Wednesday, May 31, 2017

KIFO CHA NDESA PESA: RAIS MAGUFULI, SPIKA WATOA SALAMU ZA RAMBIRAMBI

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma kuhusu msiba huo uliotokea leo ghafla asubuhi, Mhe. Mbowe amesema chama kimempoteza mmoja wa 'makamanda' waliokiasisi na kusimamia agenda za mabadiliko kwa miaka zaidi ya 25 bila kuchoka pamoja na kuwepo vikwazo mbalimbali katika mapambano hayo.
"Nimepokea kwa mshtuko mkubwa taarifa za kifo cha Mhe. Philemon Ndesamburo aliyefariki mapema leo Jumatano Mei 31, 2017, majira ya asubuhi. Ni hudhuni kubwa na maumivu makali yasiyoelezeka kwa kumpoteza Kiongozi na Mzee watu.
"Mzee Ndesamburo ni mmoja wa waasisi wa Chama Chetu cha CHADEMA na siasa za mabadiliko kwa ujumla nchini. Amekuwa Mbunge wa Moshi Mjini kwa miaka 15, ni Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Kilimanjaro na Mjumbe Baraza Kuu la CHADEMA na juzi tu siku ya Jumamosi 27 Mei 2017 alishiriki kikao cha Baraza Kuu mjini Dodoma.
"Leo alikuwa na miadi ya kukutana na Meya wa Jiji la Arusha Mhe. Lazaro Kalist kwa ajili ya kumpatia rambirambi yake kwa watoto wa Shule ya msingi ya Lucky Vincent ya Arusha waliofariki katika ajali mbaya gari hivi karibuni.
"Mstahiki Meya alifika ofisini kwa Mhe. Ndesamburo, ili aandikiwe hundi hiyo, wakati amechukua kalamu aandike hundi hiyo aghafla Mzee wetu akajisikia vibaya akaangua hivyo akalazimika kukimbizwa hospitalini ambapo mauti yalimkuta," amesema Mhe. Mbowe na kuongeza;
"Chama kimempoteza mpambanaji na mpigania ukombozi na mabadiliko ya kweli ndani ya Taifa, alifahamu kupigania na kutafuta haki, uongozi bora na demokrasia katika Taifa letu.
"Kwa niaba ya chama na viongozi wenzangu, natoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki wote bila kusahau wanachama, wapenzi wote wa CHADEMA nchi nzima na Watanzania wote walioguswa na msiba huu mkubwa kwa kumpoteza Kiongozi wetu."
Mhe. Mbowe amesema kuwa katika maisha ya mwanadamu huu ndio wakati mgumu kuliko wote, ambapo ameomba Mwenyezi Mungu awatie nguvu familia ya Mhe. Ndesamburo katika wakati huu mzito wa majonzi ya msiba huo.
Mhe. Mbowe amemuelezea Mzee Ndesamburo kama kiongozi shupavu, jasiri, aliyejiamini.
Ameongeza kuwa ingawa kimwili hatuko nae lakini, hekima, busara na matendo yake yataishi milele yakifanya akumbukwe daima.
Bwana alitoa, Bwana ametwaa. Jina lake lihimidiwe.
Imetolewa na:
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano
CHADEMA

PRESS

No comments :

Post a Comment