Afisa Mwandamizi wa Idara ya
Fedha za Nje, Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Said Nyenge (kulia)
akimuongoza Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika-AfDB,
Kanda ya Afrika Mashariki Dkt. Nyamajeje Weggoro, alipowasili Wizara ya
Fedha na Mipango kukutana na Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Dkt.
Ashatu Kijaji (Mb), Jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Wizara ya Fedha
na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (kulia) akisikiliza kwa makini
maelezo ya Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika-AfDB,
Kanda ya Afrika Mashariki Dkt. Nyamajeje Weggoro (hayupo pichani) kuhusu
ushirikiano mzuri na Benki hiyo katika Maendeleo ya kiuchumi nchini
Tanzania, Makao Makuu ya Wizara ya Fedha, Jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Wizara ya Fedha
na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) akizungumza na Mkurugenzi
Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika Kanda ya Afrika Mashariki, Dkt.
Nyamajeje Weggoro (hayupo pichani) alipokutana naye ofisini kwake
Jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango,
Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (kulia), akiishukuru Benki ya Maendeleo ya
Afrika, AfDB, kwa namna inavyoshirikiana na Tanzania kukuza uchumi
wake, wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa
Benki hiyo anayesimamia Kanda ya Afrika Mashariki, Dkt. Nyamajeje
Weggoro, Jijini Dar es Salaam
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya
Maendeleo ya Afrika-AfDB, Kanda ya Afrika Mashariki, Dkt. Nyamajeje
Weggoro, akizungumza namna Benki yake itakavyofadhili ujenzi wa Reli ya
Kati kwa kiwando cha Kimataifa (Standard gauge) pamoja na kuhuisha
Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania-TANESCO, alipokutana na kufanya
mazungumzo na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji
(Mb) (hayupo pichani), Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya
Maendeleo ya Afrika-AfDB, anayehudumia Kanda ya Afrika, Dkt. Nyamajeje
Weggoro (katikati) akimwonesha Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe.
Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), zawadi ya picha, baada ya kumalizika kwa
mazungumzo yao, Jijini, Dar es Salaam
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya
Maendeleo ya Afrika Kanda ya Afrika Mashariki Dkt. Nyamajeje Weggoro
(kushoto) na Naibu Waziri wa Wizara ya Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu
Kijaji (Mb) (wa pili kushoto) na Afisa Mwandamizi toka AfDB na Idara ya
Fedha za Nje, wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kumalizika kwa
mkutano kati yao Jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Wizara ya Fedha
na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (kulia) akiwa ameongozana na
mgeni wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika Kanda ya
Afrika Mashariki Dkt. Nyamajeje Weggoro (kushoto) mara baada ya
kumalizika kwa...
mkutano kati yao, Jijini Dar es Salaam.
……………………………………………………………………
Benny Mwaipaja, WFM, Dar es Salaam
Benki ya Maendeleo ya Afrika
(AfDB) imeahidi kushirikiana na Tanzania kujenga mradi mkubwa wa Reli ya
Kati kwa kiwango cha Kimataifa (SGR) kwa kuipatia mkopo wenye masharti
nafuu.
Ahadi hiyo imetolewa Jijini Dar
es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo anayesimamia kanda ya
Afrika Mashariki, Dkt. Nyamajeje Weggoro, alipokutana na kufanya
mazungumzo na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji.
Dkt. Weggoro amesema kuwa Benki
yake imeridhika na utendajikazi wa Serikali ya Awamu ya Tano ikiongozwa
na Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli na hivyo kuifanya Bodi ya
Wakurugenzi ya Benki hiyo kukubali kufanikisha ujenzi wa Reli hiyo kwa
ajili ya maendeleo ya nchi.
Amesema kuwa Reli ya Kati kwa
Kiwango cha Kimataifa ni muhimu kwa uchumi wa Taifa lakini pia kwa
uchumi wa nchi za Maziwa Makuu kwa kuunganisha nchi kama vile Rwanda,
Burundi, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na baadae
itaunganishwa na Reli ya Kaskazini upande wa Kenya.
“Benki iko tayari na inasubiri
Tanzania ilete mapendekezo ama maombi ili yafanyiwekazi, tutakaa pamoja
ili tuone Benki itasaidia kiasi gani na Benki pia inaweza kuwatafuta
wadau wengine tunaosaidiana nao katika miradi mikubwa kama hii”
Aliongeza Dkt. Weggoro
Mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kati
kwa kiwango cha Kimataifa (Standard gauge), yenye urefu wa kilometa
2,561 umepangwa kugharimu kiasi cha Dola bilioni 7.6 za Marekani, sawa
na shilingi za Kitanzania Trilioni 16, awamu ya kwanza imeanza kujengwa
kuanzia Dar es Salaam hadi Morogoro na baadae awamu nyingine zitafuata.
Aidha, Dkt. Weggoro amesema Benki
yake itashirikiana na Serikali kuboresha utendajikazi wa Shirika la
Umeme Tanzania (TANESCO) hasa upande wa muundo wake na madeni makubwa
yanayolikabili shirika hilo ili liweze kuchangia ipasavyo ukuaji wa
uchumi wa viwanda.
“Benki itatoa fedha ili kulifanya
shirika hilo lifanyekazi kwa ufanisi zaidi, tunajadiliana na
tutawashirikisha pia wadau wengine zaidi ili uamuzi wa Serikali wa
kuifanya nchi iwe ya viwanda uweze kufanikiwa” Alifafanua Dkt. Weggoro
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango,
Dkt. Ashatu Kujaji, ameishukuru AfDB kwakuwa mshirika mkubwa wa
kimkakati wa maendeleo kwa kusaidia miradi mbalimbali ikiwemo barabara,
nishati ya umeme, kilimo na huduma za jamii.
Dkt. Kijaji amesema kuwa
uwekezaji wa AfDB hapa nchini umefikia Dola bilioni 1.8 huku asilimia
74.5 za uwekezaji huo iko kwenye sekta ya miundombinu, ambapo barabara
imechukua asilimia 51.4, Nishati (10.1%), Maji na Usafi wa Mazingira
(13%) na Sekta nyingine za huduma za jamii, kilimo na masuala ya fedha
(25.5%).
Amesema kuwa uamuzi wa Benki hiyo
kuamua kusaidia ujenzi wa mradi mkubwa wa Reli ya Kati kwa kiwango cha
Kimataifa (SGR) pamoja na kuihuisha TANESCO ni hatua muhimu
itakayochochea ukuaji haraka wa uchumi wa nchi.
Ameitaja miradi mingine ya
kimkakati iliyotekelezwa kupitia msaada na mkopo nafuu kutoka Benki hiyo
kuwa ni ujenzi wa barabara ya lami inayoanzia Afrika
Kusini-Cairo-Misri-Tanzania, kuanzia mkoani Iringa, Dodoma hadi Babati
mkoani Manyara, inayotarajiwa kukamilika katika kipindi cha takriban
miezi miwili ijayo.
No comments :
Post a Comment