wa rasilimali za maji katika
maeneo ya mijini na Vjijini.
Kwa hapa nchini, huduma ya
usambazaji wa maji safi na salama na uondoaji wa majitaka Mijini inatekelezwa
na Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira katika Miji Mikuu ya Mikoa,
Wilaya, Miji Midogo.
Inaelezwa kuwa wastani wa
uzalishaji wa maji katika miji mikuu ya mikoa imepungua kutoka lita milioni 470
kwa siku mwezi Machi 2016 hadi kufikia lita milioni 400 kwa siku mwezi Machi,
2017 kutokana na kupungua kwa wingi wa maji katika vyanzo vya maji katika
maeneo mbalimbali nchini.
Katika kukabiliana na
changamoto hiyo, Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Jijini Tanga (TANGA
UWASA) kwa kushrikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga mwaka 2015 ilizindua
Filamu ya utafiti ya Mamba wa Zigi iliyoelezea kuhusu
uharibifu wa mazingira katika milima ya usambara ambayo ndio chanzo kikuu cha
upatikanaji wa maji Jijini Tanga.
Akizungumza hivi karibuni na
Waandishi wa vyombo vya Habari Jijini humo, Mkurugenzi Mtendaji wa TANGA UWASA,
Mhandisi Joshua Mgeyekwa anasema kabla ya uzinduzi wa filamu, mamlaka hiyo
ilikuwa ikikabiliwa na changamoto kubwa ya uharibifu wa mazingira katika mito
midogo midogo inayounganisha Mto Zigi na Bwawa la Mabayani na hivyo kutishia
uendelevu wa huduma ya kusambaza maji Jijini Tanga.
Anasema utafiti wa filamu hiyo
ulionyesha kuwa shughuli za kijamii na kiuchumi zikiwemo kilimo, ukataji miti,
uogeshaji mifugo, na uchimbaji wa madini ulichangia kwa kiasi kikubwa uharibifu
wa mazingira katika maeneo mengi Vijini vinavyozunguza Mto Zigi unaounganisha
Wilaya za Muheza, Mkinga na Tanga.
“Kufuatia hali ya uharibifu wa
vyanzo vya maji katika maeneo hayo, mwaka 2009 tuliamua kutumia fursa ya
utafiti kupitia filamu kwa kuwasiliana na wadau mbalimbali wa mazingira kwa
ajili ya kutoa elimu na kuendesha tafiti ili kuonyesha hatua zinazopaswa
kuchuliwa katika kulinda na kuhifadhi vya maji ya Mto Zigi” anasema Mhandisi
Mgeyekwa.
Kwa mujibu wa Mhandishi
Mgeyekwa anasema tangu kuzinduliwa kwa filamu hiyo mafanikio mbalimbali
yameweza kupatikana ikiwemo uanzishaji wa Umoja wa Wakulima Wahifadhi Mazingira
Kihuhwi Zigi (UWAMAKIZI) ambapo jumla ya vijiji 8 vimejiunga katika Umoja huo ulioanzishwa
mwaka 2013 kwa ajili ya ulinzi wa ardhi, maji na mazingira katika eneo la
vyanzo vya Mto Zigi.
Umoja huu ulianzishwa mwaka
2013 ukihusisha vijiji 5 ambavyo ni Kimbo, Shembekeza, Mashewa, Bombani na
Kwaisaka ukiwa na wanachama 473 na hadi Juni 2016 UWAMAKIZI ulikuwa na jumla ya
wanachama 610 kutoka vijiji 8 vya Halmashauri ya Wilaya ya Muheza.
Mhandisi Mgeyekwa anasema
kutoka mwaka 2013-2016, TANGA UWASA kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Muheza
imeupatia Umoja huo kiasi cha Tsh. Milioni 100 kwa ajili ya kuendesha elimu ya
kilimo hai na kilimo hifadhi sambamba na kampeni ya uhamasishaji wa uhifadhi wa
mazingira.
Anasema hadi kufikia Juni 2017
kupitia juhudi za Umoja huo, jumla ya miti 3,196,174 imeoteshwa na kupandwa
katika maeneo yote yanayozunguka vijiji vilivyopo ndani ya mradi ikihusisha
miti ya mbao, matunda, viungo na miti rafiki na maji.
Akifafanua zaidi Mhandisi
Mgeyekwa anasema kupitia utafiti wa filamu mwaka 2016, Serikali kupitia Wizara
ya Maji na Umwagiliaji kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Umoja wa
Mataifa (UNDP) zimeanza utekelezaji wa mradi wa miaka (2016-2020) wa uhifadhi
wa mazingira katika Bonde la Mto Wami na Bonde la Mto Zigi.
Anaongeza kuwa mradi huo
umetengewa kiasi cha Tsh. Milioni 180, ambapo mpaka sasa kiasi cha Tsh. Milioni
80 zimetolewa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo ikiwemo kutandaza mabomba
na kufunga viunganishi kwa ajili ya kusambaza maji kwa wananchi waliopo katika
vijiji vya Mashewa, Kimbo na Shembekeza waliopo katika umbali wa kiomita 2.5
kati ya kilometa 6.5 zinazohitaji.
“Mradi huu pia utasaidia
kujenga malambo ya kunyweshea mifugo katika eneo la Bwawa la Mabayani ili
kuzuia mifugo kunywa maji moja kwa moja kutoka Mto Zigi, ambapo kaisi cha Tsh.
Milioni 50 tayari zimetengwa” anasema Mgeyekwa.
Sote tunafahamu kuwa asilimia
75 ya uso wa dunia ni maji na asilimia 70 mpaka 75 ya mwili wa binadamu pia
inachukuliwa na maji, kuhakikisha kuwa utunzaji na uendelezaji wa
rasilimali za maji unaendelezwa kwa ushirikiano na mipango ya pamoja.
Mtaalam
wa Mazingira na Afisa Ubora na Viwango Ramadhan Nyabuke akielezea jambo wakati
wa mkutano baina ya Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka hiyo (hayupo pichani) na
wandishi wa habari mapema hivi karibuni Ofisini kwake kuhusu mafanikio
yatokanayo na utafiti kupitia Filamu ya Mamba wa Zigi. Filamu hiyo imeelezea
namna wananchi wanaozunguka maeneo ya mto Zigi unaounganisha wilaya za Muheza,
Mkinga na Tanga wanavyoathiriwa na uharibifu wa vyanzo vya maji.
Baadhi
ya wafanyakazi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jijini Tanga (TANGA
UWASA) wakifuatilia mkutano baina ya Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka hiyo
(hayupo pichani) na wandishi wa habari mapema hivi karibuni Ofisini kwake
kuhusu mafanikio yatokanayo na utafiti kupitia Filamu ya Mamba wa Zigi. Filamu
hiyo imeelezea namna wananchi wanaozunguka maeneo ya mto Zigi unaounganisha
wilaya za Muheza, Mkinga na Tanga wanavyoathiriwa na uharibifu wa vyanzo vya
maji
Afisa
Uhusiano wa Umma wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jijini Tanga (TANGA
UWASA) Bi. Dorah Killo akielezea jambo
wakati wa mkutano baina ya Mkurugenzi Mtendaji wa Tanga Uwasa, Mhandisi
Joshua Mgeyekwa (katikati) na waandishi wa habari mapema hivi karibuni Ofisini
kwake kuhusu mafanikio yatokanayo na utafiti kupitia Filamu ya Mamba wa Zigi.
Filamu hiyo imeelezea namna wanachi wanaozunguka maeneo ya to Zigi uliopo
Muheza Mkoani Tanga wanavyoathiriwa na uharibifu wa vyanzo vya maji. Kushoto ni
Mkurugenzi wa Kampuni iliyotengeneza Filamu hiyo Bw. Humphrey Mgema .





No comments :
Post a Comment