Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi
ya Tiba ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI), Dkt. Respicious Boniface
akizungumza na waandishi wa habari wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku
nne kwa madaktari kutoka nchi mbali mbali za Afrika, Kushoto ni Daktari
bingwa wa MOI, Dkt. Edmund Ndalama.Ufunguzi huo umefanyika leo Jijini
Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali
ya Taifa ya Muhimbili, Prof. Lawrence Msiru akiongea na waandishi wa
habari juu ya uendeshaji wa mafunzo hayo leo Jijini Dar es Salaam wakati
wa ufunguzi wa mafunzo ya siku nne kwa madaktari kutoka nchi mbali
mbali za Afrika.
Daktari bingwa wa Mifupa wa
Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI), Dkt. Edmund
Ndalama akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hali ya ajali ilivyo
nchini wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku nne ya madaktari kutoka
nchi mbali mbali za Afrika. Ufunguzi huo umefanyika leo Jijini Dar es
Salaam.
Baadhi ya madaktari kutoka nchi
mbalimbali za Afrika wakisikiliza mafunzo yenye lengo la kubadilishana
ujuzi wa jinsi ya kutibu wagonjwa waliopata ajali. Mafunzo hayo ya siku
nne yameanza leo Jijini Dar es Salaam.
…………………………
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Serikali imetoa jumla ya shilingi
bilioni 13.5 kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa awamu ya tatu wa jengo
jipya la Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI)
linalotegemewa kukamilika na kuanza kutumika kwa asilimia mia moja mwaka
huu.
Hayo yamebainishwa leo Jijini Dar
es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dkt. Respicious Boniface
alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari wakati wa ufunguzi wa
mafunzo ya siku nne ya madaktari kutoka nchi mbali mbali za Afrika.
Dkt. Boniface amesema kuwa
changamoto kubwa inayoikabili taasisi hiyo ni ongezeko la wagonjwa
sababu iliyopelekea kuanzishwa kwa mradi wa ujenzi wa jengo jipya
litakalokuwa na vifaa vya kutosha hivyo kupanua huduma za afya pamoja na
kupunguza gharama za rufaa za wagonjwa kutibiwa nje.
“Awamu ya tatu ya mradi wa ujenzi
wa jengo jipya la MOI ulianza na jumla ya shilingi bilioni 17.9 ambazo
ni fedha za mkopo kutoka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) lakini
fedha hizo hazikuweza kukamilisha ujenzi hivyo tumeongezewa na Serikali
jumla ya bilioni 13.5 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi huo,”alisema Dkt.
Boniface.
Mkurugenzi huyo amemshukuru Rais
Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuwezesha kupatikana kwa fedha hizo ambazo
zitasaidia kumalizika haraka kwa ujenzi wa jengo hilo ambalo litaondoa
changamoto ya kujaa kwa wagonjwa.
Akizungumzia mafunzo hayo ya
madaktari, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Prof.
Lawrence Msiru amesema kuwa huu ni mwaka wa tano tangu mafunzo hayo
yaanze kufanyika nchini ambapo yanashirikisha wakufunzi kutoka MOI
pamoja na Marekani.
“Lengo la mafunzo hayo ni kutoa
elimu ya tiba za majeruhi wa ajali kwa madaktari kutoka nchi mbalimbali
za Afrika zikiwemo za Zimbabwe, Liberia, Sudan,Ethiopia, Namibia na
Malawi yakiwa na nia ya kubadilishana ujuzi wa jinsi ya kutibu wagonjwa
wenye ulemavu na kuzuia vifo,”alisema Prof. Msiru.
Kwa upande wake Daktari bingwa wa
Mifupa MOI, Edmund Ndalama amesema kuwa nchi nyingi bado hazijachukulia
ajali kama ni jambo la kuwekewa msisitizo wakati ajali ni tatizo kubwa
linalopoteza maisha ya watu wengi na kuwaacha wengine wakiwa na vilema
vya maisha.
“Takwimu za Shirika la Afya
Duniani (WHO) zinaonyesha kuwa takribani watu milioni sita wanafariki
kwa ajali kila mwaka na kati ya watu milioni 20 hadi milioni 50 wanabaki
na ulemavu wa maisha, hii ni idadi kubwa ya watu ambayo hata
ukilinganganisha na idadi ya vifo vinavyotokana na magonjwa mengine
havifikii idadi hiyo”, alisema Dkt.Ndalama.
Amemalizia kuwa umefikia muda kwa
madaktari kufahamu njia nyingi zinazohusiana na kutibu magonjwa ya
mifupa yanayosababishwa na ajali ili kupunguza idadi ya vifo vya
wananchi.
No comments :
Post a Comment