Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Wanawake na vijana wanaopewa
mikopo na Serikali kupitia Halmashauri ya Mji wa Ifakara mkoani Morogoro
wamekumbushwa kupeleka marejesho kwa wakati ili kuwapa fursa na
wananchi wengine kupata mikopo hiyo.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri
hiyo, Christopher Msimbe ameyasema hayo hivi karibuni
alipokuwa
akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusu nafasi ya vijana
walemavu waliomaliza mafunzo kupitia Mradi wa Uwezeshaji Vijana
Kiuchumi (YEE) unaoratibiwa na Shirika la Plan International.
Msimbe amesema pamoja na kuwepo
kwa changamoto mbalimbali, Halmashauri inatambua nafasi ya vijana katika
jamii hasa vijana wenye ulemavu na ndio sababu wanawakumbuka katika
fursa nyingi zinazokuja katika Halmashauri hiyo kutoka kwa wadau
mbalimbali.
“Katika Halmashauri yetu
tumebahatika kupata mradi wa YEE unaowashirikisha hata vijana wenye
ulemavu, mradi huo unalenga kuwapatia mafunzo ya ufundi vijana ili
waweze kujitegemea hivyo sisi kama Serikali tumetoa jumla ya shilingi
4,000,000 kwa vikundi viwili vya vijana wenye ulemavu ili waweze kuinua
shughuli zao,”alisema Msimbe.
Amefafanua kuwa Halmashauri zote
nchini zinatakiwa kutenga fedha kwa ajili ya kuwapatia mikopo vijana na
wanawake ili kuwasaidia kujikwamua kimaisha kwa kuendelezea biashara zao
lakini asilimia kubwa wamekuwa hawapeleki marejesho kwa wakati na
kusababisha Halmashauri kushindwa kutoa mikopo kwa watu wengine.
Nae, Mwenyekiti wa Mtaa wa
Kiungwile “A” iliyopo wilayani Kilombero Mkoa wa Morogoro, Emmanuel Sama
amesema mradi huo umewasaidia vijana wengi kwa sababu kabla ya mradi
huo vijana walikuwa wakizurura mitaani bila kazi yoyote pia vijana
walemavu walikuwa wakikaa ndani bila kujua hatima yao.
“Mtaani kwangu nina vijana watano
waliopewa mafunzo na shirika hili ambao wamefanikiwa kuunda kikundi chao
kijulikanacho kama ‘Baraka Farmers Group’ ambacho kinatumia elimu
waliyoipata pamoja na mkopo wa shilingi 1,500,000 kutoka katika
Halmashauri yetu kujiendeleza kiuchumi, nawashkuru vijana hawa kwani
wanatumia vizuri fursa waliyopewa na kurejesha fedha walizokopeshwa kwa
wakati,”alisema Sama.
Sama ametoa rai kwa wananchi
wanaopewa mikopo na Serikali hasa wananchi wasio na ulemavu ambao
wanaweza kufanya kazi kwa uhakika kurejesha fedha za mikopo kwa wakati
ili Halmashauri iweze kuendelea kuwasaidia wananchi wengine na
watakaokaidi watachukuliwa hatua stahiki ili warudishe fedha hizo.
Mradi huo wa miaka mitatu umeanza
mwaka 2015 hadi 2018 unatekelezwa kwa ushirikiano wa mashirika ya VSO,
CCBRT, VETA, UHIKI, CODERT pamoja na Serikali ya Tanzania huku
ukiratibiwa na Shirika la Plan International chini ya ufadhili wa Umoja
wa Nchi za Ulaya (EU).
No comments :
Post a Comment