Tarehe 24 Novemba 2016 Wizara
ilizindua Cheti kipya cha Chanjo za Kimataifa kijulikanacho kama Cheti
cha Chanjo ya Homa ya Manjano ili kuendana na maboresho ya kipengele cha
7 cha Kanuni za Afya za Kimataifa za mwaka 2005. Lakini pia, zoezi hili
lililenga kukabiliana na kusambaa kwa vyeti vya kugushi (feki) ambavyo
watu wamekuwa wakivipata bila kupata chanjo, hali ambayo ilitishia Afya
ya Jamii dhidi ya ugonjwa huo. Kwasababu hizo, Wizara iliona ni vema
kufanya mabadiliko ya cheti hicho, ambapo wenye vyeti vya zamani
wanabadilishiwa na wale wanaopata chanjo wanapewa cheti kipya.
Wizara inapenda kutoa taarifa ya
utekelezaji wa zoezi hilo kama ifuatavyo. Kabla ya kuanza matumizi ya
vyeti vipya, wastani wa wasafiri 800 walikuwa wanapatiwa chanjo kwa
mwezi kupitia vituo vilivyoruhusiwa na Wizara. Baada ya kuzindua vyeti
vipya na kuongeza udhibiti
wa vyeti feki idadi ya wanaopata chanjo
imeongeza kutoka 800 hadi 2,445 kwa mwezi ikiwa ni ongezeko la mara 3 ya
waliokuwa wanachanja hapo awali. Ongezeko hili limesababishwa na
wasafiri zaidi ya 1,644 kusalimisha vyeti feki kwa mwezi na kuchanjwa na
kupewa vyeti halali.
Kwa ujumla tangu matumizi ya
vyeti vipya vianze mwezi wa Agosti mwaka 2016 mpaka mwezi Machi 2017,
jumla ya wasafiri 19,557 wamepatiwa chanjo ambapo kati yao 13,157
wamesalimisha vyeti feki na kupatiwa chanjo, hii ni sawa na asilimia
67.2. Halikadhalika, watu 11,644 wamebadilisha vyeti vyao halali vya
zamani.
Kupata cheti bila kupata chanjo
ni kosa na kunahatarisha afya yako na Afya ya Jamii, kwani ukienda
katika nchi zenye hatari ya ugonjwa wa homa ya manjano, unaweza
kuambukizwa kwasababu huna kinga na hatimaye kuleta ugonjwa huo nchini.
Vile vile zoezi hili limebaini uwepo wa vituo vinavyotoa chanjo hii bila
kuwa na kibali cha Wizara, hili ni kosa na hivyo ni marafuku kituo
chochote kutoa chanjo hiyo hadi hapo vituo hivyo vitakapopata kibali.
Aidha, kwa wale ambao wananunua au kutoa vyeti bila kupata chanjo nao
wanatenda kosa hivyo, waache mara moja kwani mkono wa sheria utachukua
mkondo wake.
Tarehe 16 Februari 2017 Wizara
ilikumbusha kubadili vyeti vya zamani katika muda uliopangwa yaani
Januari 1 hadi Machi 31, 2017. Kutokana na tathmini tuliyoifanya
imeonekana kuwa watu wengi bado hawajabadili vyeti vya zamani na
kutokana na umuhimu wa zoezi hilo kwa afya ya jamii, tumeamua kuongeza
muda wa mwezi mmoja ili watu wapate nafasi ya kubadili vyeti vyao, hivyo
zoezi hili litaendelea na litaitimishwa tarehe 30.04.2017. Wizara
inatoa wito kwa watu ambao bado wana vyeti vya zamani kufika katika
vituo vya kutolea huduma na kuvibadilisha. Baada ya muda huo kupita
hakutakuwa na muda mwingine wa nyongeza.
Wizara inawakumbusha tena
kuwa ugonjwa wa homa ya manjano haupo nchini ila kwa mujibu wa Shirika
la Afya Duniani, Tanzania ipo katika ukanda wa nchi zenye kiwango kidogo
cha maambukizi ya ugonjwa huo (low risk country). Hata hivyo, tupo
katika hatari ya kuupata ugonjwa huo kutokana na kuzungukwa na nchi
zilizopo kwenye ukanda wa kiwango cha juu cha hatari ya ugonjwa huo
(High risk countries). Hivyo ni jukumu la kila mtu kuhakikisha
tunajilinda dhidi ya ugonjwa huo kuingia nchini.
Ugonjwa huu husambazwa na mbu jike aina ya Aedes
aliye na virusi vya ugonjwa huo. Mpaka sasa duniani hakuna dawa ya
kutibu ugonjwa huo na mgonjwa hupatiwa matibabu ya kupunguza maumivu au
kutibu dalili zinazojitokeza. Njia pekee ya kujikinga na ugonjwa huu ni
kupata chanjo dhidi ya ugonjwa huo. Chanjo hiyo huanza kufanya kazi
kiufasaha siku kumi baada ya mtu kupata chanjo hiyo. Hivyo, nawasihi
wanaosafiri kupata chanjo hiyo angalau siku kumi au zaidi kabla ya
kusafiri kwenda kwenye nchi zenye maambukizi. Aidha, kwa watu wasio na
safari hawahitajiki kupata chanjo hiyo.
Vile vile, kwa wale ambao
hawastahili kupata chanjo kwa sababu za umri (miaka 60 na kuendelea),
wajawazito na watu wenye sababu za kiafya zilizothibitishwa na Daktari,
watapatiwa cheti maalaumu kijulikanacho kama “International Vaccination Exemption certificate” pamoja na kupewa ushauri wa hatua za kiafya za kuchukua dhidi ya kujikinga na ugonjwa huo.
Mwisho, Wizara inapenda
kuwashukuru wale wote walioitikia wito wa zoezi hili la kubadili vyeti
kwani wamefanya hivyo kwa manufaa yao na ya Taifa. Halikadhalika, wale
ambao hawajabadili vyeti vyao watumie muda huu wa nyongeza kufanya
hivyo.
Imetolewa na;
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Afya
21-04-2017.
No comments :
Post a Comment