Wachimbaji
wa mchanga unaodhaniwa kuwa na madini ya almasi ‘Wabeshi’ wilaya ya
Kishapu mkoani Shinyanga wameiomba serikali ya awamu ya tano
inayoongozwa na rais John Pombe Magufuli iwatengee eneo maalum kwa ajili
ya uchimbaji ili waache vitendo vya kuvamia mgodi wa almasi wa
Williamson (Williamson Diamonds Ltd).
Wachimbaji hao wa madini ambao wamekuwa
wakivamia mgodi na kuambulia kupigwa,kunyanyaswa na hata kuuawa na
walinzi wa mgodi huo,walisema yapo maeneo ambayo hayatumiki hivyo ni
vyema serikali ikawakatia maeneo ili iwe suluhu ya mgogoro kati yao na
uongozi wa mgodi.
Wakizunguza na waandishi wa habari hivi
karibuni kwa nyakati tofauti Wabeshi walisema wananchi wanaozunguka
mgodi huo wamekuwa hawanufaiki nao kabla na baada ya uhuru hivyo
wanaamini serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na rais Magufuli
itatatua kero yao ya muda mrefu.
Walisema vijana wengi wanategemea
shughuli ya uchimbaji hivyo wakipewa eneo la uchimbaji wataweza kumudu
gharama za maisha ikiwemo kutunza familia zao.
Mmoja wa wabeshi hao Mabula Njile mkazi
wa kijiji cha Nyenze kata ya Mwadui Luhumbo alisema endapo serikali
itawapatia maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo hawatavamia tena mgodi
wa Williamson kwenda kuchimba mchanga unaodhaniwa kuwa na madini ya
almasi.
“Tunashuhudia misimamo na maamuzi mazuri
yanayofanywa na rais Magufuli katika kuwatetea wanyonge,sisi wabeshi
tunampenda rais Magufuli tunaomba asikie kilio chetu,hatuna
ajira,tunavamia kutokana na hali ngumu ya maisha,sisi shida yetu ni
kupata eneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo hatutaingia tena kwenye eneo
la mwekezaji”,alieleza Njile.
Juma Ng’ombeyapi mbeshi kutoka kijiji
cha Ng’wang’holo alisema hajawahi kuona kiongozi yeyote wa juu wa
serikali akifika katika maeneo yanayozunguka mgodi huo ili kusikiliza
kero za wananchi na badala yake baadhi ya viongozi wamekuwa
wakishirikiana na uongozi wa mgodi kuwagandamiza wananchi wanaozunguka
mgodi huo.
“Hakuna serikali iliyokuja kutusikiliza
matatizo yetu,lakini tunaona serikali ya awamu ya tano
itatusaidia,tunaomba tupewe eneo la kuchimba ili tusivamie mgodi kwani
sasa wananchi tunapigwa,tunateswa,tunaumizwa na wapo ndugu zetu
wamepoteza maisha kutokana na kuvamia mgodi”,alieleeza Ng’ombeyapi.
“Tuna imani kubwa na rais Magufuli
tunataka atusikilize,tunasubiri maamuzi ya rais kwa sababu viongozi
wengine wameshindwa kutusaidia na hatuna Imani nao,tumechoka kunyanyaswa
katika nchi yetu”,aliongeza mbeshi mwingine Peter Joseph kutoka kijiji
cha Ng’wang’holo.
Hata hivyo mkuu wa wilaya ya Kishapu
ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wilaya hiyo
Nyabaganga Talaba alionesha kushangazwa na madai ya wabeshi na kusema
wachimbaji hao ‘wabeshi’ wamepewa maeneo ya kuchimba lakini hawataki
kuyaendeleza kuyachimba kama wachimbaji wadogo.
“Kwa ujumla wachimbaji hawa hawana vifaa
hata ule utaalamu wa kufanya kazi za madini hawana kwa hiyo hata kama
wakipewa maeneo ya kuchimba hawataweza kufanya kazi”,alisema Nyabaganga.
“Wanasema wanafanya uchimbaji wa madini
lakini uchimbaji wanaoufanya ni wa kuvamia mgodi,na huo wa kuvamia mgodi
tumewakataza,kwa sababu ni wizi kwa wizi mwingine,kwa sababu wanaingia
siyo kihalali ,wanapora,wanajeruhi hivyo tumewakataza na wala hakuna
sheria inayowaruhusu kwenda huko na hilo wanalijua”,aliongeza
Nyabaganga.
Mkuu huyo wa wilaya aliwataka wananchi
wanaozunguka mgodi huo kufanya shughuli zingine badala ya kutegemea
mgodi tu kwani mgodi pekee hauwezi kuwaondolea matatizo yao yote.
“Tupo wengi sana,tuna mahitaji
mengi,mgodi tu hautatuondolea matatizo yetu,na mgodi tu
hautatubadilisha,kuna maisha nje ya mgodi,niwashauri tu wananchi wangu
tutafute kitu kingine tunachoweza kufanya badala ya mgodi”,aliongeza
Nyabaganga.
Na Kadama Malunde-Malunde1 blog
Mkazi wa kijiji cha Nyenze kata ya Mwadui Lohumbo akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea kijiji hicho
Mchimbaji mdogo wa madini ‘Mbeshi’
akionesha jeraha kichwani lililotokana na kipigo kutoka kwa walinzi wa
mgodi wa Mwadui “Mgodi wa Williamson” baada ya kwenda eneo hilo kuchimba
mchanga unaodhaniwa kuwa na madini ya almasi
Mchimbaji mdogo wa madini akizungumza ambapo aliiomba serikali kuwapatia eneo la kuchimba madini
Mchimbaji mdogo wa madini akizungumza mbele ya waandishi wa habari( wengine hawapo pichani)
Mbeshi kutoka kijiji cha Ng’wang’holo kata ya Mwadui Lohumbo akizungumza na waandishi wa habari
Mbeshi akionesha kovu lilitokana na kipigo baada ya kuvamia mgodi wa Williamson
Mbeshi akiomba rais Magufuli kuwapatia eneo la kuchimba ili waache kuvamia mgodi wa Williamson
Mbeshi kutoka kijiji cha Wizunza kata ya
Mwadui-Lohumbo akielezea ukatili wanaofanyiwa wachimbaji wadogo wa
madini wilayani Kishapu.
Picha zote na Kadama Malunde-Malunde1 blog
No comments :
Post a Comment