Afisa kilimo na Mratibu wa MIVARF
Mkoa wa Singida akimsikiliza mkulima wa Alizeti Mkoa wa Singida
akipalilia zao hilo, mkulima huyu amefuata ushauri wa kitaalamu wa
kupanda kwa mistari, kuweka mbolea na kutumia mbegu mpya ya record
ambayo huzalisha kwa wingi.
Afisa
kilimo na Mratibu wa MIVARF Mkoa wa Singida akimsikiliza mkulima wa
Alizeti Mkoa wa Singida akipalilia zao hilo, mkulima huyu amefuata
ushauri wa kitaalamu wa kupanda kwa mistari, kuweka mbolea na kutumia
mbegu mpya ya record ambayo huzalisha kwa wingi.
Wakulima wa alizeti Mkoani Singida
wameazimia kuwa wazalishaji namba moja nchini wa alizeti kwa wingi na
ubora wa hali ya juu kutokana na kutumia mbinu bora na za kisasa huku
wakiachana na kilimo cha mazoea kilichowapa matokeo kidogo na yasiyo na
ubora.
Wakulima wa Wilaya tatu za Iramba,
Manyoni na Singida wamefikia uamuzi huo katika vikao kati yao na kamati
ya ufuatiliaji wa progamu ya Uboreshaji wa Miundombinu ya Masoko,
Uongezaji wa thamani ya mazao na Huduma za kifedha vijijini (MIVARF)
iliyokuwa ikifanya tahmini ya mradi huo kwa kutembelea mashamba na
kuzungumza na wakulima hao.
Mwenyekiti wa Kikundi cha Mwangaza
cha wakulima wa Alizeti kata ya Sanjaranda Wilayani Manyoni Bi. Janeth
Emmanuel amesema, mradi wa MIVARF umewahamasisha kutumia mbegu ya
alizeti ya kisasa aina ya record ambayo huzalisha wastani wa gunia 12
mpaka 16 kwa ekari moja wakati mbegu ya zamani ambayo walikuwa
wakiitumia ya zebra imekuwa ikizalisha gunia mbili mpaka nne kwa ekari
moja.
Bi Janeth amesema kutokana na
wakulima wengi kuhamasika kutumia mbegu mpya ya record na kufuata elimu
waliyopewa na MIVARF, Mkoa wa Singida utazalisha alizeti nyingi na bora
kwa ajili ya viwanda vya ndani na nje ya Mkoa.
Amesema wakulima wa alizeti
walikua hawafuati ushauri wa kupanda zao hilo kwa mistari, kuacha nafasi
pamoja na kuweka mbolea ambapo awali walidhani alizeti haihitaji
kuwekewa mbolea kitu ambacho sio sahihi na hivyo kupelekea mkulima
kutumia eneo kubwa na kuzalisha kidogo.
Bi. Janeth ameongeza kuwa kutokana
na matarajio ya kuvuna alizeti nyingi elimu zaidi juu ya uongezaji wa
thamani wa alizeti itolewe kwa wakulima ili waweze kupata faida kubwa
tofauti na awali ambapo wamekuwa wakimwaga mashudu ambayo huzalisha kiwi
na mkaa na kuuza alizeti ghafi badala ya mafuta.
Naye Mtoa huduma wa MIVARF Wilaya
ya Manyoni Anthony Mtu amesema mradi huo umewafikia wakulima elfu mbili
katika kata ya Sanjarada huku wakianzisha mashamba darasa 12 ya zao la
alizeti yenye ukubwa wa ekari 24 huku matarajio ya mavuno kwa mashamba
darasa yakiwa ni magunia 288.
Mtu amesema wakulima wamehamasika
kutumia mbegu ya record baada ya kuelimishwa kuwa mbegu hiyo, inatumia
maji kwa ufanisi, inatoa mavuno mengi na haishambuliwi na magonjwa kwa
urahisi.
Kwa upande wake Afisa Kilimo na
Mratibu wa MIVARF Mkoa wa Singida Lucas Mkuki amesema mradi huo umeanza
kutekelezwa mwaka 2011 ukiwa unafadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya
Afrika.
Mkuki amesema katika wilaya zote
Mradi umeweza kukarabati barabara ili kurahisisha wakulima kusafirisha
alizeti ambapo barabara zilizokarabatiwa ni ya Muhanga-Mwakajenga wilaya
ya Manyoni kilometa 20, Njiapanda-Ngimu Wilayani Singida Kilometa 28 na
wilayani Iramba kilometa 1.4 ujenzi wake utaanza hivi karibuni.
Ameongeza kuwa mradi umefanikisha
ujenzi wa maghala yenye uwezo wa kuhifadhi mazao kiasi cha tani 1000
katika kijiji cha Mtinko wilayani Singida, kijiji cha Nselembwe wilayani
Manyoni na kijiji cha Sanjaranda wilayani Manyoni.
Mkuki amesema mradi wa MIVARF
umewajengea uwezo wazalishaji wa alizeti kuyafikia masoko na kuongeza
thamani ya zao hilo huku akiwasisitiza wakulima kuendeleza elimu na
vikundi vilivyozalishwa na mradi huo endapo mradi utafikia ukomo wa
utekelezaji wake.
No comments :
Post a Comment