Mrembo wa Tanzania mwenye tamaa
ya kuwa na himaya ya samani za kimataifa kupitia kampuni yake, kama
alivyowahi kuelezwa na jarida la Forbes hivi karibuni, Jacqueline
Ntuyabaliwe ametwaa tuzo mbili za ubunifu kupitia kampuni ya Molocaho by
Amorette.
Ushindi wake huo unamuingiza
katika kundi la watu wenye ubunifu mkubwa wa bidhaa za majumbani na
katika maofisi, muda mfupi tangu kuanzishwa kwa kampuni hiyo.
Molocaho by Amorette kampuni ya
kubuni na kutengeneza samani ilizinduliwa Septemba 2016. Miezi michache
tu tangu kuundwa kwake inaonesha kukimbia na kufanikisha tuzo tatu za
kimataifa.
Katika tuzo zenye ushindani mkali
na heshima kubwa kwenye ubunifu za kimataifa zijulikanzo kama A-Prime
Design (A’Design) zilizofanyika mjini Roma mwishoni mwa wiki Jacqueline
amepata tuzo katika kategori mbalimbali na kuwa wa pili kategori
nyingine.
Bidhaa zilizompatia tuzo ni samani na pia za mwanga.
Ngorongoro Settee ilimpatia
medali ya shaba kwa upande wa samani na katika bidhaa za mwanga Sayari
Lamp pia ilimpatia tuzo ya shaba. Nafasi ya pili ilipatikana katika kiti
cha Flamingo.
Taarifa zilizofikia thebeauty zinasema
kategori ya Furniture, Decorative Items and Homeware Design Category ya
mwaka 2016 na kiti cha Ngorongoro na kategori ya Lighting Products and
Lighting Projects Design Category ya mwaka 2016 ilikuwa na Sayari lamp.
Na Kiti cha Flamingo kilimpatia
nafasi ya pili katika kategori ya Furniture, Decorative Items and
Homeware Design Category ya mwaka 2016.
A-Prime Design Shindano
aliloshiriki Jacqueline Mengi akiwa na kampuni yake ya Molocaho by
Amorette la A’Design hushirikisha wabunifu, wagunduzi na makampuni
yanayotengeneza bidhaa mbalimbali za ubunifu wa ndani.
Shindano la A’ Design
limeanzishwa kwa lengo la kuhakikisha kwamba wabunifu wanakuja na bidhaa
bora kabisa zenye ushindani mkali katika soko la kimataifa.
Kwa kawaida tuzo zake hutolewa
katika kusanyiko kubwa la wabunifu linalofanyika Roma, Italia kwa
kuratibiwa na OMC Design Studios SRL .
Jacqueline, Miss Tanzania (2000)
hivi karibuni alishiriki tuzo za rais za CTI na ana mafunzo ya Interior
Design kutoka Rhodec International.
Kampuni ya Molocaho by Amorette,
kampuni ya Tanzania inajishughulisha na utengenezaji wa samani bora kwa
namna mteja anavyohitaji, nyuzi, taa, urembaji, samani za nje na kwenye
bustani.
Molocaho inatengeneza samani
zenye mahadhi ya kiafrika ikichanganya utamaduni wa Tanzania katika
mazingira ya kisasa na kumalizia na ubunifu wa kimataifa.
Molocaho, moja ya makampuni ya
Afrika Mashariki ya samani yanayokua kwa kasi, imejipatia nafasi kubwa
ya heshima kwa kuhakikisha kwamba inatumia mali ghafi na mbao njema
pekee za Tanzania kutengeneza samani zenye kwenda kimataifa.
Katika mahojiano na jarida
maarufu la Forbes alishawahi kusema kwamba anawania soko la kimataifa
kutokana na ukweli kuwa bidhaa anazotengeneza zimejipambanua kwa wateja.
Jacqueline Ntuyabaliwe, pamoja na
kuwa na ratiba yenye changamoto sana (Yeye ni balozi wa WildAid na yumo
ndani ya bodi kadhaa; mama wa watoto pacha wavulana; mke kwa
mfanyabiashara mwenye mafanikio makubwa na akiendesha taasisi ya hisani
ya elimu), huhakikisha anakagua kila samani inayozalishwa kiwandani
kwake kabla ya kuuzwa au kusafirishwa.
Mume wake, Reginald Mengi, ni
tajiri mwenye mafanikio makubwa nchini Tanzania ambaye ameujenga utajiri
wake kwa kufanya karibu kila kitu kuanzia uzalishaji wa kinywaji cha
Coca-Cola hadi uchimbaji wa madini na kumiliki vituo vya televisheni na
magazeti.
Kwa tuzo hizo Amorette, inajidhihirisha kuwa chata yenye mafanikio makubwa nchini Tanzania na huku ikipanda kwa kasi kimataifa.
No comments :
Post a Comment