Meneja
Uhusiano wa Umma wa Jumia Travel nchini Tanzania, Geofrey Kijanga,
akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo wakati wafanyakazi wa kampuni hiyo walipokitembelea Kituo cha kulelea watoto wanaoshi katika mazingira magumu cha Malaika Kids Tanzania na kutoa msaada wa vyakula na vitu mbalimbali kwa ajili ya Sikukuu ya Pasaka. Kituo hicho kipo Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Mwanzilishi
na Ofisa Mtendaji Mkuu wa kituo cha Malaika Kids Reception, Najma Manji
akizungumza na wanahabari kuhusu kituo hicho.
Meneja
Uhusiano wa Umma wa Jumia Travel nchini Tanzania, Geofrey Kijanga
(kulia), akimkabidhi Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kituo hicho msaada huo.
Meneja
Uhusiano wa Umma wa Jumia Travel nchini Tanzania, Geofrey Kijanga
(kulia) akimkabidhi katoni ya sabuni Leila Mustafa anayelelewa katika
kituo hicho
Ofisa kutoka Jumia Travel, Patricia Muthama, akimkabidhi msaada huo, Amina Rodvick anayelelewa kwenye kituo hicho.
Ofisa wa Jumia Travel, Mustafa Ali (kulia), akimkabidhi
msaada huo mtoto, Najma Mohamed
Muonekano wa vitanda vinavyotumiwa na watoto wa kituo hicho.
Kituo hicho kinavyoonekana kwa nje.
Na Dotto Mwaibale
JAMII
imetakiwa kuunga mkono jitihada za kituo cha kulelea watoto wanaoshi
katika mazingira magumu cha Malaika Kids Tanzania kinachopokea watoto,
kuwalea, kuwasomesha na kuwatafutia kazi ili kuweza kujitegemea.
Hayo
yamesemwa na Meneja Uhusiano wa Umma wa Jumia Travel nchini Tanzania,
Geofrey Kijanga Dar es Salaam leo wakati wafanyakazi wa kampuni hiyo
walipokitembelea na kutoa msaada wa vyakula na vitu mbalimbali kwa ajili
ya sikukuu ya Pasaka.
“Kwanza
kabisa ningependa kuchukua fursa hii kuupongeza uongozi wa kituo cha
Malaika Kids Reception kwa jitihada wanazozifanya. Kuanzisha kituo cha
kuwapa hifadhi watoto ambao wanakosa malezi aidha kutokuwa na wazazi,
ndugu au kutelekezwa mitaani kuna changamoto nyingi. Lakini changamoto
hizo zinawezekana endapo tu jamii itaungana kwa pamoja kwa kutoa msaada
wa hali na mali, uwe mdogo au mkubwa ili kuvipa uwezo vituo hivi,”
alisema Kijanga.
“Kuna
usemi unaosema mcheza kwao hutunzwa, nasi kama Jumia Travel Tanzania
tukiwa tunafanyia shughuli zetu eneo hili tumeonelea ni vema kwa kuanza
kusaidia jamii inayotuzunguka kabla ya kwenda mbali zaidi. Tunaunga
mkono juhudi zinazofanywa na kituo hiki kwani hawa watoto wanaolelewa
hapa nao wanatamani wangekuwa wanaishi na familia zao. Kwa kufanya hivi
tunaamini kuwa tutakuwa tunaikumbusha jamii ya watanzania kuwa tatizo la
watoto yatima au wa mitaani lipo na linahitaji nguvu za ziada katika
kupamba nalo,” aliongezea Meneja huyo wa Uhusiano wa Umma kampuni
inayojihusisha na huduma za hoteli kwa njia ya mtandao.
“Ningependa
kutoa wito kwa kampuni nyingine, serikali, watu binafsi na jamii kwa
ujumla kukitupia macho kituo hiki na kuunga mkono jitihada
wanazozifanya. Nilifanya mazungumzo na Mkuu wa kituo hiki na amenieleza
kuwa mbali na kuwalea watoto lakini pia wanawasomesha pamoja na
kuwatafutia ajira ili waweze kuanza maisha yao ya kujitegemea. Hivyo ili
kukipunguzia mzigo kituo hiki, jamii inaweza kusaidia kusomesha baadhi
ya watoto au kuwatafutia kazi wale wanaomaliza masomo yao,” alisema
Kijanga.
Mwanzilishi
na Ofisa Mtendaji Mkuu wa kituo cha Malaika Kids Reception, Najma Manji
amesema kuwa inatia moyo kuona jamii inayozunguka inatambua uwepo wao
na kujitokeza kuwasaidia.
“Kwanza
kabisa ni jambo la kumshukuru Mungu kuona kwamba jamii inayotuzunguka
inatambua jitihada tunazozifanya katika kuwalea watoto wanaoishi katika
mazingira magumu. Hatua ya kuanzisha kituo hiki sikuifanya kana kwamba
ninao uwezo mkubwa, la hasha, bali ni kwa kuguswa tu na magumu
wanayoyapitia watoto hawa wanaokosa msaada. Na huwa najaribu kuvuta
picha kama endapo wangekuwa ni watoto wangu,” alisema Manji.
Akielezea
kwa ufupi shughuli wanazozifanya kituoni hapo pamoja na changamoto
wanazokumbana nazo mwanzilishi wa kituo hiko alisema kuwa, “Mpaka hivi
sasa tunao watoto takribani 80, sina idadi kamili ya wanawake ni wangapi
na wanaume ni wangapi lakini wanaume ni wengi kidogo kuliko wanawake.
Tunawapokea watoto kuanzia miako 0 mpaka 7 kutoka ustawi wa jamii,
hatupendelei watoto wanaozidi umri huo kwani inakuwa ni vigumu
kuwabadili tabia zao.”
“Mbali na
malezi lakini pia tunawasomesha pamoja na kuwatafutia kazi ili waweze
kujitegemea. Kwa mfano, hivi sasa tunao wawili ambao wamekwisha maliza
masomo yao katika masuala ya hoteli lakini bado hawajapata kazi. Na
tayari kuna wengine ambao walishalelewa hapa na kusomeshwa wapo makazini
wakijetegemea na maisha yao. Ningependa kutoa wito kwa watanzania
wenzangu kuja kutusaidia kwa chochote walichonacho iwe ni vyakula, nguo,
vifaa vya shule, kusaidia kulipa ada na hata kuwatafutia au kuwapa kazi
wale wanaohitimu masomo yao ili nao waweze kujitegemea na kuendelea na
maisha yao,” alisema Manji.
Msaada wa
vyakula uliotolewa na wafanyakazi wa kampuni hiyo walipotembelea kwenye
kituo hiko ni pamoja na unga, mchele, maharage, mafuta ya kupikia,
sukari, chumvi, sabuni na mengineyo. Dhumuni kubwa la kufanya hivyo ni
kuwafanya watoto hao nao kufurahia sikukuu ya Pasaka itakayosherehekewa
siku ya Jumapili na Jumatatu duniani kote.
No comments :
Post a Comment