Saturday, May 13, 2017

MAJERUHI WA LUCKY VINCENT WAPATIWA VISA TAYARI KWA SAFARI YA MAREKANI

MBUNGE wa Singida Kaskazini, Mhe.Lazaro Nyalandu amesema Ubalozi wa Marekani umetoa hati ya kusafiria (visa) kwa ajili ya kuwawezesha wanafunzi watatu wa Shule ya Lucky Vincent kupata matibabu nchini Marekani.
Katika ukurasa wake wa Facebook leo Nyalandu amesema waliopata Visa ni wazazi,watoto na wataalamu wawili wa afya ambao watasafiri kwenda Marekani.
"Wote wamepewa visa asubuhi ya leo Ubalozi wa Marekani Dar es Salaam. Akina Mama watatu, watoto wote watatu, na Daktari Moja na Nurse Moja. Kansela wa Ubalozi wa Marekani alinipigia simu asubuhi akiwasubiri katika siku ambayo haikuwa ya kazi,” amesema Nyalandu na kuongeza:
“Mungu ambariki sana kwa moyo huu. Napenda pia kutoa taarifa kuwa ndege yao aina ya DC 8 inatarajiwa kutua Leo usiku saa 2:15 majira ya Afrika Mashariki katika uwanja wa KIA. Mungu wa Watanzania awabariki wote kwa sala na dua zenu kwa ajili ya hawa watoto. Sifa na utukufu kwa Mungu wetu.”
Katika taarifa ya awali kwa vyombo vya habari Nyalandu amesema safari ya kuelekea Marekani itakua kesho asubuhi na ndege itatua Charlotte,New York na kisha wagonjwa pamoja na waliowasindikiza wataingia katika ndege nyingine maalumu ya kubeba wagonjwa hadi katika mji wa Sioux City,Iowa
Watoto hao watatu walijeruhiwa wakati wakiwa katika safari ya masomo wilayani Karatu mkoa wa Arusha jumamosi iliyopita na kusababisha vifo vya wanafunzi 32,walimu wawili na dereva wao.

No comments :

Post a Comment