Wednesday, May 10, 2017

MJUMBE MAALUM WA AU, RAIS MSTAAFU DKT. JAKAYA KIKWETE AENDELEA KUSAKA AMANI YA LIBYA

Rais Mstaafu wa Awamu ya Nnne, Dkt. Jakaya Kikwete (katikati), ambaye ni Mjumbe Maalum wa Umoja wa Afrika, (AU), katika Mgogoro wa Libya akijadiliana jambo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Congo na Mwenyekiti wa AU Mhe. Jean-Claude Gakosso. (Kushoto) na Mkuu wa Ofisi ya Uwakilishi wa AU kwa Libya Bi. Wahida Ayari .



Rais Mstaafu Dkt Jakaya Kikwete akifanya mazungumzo na Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa katika Mgogoro wa Libya Balozi Martin Kobler jijini Algiers
Rais Mstaafu Dkt Jakaya Kikwete akitoa msimamo wa Umoja wa Afrika kuhusu Mgogoro wa Libya .
Rais Mstaaafu Dkt Jakaya Kikwete akifuatilia Mkutano wa Nchi Majirani wa Libya
NA MWANDISHI MAALUM, ALGIERS



MJUMBE Maalum wa mgogoro nchini Libya, Rais Mstaafu wa awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ameendelea na juhudi zake za usuluhishi wa mgogoro wa nchi hiyo kwa kushiriki katika Kikao cha 11 cha Mawaziri wa zinazopakana na Libya kilichofanyika jijini Algiers, Algeria Mei 8, 2017.

Katika Kikao hicho, Rais Mstaafu amepongeza juhudi zinazoendelea za kupatanisha pande zinazogombana nchini Libya na mafanikio yanayopatikana ikiwemo kuimarika kwa hali ya usalama, kudhibitiwa kwa vitendo vya kigaidi, kuongezeka kwa shughuli za uzalishaji wa mafuta na kufufuliwa kwa mawasiliano kati ya pande zinazohasimiana.
 
 Ameunga mkono jitihada zinazochukuliwa na nchi za Algeria, Misri, Tunisia na UAE katika kuhimiza mazungumzo ya Amani. Amesisitiza umuhimu wa pande mbili za mgogoro kuheshimu Makubaliano ya Amani ya Libya (Libya Political Agreement) na kutekeleza vipengele vyake bila ajizi.

Akiwa jijini Algiers, Rais Mstaafu amefanya pia mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Congo anayemuwakilisha Mwenyekiti wa Kamati wa Wakuu wa Nchi za Umoja wa Afrika kuhusu Libya Mhe Jean-Claude Gakosso na Balozi Martin Kobler, Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa na Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia Mgogoro wa Libya (UNSMIL).

Rais Mstaafu anatarajiwa kumalizia ziara yake nchini Libya kukutana na viongozi wakuu wa pande zinazotofautiana nchini humo.

No comments :

Post a Comment