Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na
Mbunge wa Ruangwa, akiweka mchanga kwenye kaburi la aliyekuwa Diwani
wa CCM Kata ya Mnacho ,Kijij cha Nandagala , Bw. Daniel Petro Mtawa
ambaye amefariki tarehe May 7,2017 na kuzikwa kijijini kwake
Nandagala Wilaya ya Ruangwa Mkoani Lindi May 8 ,2017. (PICHA NA OWM)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
akitoa salamu za Pole Katika Msiba kwa aliyekuwa Diwani wa CCM Kata
ya Mnacho ,Kijij cha Nandagala , Bw. Daniel Petro Mtawa aliyefariki
tarehe May 7,2017 na kuzikwa kijijini kwake Nandagala Wilaya ya
Ruangwa Mkoani Lindi May 8 ,2017. (PICHA NA OWM)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
akiwa ameongozana na Viongozi wa Mkoa wa Lindi na Mtwara pamoja na
wananchi kuelekea makaburini kwa ajili ya mazishi ya aliyekuwa Diwani
wa CCM Kata ya Mnacho, Kijiji cha Nandagala , Bw. Daniel Petro Mtawa
aliyefariki tarehe May 7,2017 na kuzikwa kijijini kwake Nandagala
Wilaya ya Ruangwa Mkoani Lindi May 8,2017. Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa
Mtwara, Bi. Halima Dendego na wa pili kulia, ni Mkuu wa Mkoa wa
Lindi, Bw. Godfrey Zambi. Kushoto ni Kaimu Mkuu wa Wilaya ya
Ruangwa , Bi. Rukia Mhango. (PICHA NA OWM)
……………………………………………………………
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
ameongoza mamia ya wakazi wa kata ya Mnacho, wilayani Ruangwa kwenye
mazishi ya aliyekuwa diwani wa kata hiyo, Bw. Daniel Mtawa ambaye
alifariki dunia Mei 7, 2017.
Akizungumza na waombolezaji
katika ibada ya mazishi iliyofanyika kwenye kijiji cha Nandagala,
wilayani Ruangwa, mkoani Lindi jana (Jumatatu, Mei 8, 2017), Waziri Mkuu
alisema msiba uliowapata wana-Mnacho ni mkubwa, na akatumia fursa hiyo
kuwapa pole wanafamilia na wanakijiji wenzake.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Ruangwa, anatoka katika kijiji cha
Nandagala, kwenye kata hiyohiyo ya Mnacho.
Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo
kufikisha salamu za rambirambi ambazo zilitolewa na Mheshimiwa Rais, Dk.
John Pombe Magufuli pamoja na Mheshimiwa Makamu wa Rais, Samia Suluhu
Hassan. “Mheshimiwa Rais ametoa salamu za pole kwa mke wa marehemu,
familia na wana-Ruangwa wote. Pia Mheshimiwa Makamu wa Rais, anawapa
pole wana-Ruangwa wote kwa msiba huu mzito,” aliongeza.
“Ndugu yetu Mtawa amemaliza
safari yake na ametangulia mbele ya haki. Tuendelee kumuombea marehemu
Mtawa, kila mtu kwa imani yake. Ninatoa pole kwa familia, kwa Mwenyekiti
wa Halmashauri na madiwani wenzangu wote,” alisema.
Akitoa salamu za rambirambi,
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Ruangwa, Bw. Rashid Nakumbya, alisema Bw.
Mtawa alikuwa diwani wa kata hiyo tangu mwaka 2015 lakini alianza kupata
tatizo la shinikizo la damu Desemba mwaka jana. “Alilazwa katika
hospitali ya Nyangao kwa mwezi mmoja, na baadaye akahamishiwa Hospitali
ya Taifa Muhimbili ambako alilazwa kwa miezi miwili kabla ya kupata
nafuu na kuruhusiwa kurudi nyumbani kuendelea na dawa,” alisema.
Marehemu Mtawa ameacha mjane, watoto saba (wa kiume watano na wa kike wawili) na wajukuu wanane.
Kwa upande wake, Mwinjilisti
Sebastian Francis wa Kanisa la Anglikana Ruangwa alisema mshahara wa
dhambi ni mauti na akawataka waombolezaji wote kila mmoja kwa imani yake
wajiepushe na anasa za dunia ili waweze kuurithi ufalme wa mbinguni.
“Baada ya kifo yapo maisha na Bw.
Daniel Mtawa amemaliza safari yake, lakini je mimi na wewe tumejiandaa
vipi kufika mwisho wa safari yetu? Ndugu zangu, maisha ya starehe na
anasa yasitufanye tuukose ufalme wa Mbinguni,” alisema.
Akitoa mfano kutoka kitabu cha
Luka (16:19-31) wa Lazaro maskini ambaye alikuwa akiomba chakula lakini
hapewi hadi kutamani makombo kutoka kwa tajiri, Mwinjilisti Francis
alisema wanadamu tunapaswa kubadilika na kujaliana.
“Huu mfano unaonyesha kuwa hakuna
aliyemjali wala hakuna aliyemhudumia yule maskini. Tunafundishwa kuwa
watu wa kuhurumiana na kujaliana bila kujali dini, rangi au kabila la
mtu,” alisisitiza.
Waziri Mkuu alirejea Dodoma jana usiku kuendelea na ratiba za vikao vya Bunge
No comments :
Post a Comment