NA DAUDI MANONGI-MAELEZO, DODOMA.
SERIKALI kupitia Wizara ya Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano
imesema itajenga daraja la juu kwa ajili ya kivuko cha waenda kwa miguu(Over
head Pedestrian Bridge) eneo la Kawe Bondeni.
Hayo yamesemwa Bungeni leo na Naibu Waziri wa Maji na
Umwagiliaji Mhe.Isack Kamwelwe aliyekuwa akijibu swali la Mbunge wa Kawe
Mhe.Halima Mdee kwa Niaba ya Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano.
“Tatizo la kivuko cha waenda kwa miguu eneo la Kawe
Bondeni hadi Jeshini Kata ya Mbezi Juu na Kawe Tayari limeshapatiwa
ufumbuzi”,Aliongeza Mhe.Kamwelwe.
Amesema kwa sasa Mkandarasi wa kujenga daraja hilo yupo
kwenye hatua za maandalizi ya kuanza ujenzi katika eneo hilo muhimu.
Aidha Serikali ina mpango wa kuweka taa za kuongozea
magari katika Barabara ya Mwenge-Tegeta ambapo Mkandarasi ameshapatikana
wa kuweka taa hizo katika makutano ya Afrikana na anatarajia kuanza kazi wakati
wowote.
Mbali na Hayo tatizo la Udogo wa mapokeo na matoleo ya
maji ya mvua yanayosababisha kero katika eneo la Makonde hadi Mbuyuni,Serikali
inakamilisha taratibu za kusaini mkataba wa ujenzi wa mtaro mkubwa eneo la
Mbezi Samaki ambao utatatua kero ya barabara kujaa maji nyakati za mvua.
“Serikali ya Awamu ya Tano ni makini sana na itahakikisha
changamoto hizi inazifanyia kazi ili wananchi waweze kutumia barabara zetu
vyema”Aliongeza Mhe.Kamwelwe.
No comments :
Post a Comment