NA JACQUILINE MRISHO – MAELEZO.
Mfuko
wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umeishauri Serikali kuifanya bima ya
afya iwe lazima kwa kila mwananchi na sio hiari kama ilivyo sasa.
Ushauri
huo umetolewa jana Jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa
Mfuko huo, Benard Konga alipokuwa akizungumza katika kipindi cha
TUNATEKELEZA kinachorushwa hewani na Shirika la Utangazaji Tanzania
(TBC).
“Ifike
wakati suala la bima liwe ni lazima sio hiari na kwamba lengo sio
kukusanya fedha nyingi bali kumpunguzia mwananchi gharama za matibabu na
kuhakikisha mwananchi huyo anapata huduma bora za afya kwa wakati wote
anapohitaji matibabu”alisema Konga.
Konga
alieleza kuwa mpango wa baadae wa Mfuko huo ni kuongeza hamasa
itakayopelekea wananchi wengi zaidi kujiunga na bima za afya ili
kutimiza lengo la kufikia asilimia 75 ya wananchi wote kuwa na bima ya
afya ifikapo mwaka 2020 kutoka asilimia 29 iliyopo hivi sasa.
Kaimu Mkurugenzi huyo, alibainisha kuwa mfuko huo hivi sasa unahudumia zaidi ya asilimia 80 ya wananchi wanaoishi vijijini.
Kwa
upande wa utoaji huduma, Konga alieleza kuwa Mfuko huo umesajili jumla
ya vituo 6600 vinavyotoa huduma kwa bima ya afya pamoja na maduka ya
madawa 200 yanayotoa dawa kwa kutumia bima ya Mfuko huo.
Hata
hivyo, alitoa rai kwa hospitali mbalimbali nchini kuzingatia masharti
na vigezo vilivyowekwa katika utoaji wa huduma za bima na kuepuka tabia
ya kunyanyasa wanachama wa Mfuko huo.
Aidha, amewataka waajiri kuiga mfano wa Serikali katika suala zima la kupeleka kwa wakati michango ya wanachama.
Mfuko
wa Taifa wa Bima ya Afya umeanzishwa mnamo mwaka 1999 baada ya Serikali
kupitisha Sheria ya kuruhusu Mfuko huo ambapo mwaka 2001 ulianza rasmi
kutoa huduma kwa watumishi wa umma. Mwaka huo huo,marekebisho ya sheria
yalifanyika kuruhusu Mfuko huo kutoa huduma kwa wananchi walio katika
sekta zisizo rasmi.
No comments :
Post a Comment