Naibu
Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani, (mwenye suti ya
bluu) akicheza pamoja na kikundi cha ngoma za asili kutoka katika kijiji
cha Rwabigaga wilayani Kyerwa mkoani Kagera kabla ya uzinduzi wa Mradi
wa Usambazaji wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA III) uliofanyika
mkoani humo mapema Julai 11, 2017
Naibu
Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani (katikati) akikata
utepe kuashiria uzinduzi wa Mradi wa Usambazaji wa Umeme Vijijini Awamu
ya Tatu (REA III) katika mkoa wa Kagera uliofanyika katika kijiji cha
Rwabigaga wilayani Kyerwa. Kulia kabisa ni Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa
Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga
Naibu
Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani (katikati) akibonyeza
kitufe kuashiria uzinduzi wa Mradi wa Usambazaji wa Umeme Vijijini
Awamu ya Tatu (REA III) katika mkoa wa Kagera uliofanyika katika kijiji
cha Rwabigaga wilayani Kyerwa. Kulia kabisa ni Mkurugenzi Mkuu wa
Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga na
kushoto ni Mbunge wa Kyerwa, Innocent Bilakwate.
Waliosimama
( kuanzia wa pili kutoka kulia mbele), Mbunge wa Kyerwa, Innocent
Bilakwate, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani, Mkuu
wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali Mstaafu Salum Kijuu na Mwenyekiti wa
Bodi ya Nishati Vijijini, Dkt. Gideon Kaunda wakiwa katika picha ya
pamoja na wanakijiji wa Rwabigaga wilayani Kyerwa mkoani Kagera mara
baada ya kumalizika kwa uzinduzi wa Mradi wa Usambazaji wa Umeme
Vijijini Awamu ya Tatu (REA III) katika mkoa wa Kagera uliofanyika
kijijini hapo mapema Julai 11, 2017
Mbunge
wa Kyerwa, Innocent Bilakwate akielezea hali ya upatikanaji wa nishati
ya umeme katika wilaya ya Kyerwa kwenye uzinduzi huo.
Mkurugenzi
Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga,
akielezea utekelezaji wa Mradi wa Usambazaji wa Umeme Vijijini Awamu ya
Tatu (REA III) kwenye uzinduzi huo.
Waliokaa
meza kuu mbele kutoka kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali
Mstaafu, Salum Kijuu, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard
Kalemani, Mbunge wa Kyerwa, Innocent Bilakwate pamoja na watendaji
wengine kutoka serikalini, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na
wakandarasi wakifuatilia maelezo yaliyokuwa yanatolewa na Mkurugenzi
Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga
(hayupo pichani) kwenye uzinduzi huo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini, Dkt. Gideon Kaunda akisisitiza jambo kwenye uzinduzi huo.
Sehemu
ya Mameneja kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) katika wilaya za
Karagwe, Ngara, Misenyi, Muleba na Biharamulo wakifuatilia hotuba ya
uzinduzi iliyokuwa inatolewa na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt.
Medard Kalemani (hayupo pichani) kwenye uzinduzi huo.
Sehemu
ya wananchi wa kijiji cha Rwabigaga wilayani Kyerwa mkoani Kagera
wakishangilia hotuba iliyokuwa inatolewa na Naibu Waziri wa Nishati na
Madini, Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani) kwenye uzinduzi huo.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani akisisitiza jambo kwenye uzinduzi huo.
Naibu
Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani (kushoto) akitoa
maelekezo kwa wakandarasi na wa watendaji kutoka Shirika la Umeme
Tanzania (TANESCO) (kulia) kwenye uzinduzi huo.
……………………………………………………………..
Na Greyson Mwase, Kagera
Naibu
Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani amesema vijiji na
vitongoji vyote vya mkoa wa Kagera vinatarajiwa kupata umeme wa uhakika
ifikapo mwaka 2021 kama sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa Usambazaji wa
Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA III)
Dkt.
Kalemani aliyasema hayo mapema Julai 11, 2017 kwenye hafla ya uzinduzi
wa Mradi wa Usambazaji wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA III)
utakaosimamiwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) iliyofanyika katika
kijiji cha Rwabigaga wilayani Kyerwa mkoani Kagera pamoja na
kumtambulisha mkandarasi atakayefanya ujenzi wa sehemu ya kwanza ya
mradi katika mkoa huo.
Alisema
utekelezaji wa Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu
katika mkoa wa Kagera utahusisha vipengele vitatu ambavyo ni pamoja na
kusambaza umeme katika maeneo ambayo hayajafikiwa kabisa na miundombinu
ya umeme na kuongeza wigo wa usambazaji umeme katika vijiji ambavyo
vimefikiwa na miundombinu ya umeme lakini baadhi ya maeneo na vitongoji
havikuungwa.
Waziri
Kalemani alisema kipengele cha tatu kinahusisha usambazaji wa umeme
utokanao na vyanzo vya nishati jadidifu kwenye maeneo yaliyo mbali na
gridi hususan visiwani.
Aliendelea
kusema kuwa utekelezaji wa mradi huu utatekelezwa kwa vipindi viwili
tofauti ambapo sehemu ya awali itahusisha upelekaji umeme katika
vijiji 141 kwa gharama ya shilingi bilioni 45.43 na kuongeza kuwa
utekelezaji wa sehemu ya kwanza ulianza tangu mwezi Februari mwaka huu
ambapo inatarajiwa kukamilika mapema Aprili, 2019
Alieleza
kuwa kazi hii itafanywa na mkandarasi ambaye ni kampuni ya M/S Nakuroi
Investment Company Limited na kuongeza kuwa sehemu ya pili ya mradi
huu wa kusambaza umeme vijijini kwa vijiji 180 vilivyobakia utaanza
kutekelezwa baada ya sehemu ya kwanza kukamilika mwaka 2019, hivyo
kufikisha umeme katika vijiji vyote vya mkoa wa Kagera ifikapo mwaka
2021.
Dkt.
Kalemani aliwaomba wananchi kutumia fursa ya umeme wa uhakika kwa
kuboresha maisha yao kupitia miradi ya uzalishaji mali pamoja na huduma
mbalimbali za jamii ili uwekezaji huu wa Serikali ulete manufaa
yaliyokusudiwa kwa wananchi.
“Wananchi
sasa ninawaomba mtumie fursa hii ya umeme wa uhakika kwa kujenga
viwanda vya kusindika mazao pamoja na huduma za afya, elimu, maji,
kilimo na viwanda vingine, mashine za kusaga, useremala, kuhifadhi
vinywaji na vyakula pamoja na kuchomelea vyuma shughuli ambazo
zitawapatia kipato na kuboresha maisha yenu,” alisisitiza Dkt. Kalemani.
Aidha,
Dkt. Kalemani aliwataka wananchi watakaounganishwa na huduma ya umeme
kukamilisha utandazaji wa nyaya katika nyumba zao mapema ili mkandarasi
atakapofika katika maeneo yao wawe tayari kulipia na kuunganishiwa na
huduma ya umeme.
Aliongeza
kuwa, wananchi ambao nyumba zao si kubwa sana wanahimizwa kuomba
kufungiwa kifaa maalum kijulikanacho kama Umeme Tayari (UMETA) ambacho
hakihitaji kutandaza nyaya katika nyumba.
Waziri
Kalemani aliwaomba wananchi kutoa maeneo yao kwa ajili ya kupitisha
miundombinu ya umeme bila ya kudai fidia kama mchango wao kwenye mradi
huu na kuwezesha fedha iliyotengwa kuunganisha wateja wengi zaidi.
Katika
hatua nyingine, Dkt Kalemani aliagiza Shirika la Umeme Tanzania
(TANESCO) katika mkoa wa Kagera kusogeza huduma karibu na wananchi wa
wilaya ya Kyerwa ili kuepuka gharama ya kufuata huduma mbali.
Wakati
huo huo akielezea kwa kifupi Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini
Awamu ya Tatu, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA)
Mhandisi Gissima Nyamo- Hanga, alisema mradi unalenga kufikisha huduma
ya umeme kwenye vijiji 7,873 katika wilaya na mikoa yote Tanzania
Bara ambavyo bado havijafikiwa na huduma ya umeme.
Alisema
kwa mujibu wa taarifa ya maeneo rasmi ya kiserikali kutoka Ofisi ya
Rais –Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Tanzania Bara
ina vijiji 12,268 ambapo vijiji vilivyofikiwa na umeme hadi Juni, 2016
vilikuwa ni 4,395 sawa na asilimia 36.
Mhandisi
Nyamo-Hanga aliongeza kuwa kati ya vijiji 7,873 ambavyo havijapata
umeme, vijiji 7,697 vimepangwa kupatiwa umeme wa gridi na vijiji 176
pamoja na visiwa vitapatiwa umeme wa nje ya gridi kwa kuwa ndiyo njia
muafaka ya kuvipatia umeme kwa sasa na kusisitiza kuwa mradi huu
umepangwa kutekelezwa katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka wa
fedha 2016/17 hadi 2020/21.
No comments :
Post a Comment