
Mkurugenzi Mkuu wa
Mfuko wa Pensheni wa PSPF, Bw. Adam Mayingu, (kushoto), akizungumza jambo na
Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya CRDB, Dkt. Charels Kimei, wakati wa uzinduzi wa
ushirikiano baina ya taasisi hizi mbili ambapo PSPF sasa itawakopesha wanachama
wake kwa kupitia Benki ya CRDB kwenye
maeneo ya elimu, viwanja na pesa za kuanzia maisha.
Christian Gaya
Mfuko wa PSPF na CRDB wanalenga
kupanua uwigo wa huduma na fursa kwa wanachama wa PSPF kujipatia huduma ya
mikopo nafuu kwa kiwango cha riba
kilicho chini ya kile kinachotolewa katika soko na taasisi zingine za
kifedha nchini. Mfuko umeona haja ya kushirikiana na CRDB kuanzisha huduma hii
kupitia mtandao wa CRDB ulioenea nchi nzima nchini
Akizungumza kwenye hafla ya utiaji
saini mpango huo, Mkurugenzi Mkuu wa
PSPF, Bw Adam Mayingu, anasema kuwa mpango huu wa kutoa mikopo kwa wanachama
ulianza tangu Desemba 2014 kwa kupitia taasisi nyingine za kifedha.
Mikopo hiyo ni pamoja na mkopo wa
elimu, mkopo wa kuanzia maisha na mkopo wa viwanja yaani nipo site na PSPF
Anafafanua ya kuwa kwa upande wa
mkopo wa elimu, mwanachama anaweza kukopa kwa ajili ya kujiendeleza kielimu
katika ngazi yeyote ya elimu. Ngazi hiyo ni
stashahada, shahada, shahada ya uzamili na hata mafunzo ya ufundi.
Mkopo wa elimu ni huduma nyingine
inayolengwa na ushirikiano huu kati ya PSPF na CRDB.

"Kupitia huduma hii mwanachama
wa PSPF atafaidi matunda ya uanachama wake kwa kuweza kupata mkopo
utakaomwezesha kujiendeleza kielemu na kuzifikia ndoto za kupata elimu ya juu.
mkopo huu utatolewa kwa mwanachama wa PSPF aliyechangia katika mfuko kwa muda
usiopungua miezi 24" Mayingu anasema.
Kwa upande wa mkopo wa kuanzia
maisha, anasema mwanachama aliyepata ajira kwa mara ya kwanza huwa na mahitaji
yake muhimu na kwa kutambua hilo, PSPF kwa kushirikiana na CRDB
wameanzisha mpango huu ambapo mwanachama
anaruhusiwa kukopa mishahara yake ya miezi miwili ili aweze kujipanga na maisha
mapya ya ajira. Na kurejesha mkopo huu kupitia makato madogo madogo ya mshahara
wake kwa kipindi cha miaka miwili hadi mitano.
"Ni kweli usiopingika wengi wa
waajiriwa wapya hukutana na changamoto kadha ikiwa ni pamoja na ile ya kumudu
gharama za kuanza maisha pale wanapoajiriwa katika maeneo yao ya kazi. kwa
kuzingatia hilo mfuko ulianzisha mkopo huu kumwezesha mwajiriwa mpya kujiandaa
na changamoto hizi mpya kimaisha" Mayingu anafafanua.
Anaendelea kufafanua ya kuwa chini
ya makubaliano haya ya PSPF na CRDB, mwanachama wa PSPF aliyechangia katika
mfuko kwa kipindi cha kati ya miezi 6 na kisichozidi miezi 12 ataweza kupata
mkopo huu nafuu kupitia CRDB ili kumwezesha kumudu gharama za awali kama vile:
kulipia kodi ya nyumba, kununua fenicha za ndani, kununua nyenzo za usafiri,
kununua kiwanja au shamba pamoja na kugharamia shughuli mbalimbali za kijamii.
Kuhusu mkopo wa viwanja kwa wanachama, anasema kuwa
huduma hii itawawezesha wanachama wa PSPF kukopa na kumiliki viwanja vya
makazi ambavyo vinapatikana maeneo mbali
mbali ya nchi.
“Lengo kubwa hapa ni kuwawezesha wanachama wa PSPF
kumiliki viwanja vya makazi vilivyopimwa iii kuwaepusha dhidi ya ujenzi katika
makazi holela, ambayo yamekuwa na gharama kubwa kuliko makazi
yaliyopangiliwa”,anasema.
Alifafanua kuwa lengo kubwa la
kuanzisha mikopo hiyo ni kuhakikisha kila mtanzania anatimiza ndoto yake ikiwa ni katika masomo kupitia mkopo
wa elimu, ndoto yake nyingine kupitia
mkopo wa kuanzia maisha au mkopo wa viwanja.
Afisa Uhusiano Mwandamizi wa PSPF, Bw. Abdul Njaidi, akitoa hotuba ya ukaribisho
Anasema mkopo wa viwanja vya makazi
ni eneo jingine linalolengwa na ushirikiano huu kati ya PSPF na CRDB. Huduma
hii ilianzishwa na PSPF ili kuwawezesha wanachama wake pote nchini kumiliki na
kuishi katika makazi bora yaliyopimwa. kupitia mkopo huu mwanachama wa PSPF
anaondolewa ugumu unaotokana na gharama kubwa za kumiliki ardhi katika maeneo
yaliyopimwa kisheria.
"Chini ya makubaliano haya kati
ya PSPF na CRDB mwanachama yeyote wa PSPF aliyechangia katika mfuko kwa kipindi
cha kati ya miezi 6 na kisichozidi miaka 60, anaweza kukopa mkopo huu kupitia
CRDB na kurejesha mkopo huu kupitia makato madogo madogo ya mshahara wake kati
ya kipindi cha miaka 2 hadi 5" anafafanua.
Anasema katika awamu hii ya pili ya
utekelezaji wa huduma hii maeneo yafuatayo yamelengwa na mpango huu: Dar es
salaam, Morogoro, Pwani, Dodoma, Songea, Tabora, Lindi, Singida, Arusha,
Kagera, Mwanza, Iringa, Shinyanga, Mpanda, Katavi, Tanga, Kigoma na Mtwara.
"Mara zote PSPF inajivunia
ubunifu ambao umeufanya mfuko huu kuwa wa kwanza hasa kwa upande wa mafao kwa
wanachama . Ubunifu wa PSPF umekuwa kivutio
sio tu kwa wanachama wake bali pia kwa mifuko mingine ya pensheni nchini. Hivyo
natoa wito kwa watanzania wenzetu kujiunga na PSPF ili waweze kunufaida na
fursa hizi", Mkurugenzi mkuu wa PSPF ndugu Mayingu anasema.
Mayingu anataja ya kuwa hadi kufikia
tarehe 17 Mwezi huu idadi ya wanachama walionufaika na mikopo hiyo na idadi kwenye mabano ni Elimu
(1,432)), mkopo wa kuanzia maisha (847), mkopo wa viwanja (58).
“Kwa kushirikiana na benki ya CRDB
ambayo ina mtandao mkubwa wa matawi hapa nchini tunaamini watanzania wengi
watanufaika na mikopo hii na kwa kufanya hivyo tutakuwa tunatakeleza juhudi za
serikali ya awamu ya tano ya kuhakikisha watanzania wengi zaidi wananufaika na
huduma mbali mbali za Mifuko ya Hifadhi ya jamii”, anaeleza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji
wa Benki ya CRDB, Dk Charles Kimei, anasema azma yao ni kuhakikisha kuwa
ushirikiano na wadau wanamkomboa kiuchumi mwananchi hususan mwenye kipato cha chini kwa kumpatia
mkopo wenye riba ya asilimia 14 tu kwa mwaka. Kuhusu marejesho anasema
ni kuanzia mwaka mmoja hadi miaka mitano.
Ushirikiano wetu na PSPF bado una muendeleo ulio mpana kwani kwa
pamoja tunadhamiria hapo baadae kuingiza sokoni mikopo kwa ajili ya wastaafu yaani
‘pensioners’.
Anasema mpango huu wa utoaji wa mikopo
kwa wastaafu una lengo la kuleta faraja na kuwasaidia wastaafu katika kukidhi
mahitaji yao mbali mbali ya kimaisha ikiwamo kulipia gharama za matibabu, ada
za shule za watoto au wajukuu na
kuendesha biashara ndogo ndogo zitakazosaidia kupunguza ukali wa maisha ya kila
siku.

Dkt. Charles Kimei, akitoa hotuba yake kueleza jinsi benki yake ilivyofurahishwa na ushirikiano huo.
Dkt Kimei anafafanua kuwa nia yao ni kujenga mazingira mazuri kwa
wastaafu walio wanachama wa PSPF ili kustaafu kusiogopwe na kuonekana ni mwanzo
wa kuanza kwa kipindi cha maisha ya shida yasiyokuwa na matumaini.
“Tunataka kujenga tabia ya kuwafanya
wafanyakazi wanapopata barua za kustaafu wasihuzunike kama ilivyozoeleka”,anadokeza
na kusema ya kuwa mwanachama wa PSPF
anayetaka mkopo anatakiwa aende kwenye tawi lolote la benki ya CRDB ililopo
karibu naye ili kupata huduma Dkt Kimei anasema
Christian
Gaya ni mwanzilishi wa Kituo cha HakiPensheni Tanzania, mshauri na mtaalamu wa
masuala ya pensheni. Kwa maelezo zaidi wasiliana kwa: gayagmc@yahoo.com unaweza kutembelea tovuti
hakipensheni monitor online na
hakipensheni blog Simu namba +255 655 13 13 41

No comments :
Post a Comment