WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amesema viongozi wa mataifa ya Afrika wamekubaliana kufungua fursa za
kiuchumi baina ya nchi hizo pamoja na kuweka utaratibu wa kutumia hati
moja ya kusafiria.
Alitoa kauli hiyo jana (Jumatano,
Machi 22, 2017) wakati akingumzia makubaliano yaliyofikiwa katika
uzinduzi wa Jukwaa la Uchumi Barani Afrika (AEP) uliofanyika nchini
Mauritius Machi 20 hadi 21, 2017. Waziri Mkuu alimuwakilisha Mheshimiwa
Rais Dkt. John Magufuli.
Waziri Mkuu alisema viongozi hao
wamekubaliana kwamba mataifa ya Afrika yawe na hati moja ya kusafiria,
ambayo itawawezesha wananchi kuingia nchi yoyote ndani ya bara hilo bila
ya vikwazo kwa lengo la kurahisisha muingiliano wa watu na bidhaa.
Alisema jambo jingine
walilokubaliana ni kuimarisha Jumuiya zao ikiwemo ya Afrika Mashariki
(EAC), Jumuiya ya Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika
(COMESA) na Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na
kuzishawishi nchi nyingine ambazo hazijajiunga kujiunga jumuia hizo.
Alisema viongozi hao walijadili
namna watakavyoweza kuinua uchumi na kuweka mikakati ya kuimarisha
viwanda, ambapo Tanzania ipo katika nafasi nzuri kwa kuwa tayari
inatekeleza mpango wa kukuza uchumi wake kwa kupitia sekta ya viwanda.
“Viwanda ndiyo mkombozi wa
changamoto mbalimbali barani Afrika ikiwemo ya ajira, hivyo Serikali ya
awamu ya Tano imedhamiria kujenga uchumi wa viwanda ili kuongeza ajira
na kuondoa umaskini miongoni mwa wananchi wake,” alisema.
Jukwaa hilo lilizinduliwa Machi
20, 2017 na Waziri Mkuu wa Swazland Bw. Barnabas Sibusiso Dlamini kwa
niaba ya Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) na Rais wa Chad, Idriss
Deby. Pia Bw. Dlamini alimuwakilisha Mfalme Muwsati wa III.
Bw. Dlamini alisema nchi za
Afrika zinatakiwa kuboresha mitaa yake na kujikita katika kutoa elimu ya
masuala ya sayansi na viwanda ili kuwajengea wanafunzi uelewa wa
masuala hayo angu wakiwa na umri mdogo.
Alisema iwapo wanafunzi wataanza
kujifunza masuala ya viwanda kuanzia shule watakuwa na uelewa wa kutosha
wa masuala hayo jambo ambalo litawarahisishia kupata ajira katika
viwanda mbalimbali, hivyo kuondokana na tatizo la ajira linalozibakili
nchi nyingi za Afrika.
Uzinduzi wa jukwaa hilo ulikuwa
na ajenda nne ambazo zilihusu sekta ya viwanda, kukuza biashara miongoni
mwa nchi za Afrika, kukuza ujuzi katika taaluma mbalimbali na
kurahisisha muingiliano wa watu na bidhaa baina ya mataifa hayo.
Jukwaa hilo lilifanyika kwa siku
mbili lilihudhuriwa na viongozi wakuu wa nchi za Afrika, wanazuoni,
wafanyabiashara pamoja na watu kutoka kwenye asasi mbalimbali za kiraia
barani Afrika.
No comments :
Post a Comment