Naibu Waziri Ofisi ya Rais, (TAMISEMI), Mhe. Selemani Jafo
akikagua chumba cha upasuaji kilichopo katika moja ya kituo cha Afya wilayani
Ukerewe, mkoani Mwanza Julai 30, 2017
NA K-VIS BLOG, UKEREWE
NAIBU Waziri Ofisi ya Rais Tamisemi Selemani Jafo amewajia juu
Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya(DMO), Afisa Manunuzi, na mwakilishi wa Mweka hazina
wa halmashauri ya wilaya ya ukerewe baada ya kushindwa kutoa ufafanuzi sahihi
juu ya ununuzi wa dawa chini ya mfuko wa Afya wa pamoja (Busket Fund).
Akiwa katika ziara yake ya kukagua miradi mbalimbali ya
maendeleo wilayani humo, Jafo amefika kwenye hospitali ya wilaya ya ukerewe na
kuwaomba wananchi waliokuwepo hospitalini hapo kueleza changamoto wanazozipata
wanapofika hospitalini hapo.
Kufuatia changamoto walizoeleza wananchi, Jafo alionyesha
kukerwa kutokana na maafisa hao kushindwa kujibu hoja ya wananchi waliokuwa
wakilalamika kwamba wanapofika kwenye hospitali hiyo mara nyingi wataalam
wamekuwa na kauli mbaya sambasamba na kukosa dawa.
Jafo aliwageukia wataalam hao kwa kuwauliza ni kiasi gani cha
fedha za basket fund wamepokea kwa mwaka Fedha 2016/2017 na kiasi gani
kilitumika kununua dawa na vifaa tiba.
Kutokana na Jafo kuhoji fedha hizo, wataalam hao wote
walishindwa kufahamu, jambo lililomkera Naibu Waziri Jafo.
Alisema ameshangazwa na kitendo cha wataalam wahusika kushindwa
kutambua mambo ya msingi ambayo wanapaswa kuyasimamia ili kutatua kero ya afya
kwa wananchi.
Jafo aliwajulisha wananchi kuwa halmashauri yao imepokea jumla
ya sh.milioni 727.4 ambapo 33% ilipaswa kununulia dawa na vifaa tiba.
Naibu Waziri Jafo amewataka watumishi wote kusimamia mipango ya
serikali ili kutatua kero za wananchi ili kuleta maendeleo katika jamii.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jafo akiwa katika picha ya pamoja na wataalam wa Afya wilayani Ukerewe




No comments :
Post a Comment