WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa ametembelea mradi wa ujenzi wa daraja la mto
Lukuledi lenye urefu wa kilomita 30.45 linalounganisha mikoa ya Lindi na
Mtwara na na kusema kwamba ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi wake.
Amesema
ujenzi wa daraja hilo unatakaogharimu sh. bilioni 5.4 ni mkombozi kwa
wananchi wa mikoa hiyo hasa wa wilaya za Ruangwa na Masasi ambao kwa
muda mrefu wamekuwa wakishirikiana katika masuala mbalimbali yakiwemo
kilimo na huduma za kijamii.
Waziri
Mkuu amesema hayo leo (Jumanne, Julai 11, 2017) alipotembelea mradi huo
wa ujenzi wa daraja hilo katika kijiji cha Nandanga alipowasili
wilayani Ruangwa akiwa katika siku ya pili ya ziara yake ya kikazi ya
siku nne Mkoani Lindi.
“Watu
wengi wamepoteza maisha kwa kuliwa na mamba walipokuwa wakikatiza
katika eneo hilo. Ujenzi wa daraja hili ni muhimu, watu wengi wa Ruangwa
wanavuka kufuata matibabu katika hospitali ya Ndanda, wilayani Masasi
na wakazi wa Ndanda wanavuka kufanya shughuli za kilimo wilayani
Ruangwa.”
Pia
Waziri Mkuu amewaomba wananchi wa maeneo hayo kuhakikisha wanatoa
ushirikiano kwa mkandarasi anayejenga daraja hilo ili aweze kutekeleza
majukumu yake ipasavyo na kumaliza mradi huo kwa wakati.
Kwa upande wake Mbunge
wa jimbo la Ndanda, Mheshimiwa Cecil Mwambe ameipongeza na kuishukuru
Serikali kwa jitihada zake za kuwaletea wananchi maendele0 na
kubadilisha maisha yao.
Amesema
mradi wa ujenzi wa daraja hilo ni faraja kwa wananchi wa mikoa hiyo kwa
kuwa eneo hilo ni makazi ya mamba, hivyo kukamilika kwake kutaokoa
maisha ya watu pamoja na kurahisisha usafiri wa watu na bidhaa.
Katika hatua nyingine,
Waziri Mkuu amesema changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na
salama katika vijiji vya Litama, Luchelegwa, Nandanga, Ipingo na Chiapi
kuwa historia baada kuungwanishwa na mradi wa maji wa Mbwinji.
Ameyasema
hayo leo wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wa vijiji
vya Litama, Chiapi, Nandanga, Luchelegwa alipowasili wilayani Ruangwa
akiwa katika siku ya pili ya ziara yake ya kikazi ya siku nne Mkoani
Lindi.
Waziri
Mkuu amesema Serikali inatekeleza Kampeni yake ya kumtua mama ndoo,
hivyo itahakikisha wananchi katika maeneo yote nchini, hususan ni ya
vijijini wanapata huduma ya maji safi na salama katika umbali usiozidi
mita 400.
Ameitoa
kauli hiyo baada ya wananchi wa vijiji hivyo kumueleza changamoto
mbalimbali zinazowakabili kwenye maeneo yao zikiwemo za maji, barabara,
umeme, ambapo aliwahakikishia kwamba Serikali imeshaanza kuboresha
huduma hizo.
Wakati
huo huo, Waziri Mkuu amezindua Zahanati ya Nandanga ambayo imejengwa
kwa fedha kutoka mfuko wa jimbo umegaharimu kiasi cha sh. milioni 73.47
na kuwahakikishia kwamba Serikali itawapelekea wataalam wa kutosha ili
kuwahudumia.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akikagua mradi wa daraja la
Likuledi, linalo unganisha Wilaya ya Ruangwa na Wilaya ya Masasi, kutoka kwa
Mhandisi Josam Mlaki, kwenye ziara ya kikazi ya siku nne Mkoani Lindi, Julai 11, 2017. (Picha
na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akipata maelezo ya mradi wa daraja la Likuledi, linalo unganisha Wilaya ya Ruangwa na Wilaya ya Masasi, kutoka kwa Mhandisi Josam Mlaki, kwenye ziara ya kikazi ya siku nne Mkoani Lindi, Julai 11, 2017. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)


No comments :
Post a Comment