Baada ya kazi ya kuunganisha
umeme wa kutosha kukamilika 15 Aprili, 2017 kazi ya kuwasha pampu kubwa
mpya za majighafi na majisafi katika Mtambo wa Ruvu Juu sasa imekamilika
rasmi ambapo mtambo huo sasa umeanza kuzalisha lita milioni 196 kwa
siku. Taarifa ya
Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar Es salaam (DAWASA)
inaeleza.
Ili kufikia uwezo huo wa
uzalishaji kutoka lita milioni 82 zilizokuwa zikizalishwa hapo awali,
kazi mbalimbali zilifanyika ikiwemo ujenzi wa kituo kipya cha kusukuma
maji na ufungaji wa pampu mpya, maeneo mapya ya kusafisha maji, mitambo
ya kuchuja maji, maeneo ya kuchuja tope na tenki kubwa la kuhifadhia
maji safi.
Katika kuhakikisha kuwa maji hayo
yanawafikia wananachi, kituo kipya cha kusukuma maji safi na salama
kilijengwa sambamba na mabomba makuu ya kusafirishia maji hayo yenye
jumla ya urefu wa kilomita 70 kutoka Mlandizi hadi Dar es salaam.
Aidha, tenki jipya lenye uwezo
wakuhifadhi lita milioni 10 limejengwa eneo la Kibamba lenye mwinuko; na
kutoka hapo maji hushuka kwa nguvu ya mtiririko hadi katika matenki ya
Kimara.
Kazi iliyokuwa imebaki ilikuwa ni
kuongeza nguvu ya umeme ili kuwezesha pampu hizo mpya kufanya kazi.
Hivi sasa kazi hiyo imekamilika, ukaguzi umefanyika na pampu moja baada
ya nyingine zimewashwa ili kuhakiksha mfumo mzima sasa unafanya kazi.
Hadi kufika jana jioni (17 Aprili) maji yalikuwa yanaingia katika matenki yote kwa kupitia mabomba mapya bila matatizo.
Mtambo huo wa maji wa Ruvu Juu
sasa unapokea umeme wa kutosha kutoka katika transfoma kubwa iliyopo
kituo kidogo cha umeme cha Chalinze (Sub-station) yenye uwezo wa 45/55
MVA ambapo inawezesha pampu zote mpya na za kisasa zilizofungwa kuwashwa
kwa wakati mmoja.
Mikataba ya jumla ya dola za
Marekani milioni 99 ya upanuzi wa mtambo na ujenzi wa mabomba mapya
kutoka Ruvu Juu mpaka Kimara, ujenzi wa tanki kubwa lenye ujazo wa lita
million 10, ofisi kwa ajili ya shughuli za uendeshaji wa huduma na
nyumba za watumishi wa mtambo ilisainiwa mwaka 2014. Fedha hizo zilikuwa
ni mkopo wa masharti nafuu toka Benki ya Exim ya India.
Kazi inayopewa msukumo mkubwa kwa
sasa ni ujenzi wa miundombinu ya usambazaji maji yaliyoongezeka ili
wananchi wengi zaidi waweze kunufaika na jitihada na uwekezaji
uliofanywa na Serikali yao.
Maeneo yanayonufaika ni pamoja na
miji ya Kibaha, Mlandizi na baadhi ya Vitongoji vyake katika mkoa wa
Pwani pamoja na maeneo yote yaliyopo jirani na barabara ya Morogoro
yaani Kiluvya, Kibamba, Mbezi, Kimara, Ubungo, Malamba mawili, Msigani,
Msakuzi, Makabe, Kibangu, External, Makuburi, Tabata, Segerea, Buguruni
pamoja na Vingunguti.
No comments :
Post a Comment