Waziri
wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, (kushoto), akisikiliza kero za
wananchi wakati alipofanya ziara ya kushtukiza kwenye ofisi za Mamlaka
ya Mapato Tanzania, (TRA), huko Vingunguti jijini Dar es Salaam, leo
Julai 11, 2017, kujionea jinsi Mamlaka hiyo inavyowahudumia wananchi
waliojitokeza kulipia kodi ya majengo. TRA imesogeza mbele zoezi hilo la
ulipaji kodi ya majengo hadi Julai 15, 2017 ili kuwawezesha wananchi
kufanya hivyo.
NA BENNY MWAIPAJA,
WFM, DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, amefanya ziara
ya kushitukiza katika Ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA, eneo la
Vingunguti Jijini Dar es Salaam leo Julai 11, 2017 na kuagiza kuongezwa kwa wafanyakazi na
vitendea kazi katika ofisi hiyo baada ya kukuta msongamano mkubwa wa watu
waliojitokeza kulipa kodi ya majengo.
Dkt. Mpango ambaye alitumia muda wake mwingi kusikiliza kero za
baadhi ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam waliojitokeza kwa wingi kulipa kodi
hiyo, ameiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania kuongeza wafanyakazi kumi pamoja na
mashine za kieletroniki za kukusanyia kodi pamoja na kuweka utaratibu mzuri wa
kuwahudumia wazee na watu wenye ulemavu.
“Nimeagiza wafanyakazi waongezwe, viti 50 kwa ajili ya kutumiwa
na wazee pamoja na akina mama wenye watoto vitaletwa, pamoja na kuongeza
mashine za kielektroniki 5 kutoka 3 zilizokuwepo ambapo sasa zitakuwa mashine
8, hatua hii itaondoa changamoto hii” alifafanua Dkt. Mpango
Amerejea pongezi zake kwa Watanzania kwa kujitokeza kwa wingi
kila mahali nchini kote kulipa kodi ya majengo akikielezea kitendo hicho kuwa
ni cha kizalendo na kitaisaidia nchi kuondokana na umasikini kwa kuwa itakuwa
na uwezo wa kuwahudumia wananchi wake kikamilifu.
Dkt. Mpango amewahakikishia Wazee waliotimiza umri wa kuanzia
miaka 60 na kuendelea kwamba Serikali imewaondolea kodi ya majengo kwenye
nyumba zao wanazoishi kutokana na kutambua mchango wao mkubwa katika
kulitumikia Taifa wakati wa ujana wao.
Baadhi ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam waliojitokeza kulipa
kodi katika Ofisi hiyo ya TRA, Vingunguti, wamepongeza utaratibu wa Waziri wa
Fedha na Mipango, Dkt Philip Mpango wa kuwajibika na kutumia muda wake
kuwatembelea na kuwahudumia wananchi na pia wamemmwagia sifa kem kem Rais Dkt.
John Pombe Magufuli kwa hamasa kubwa aliyowapa na kwamba wako tayari kumuunga
mkono kwa hali na mali ili nchi ipate maendeleo kwa haraka
Hii ni siku ya pili kwa Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt.
Philip Mpango kufanya ziara za kushitukiza katika maeneo muhimu kwa lengo la
kuangalia utaratibu wa ulipaji kodi mbalimbali hususan ya majengo na vituo vya
mafuta ili kubaini kasoro mbalimbali na kutoa maelekezo masuala muhimu
anayoyabaini ambapo jana alikuwa Kigamboni, Jijini Dar es Salaam.
Dkt. Mpango (kushoto), akizunguzma na afisa kodi wakati wa ziara hiyo
Waziri Dkt. Mpango, akizungumza na wananchi walipa kodi kwenye ofisi za TRA Vingunguti jijini Dar es Salaam.
Kamishna Mkuu wa TRA, Bw. Charles Edward Kichere(kulia), akiangalia jinsi watendaji wake wanavyowahudumia wananchi.
Kamishna Mkuu wa TRA, Bw. Charles Edward Kichere(kushoto), akizunhumza na mwananchi aliyefika kulipia kodi ya majengo.
Waziri Dkt. Mpango, akizungumza na wananchi walipa kodi kwenye ofisi za TRA Vingunguti jijini Dar es Salaam.
Dkt. Mpango akiondoka ofisi za TRA Vingunguti jijini Dar es Salaam, baada ya ziara yake
| Dkt. Mpango akiondoka ofisi za TRA Vingunguti jijini Dar es Salaam, baada ya ziara yake |
No comments :
Post a Comment