Wednesday, March 29, 2017

WAZIRI MAHIGA AWASILISHA UJUMBE MAALUM WA MHE. RAIS MAGUFULI KWA KATIBU MKUU WA UMOJA WA MATAIFA


mah1
Mhe. Mahiga akiwakilisha Ujumbe Maalum wa Mhe. Rais Magufuli kwa Bi Maria Luiza Ribeiro – Mnadhimu Mkuu wa Ofisi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.
mah2
Mhe. Mahiga akielezea ujumbe aliouwasilisha  kutoka kutoka kwa Rais Magufuli. (Kushoto kwa Mhe. Mahiga ni  Balozi Celestine Mushy Mkurugenzi Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, kulia ni Mhe. Balozi Modest Mero – Mwakilishi wa Kudumu  wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa  na mwisho ni Lt Col George Itang’are – Mwambata Jeshi.
mah3
Mhe. Mahiga akizungumza na Mabalozi wa nchi za SADC wanaochangia majeshi ya Ulinzi wa Amani – FIB – MONUSCO – DRC. mah4
Mhe. akiagana na Bi Ribeiro baada ya Mazungumzo
………………………………………………………………………………
Mhe. Dkt Augustine Mahiga amewasilisha kwenye Umoja wa Mataifa ujumbe maalumu wa Mhe. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Asasi ya SADC ya Siasa, Ulinzi na Usalama unaoeleza msimamo wa Wakuu wa
Nchi na Serikali ya Nchi za SADC kuhusu kuongezewa muda wa jukumu wa  kikosi cha Ulinzi wa Amani cha Umoja wa Mataifa (MONUSCO – Force Intervention Brigade – FIB) nchini DRC kinachotarajiwa kumaliza muda wake wa jukumu ifikapo tarehe 31 Machi  2017.
Waziri Mahiga aliwasilisha ujumbe huo kwa Mhe. Maria Luiza Ribeiro, Mnadhimu Mkuu wa Ofisi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (Chef de Cabinet) kwa niaba ya Mhe. Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ambaye alikuwa safarini nje ya Marekani kikazi.
Akiwasilisha ujumbe huo, Mhe. Mahiga alieleza kuwa, moja ya maazimio ya Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC uliofanyika tarehe    18 Machi 2017 nchini Swaziland ni pamoja na Jumuiya ya SADC kufikisha ujumbe  kwenye Umoja wa Mataifa wa kuunga mkono jitihada zinazofanywa  na Umoja wa Mataifa (Baraza la Usalama) kukiongezea muda kikosi cha Ulinzi wa Amani cha Umoja wa Mataifa kinachotarajia kumaliza muda  wake  wa jukumu kwa mujibu wa Mkataba tarehe   ifikapo 31 Machi 2017.
Mhe. Mahiga alimueleza Bibi Maria kuwa, Jumuiya ya SADC inaupongeza Umoja wa Mataifa kwa jitihada za kuleta amani nchini DRC na kwamba, Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC wanamatumaini kuwa kuongezewa muda kwa kikosi hicho kutazingatia mahitaji ya changamoto za usalama zilizopo nchini DRC na hivyo kukiwezesha kikosi hicho kukabiliana na changamoto hizo.
Mhe. Mahiga alitumia nafasi hiyo kueleza hali  iliyopo  kwa sasa  ya ulinzi na usalama katika nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu, ambapo aligusia na kuomba Umoja wa Mataifa kuongeza jitihada za kupatia ufumbuzi wa matatizo yaliyopo nchini DRC na Burundi.
Waziri Mahiga alifanya mazungumzo na wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na  Mabalozi wa Nchi zinazochangia vikosi vya Ulinzi na Usalama  MONUSCO – FIB  nchini DRC, Balozi wa Uingereza kwenye Umoja wa Mataifa ambaye ni Rais wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Balozi wa Ufaransa kwenye Umoja wa Mataifa (Pen-holder) wa DRC na Mabalozi wa Afrika wanaowakilisha nchi zao kwenye Umoja wa Mataifa.
Mhe. Mahiga anatarajia kuhutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kesho tarehe 30 Machi  2017.

No comments :

Post a Comment