Tuesday, May 9, 2017

WACHIMBAJI 3000 KUNUFAIKA AJIRA KATIKA MACHIMBO YA KITUNDA Profesa-Sospeter-Muhongo

Profesa-Sospeter-Muhongo
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Mhongo
 
NA TIGANYA VINCENT-MAELEZO, TABORA
Waziri wa Nishati na Madini  Profesa Sospeter  Muhongo amevitaka vikundi  vyote vilivyopewa leseni ya kuanza uchimbaji mdogo mdogo wa madini ya dhahabu katika eneo la Kitunda wilayani Sikonge kuhakikisha vinatoa ajira kwa wachimbaji 3000 walipo katika eneo hilo.
Waziri ametoa agizo hilo  jana wilayani Sikonge katika eneo la Kitunda ,wakati yeye na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Tabora alipotembelea eneo lililosababisha vifo vya wachimbaji saba wa madini kwa ajili ya kujionea na kutoa pole kwa wananchi wa eneo hilo.
Alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliahidi wakati ikiomba kura kwa wananchi ya kuwashika mkono wachimbaji wadogo wadogo na kwa kuwa neema hiyo imepatikana hapo ni vema vijana wengi wa eneo hilo wenye nia ya kushiriki katika uchimbaji wa madini wakanufaika na ajira.
Hivyo ,Profesa Muhongo alisema kuwa ni vema kila Kikundi kilichopewa leseni na kibali cha kuanza uchimbaji mdogo mdogo kikaandaa orodha ya majina ya vijana ambayo kitawaajiri katika mgodi wao ili Serikali ijue na iwe na idadi kamili wanaofanyakazi katika eneo lao na kwa ajili ya usalama.
“Kila mgodi uwe na majina ya watu wanaotaka kuwaajiri na orodha hiyo ifike kwa Mkuu wa Mkoa , Maafisa wa Madini wa Kanda ikiwa imeonyesha jina la kila moja na  idadi yao…hatuwezi kuwacha vijana hawa wote bila ajira”alisisitiza Waziri huyo.
Kufuatia hatua hiyo alimuomba Mkuu wa Mkoa wa Tabora Bw. Aggrey Mwanri na timu yake kuhakikisha wanasimamia zoezi la orodheshaji wachimbaji wote waliopo katika eneo hilo na kuwagawa katika vikundi vya Kapumpa, Winima, Gold Stone na Mawina kwa lengo la kuhakikisha kuwa kila mtu anapata sehemu ya kufanyia kazi na anafanyakazi katika eneo salama.
Hatua hiyo inalenga kuondoa tabia za baadhi ya wachimbaji hao kuvamia maeneo ya wengine na hivyo kuhatarisha maisha yao nay a wengine.
Alitoa agalizo watu wote wanaomiliki leseni , wachimbaji na wataosimamia zoezi hilo kuhakikisha hakuna jina litakalojitokeza katika kundi zaidi ya moja na kuongeza kuwa ni vema mtu akafanyakazi katika kundi moja.
Profesa Muhongo alisema kuwa kuhusu suala la malipo ni juu yao kufuatia taratibu watakazojiwekea.
Katika hatua nyingine Waziri huyo ametoa siku tatu kwa Maafisa wa Madini wa Kanda kuhakikisha  wanakamilisha haraka taratibu zinatakiwa iwemo kuwa watu wa mazingira, upimaji wa mashimo kwa umbali unaotakiwa na upangaji wa wachimbaji hao kulingana na vikundi vinne vilivyopewa leseni katika eneo hilo.
Alisema kuwa baada ya hapo Mkaguzi Mkuu wa Madini atapitia na kuona kama taratibu zote za usalama zimezingatiwa katika eneo hilo na ndipo  Serikali itakaporuhusu zoezi hilo kuanza tena uchimbaji wa dhahabu katika machimbo hayo.
Kwa upande wa wachimbaji wadogo wadogo katika eneo hilo wamemuomba Waziri huyo kuharakisha kuwaondolea zuio la kuchimba madini kwa kuwa walitegemea kazi hiyo kama chanzo cha mapato kwa ajili ya matumizi yao na familia zao.
Walisema kuwa kwa kipindi ambacho wamekuwa hawachimbi wamekuwa na maisha magumu kwa sababu hawana chanzo kingine cha mapato.
Wakati huo huo wachimbaji hao wamemuhakikishia Waziri wa Nishati na Madini Profesa Muhongo kuwa ni watu saba tu ndio waliofariki katika eneo hilo na sivyo zaidi ya hao.
Walitoa ufafanuzi kuwa watano walikufa pale pale kwa kufikiwa na kifusi katika eneo linalomikiwa na moja alifariki wakati akiendelea na matibabu hospitali na mwingine alifariki kwa kukosa hewa.
Kwa upande wa Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda Kati Magharibi Salim Salim alisema kuwa ili kuhakikisha maafa mengine hayatokei, kabla ya kuanza tena uchimbaji katika eneo hilo Ofisi ya Kanda kwa kushirikiana na Afisa Mkazi wa Madini wameshaanza kusimamia zoezi la kuhakikisha mashimo ya uchimbaji wa dhahabu yanakuwa wa kuanzia mita 15 toka moja kwenda jingine.
Bw. Salim aliongeza kuwa hatua nyingine ni kuhakikisha kuwa kila kiwanja cha uchimbaji kina kuwa na Meneja wa kusimamia Mgodi ambaye atapanga msimamizi wa kila shimo.

No comments :

Post a Comment