Benjamin Sawe,Dar es Salaam.
Maelezo.
Zaidi ya asilimia 60 ya watoto
wenye umri wa miaka 13 hadi 17 wanatumia zaidi ya masaa mawili kila siku
kuangalia mitandao ya kijamii pamoja na vipindi mbalimbali vya
Televisheni.
Hii inaweza kuwa njia kubwa ya
kuunganisha, lakini pia kuna hatari zinazohusiana na kutumia muda mwingi
sana kwenye vyombo vya habari kijamii.
Leo hii ni nadra kukuta familia
ambazo watoto na vijana wake hawajaathirika na vyombo vya
habari na
elektroniki kama vile televisheni, intaneti na michezo mingine tofauti
ya kompyuta.
Hata hivyo utumiaji mkubwa na wa
masaa mengi wa vyombo hivyo hauwahusu watoto na vijana tu, bali watu
wazima pia wameathirika na jambo hilo.
Kutokana na sababu kadhaa za
kimwili, kisaikolojia na kiroho, kuna udharura kwa watoto kusimamiwa
vyema na wazazi, mashirika na taasisi za kielimu na kiutamaduni na
kadhalika vyombo vya habari ili kupunguza madhara yanayotokana na
matumizi mabaya ya vyombo hivyo vya elektroniki.
Licha ya kompyuta kuwa na pande
chanya tofauti za kimaendeleo, hasa katika nyanja za kielimu na huduma
za mawasiliano, lakini chombo hicho pia kina nafasi hasi kwa watoto na
hata kwa watu wazima.
Utumiwaji usio na udhibiti wa
chombo hicho na kadhalika vyombo vingine vya elektroniki kama vile
televisheni, unaweza kuyaweka hatarini maisha ya watoto kutokana na
athari zake mbaya kwa ustawi wa kiroho, kisaikolojia na kijamii wa
watoto hao.
Harakati zetu za kifizikia na
miamala yetu tofauti ya kijamii, ni umuhimu yenye taathira kubwa kwa
afya na tabia za mtoto. Kinyume chake, ikiwa mtoto atatumia muda wake
mwingi katika matumizi ya michezo ya kompyuta, basi hawezi kunufaika na
upande chanya wa kujenga akili yake wala harakati bora kwa ajili ya
kuufikia ukamilifu wake kijamii.
Mbali na hayo, watoto pia
wanaweza kukabiliwa na hatari ya kutekeleza vitendo vya ukatili na
visivyo vya kikatili hata katika umri wao mdogo. Hali hiyo ambayo
inaweza kufikiwa ghafla au hata kwa makusudi, huwaletea watoto na vijana
madhara yasiyoweza kufidika hasa kuhusiana na masuala ya kiafya,
kisaikolojia sambamba na kueneza kwa kiasi kikubwa matatizo ya kimwili
na kiakili kama vile utovu wa maadili, vitendo vya ukatili, madawa ya
kulevya, tabia mbaya katika jamii, kuzorota thamani za familia na kuenea
jinai na uhalifu wa kila aina katika jamii.
Ukweli ni kwamba, wazazi
hawajawachwa peke yao katika jukumu la kutoa malezi bora kwa watoto wao,
bali wataalamu wa mambo wamefanya utafiti wa kina katika uwanja huo na
kuwasaidia katika suala hilo kwa kuwasilisha njia bora za malezi ambazo
zinawavutia watoto na kuwafanya waishi maisha bora katika jamii.
Watafiti hao wanasema kuwa, licha
ya kwamba haiwezekani kuwatenga watoto na ulimwengu wa michezo ya
kompyuta lakini tunaweza kuwaepusha na madhara ya michezo hiyo kwa
kutumia njia na mbinu zinazofaa.
Udhibiti fulani wa matumizi ya
kompyuta kila siku au kwa wiki, ni moja ya njia hizo. Kwa mbinu hiyo,
mtoto anaweza kutumia chombo hicho kwa muda na kiwango kilichoainishwa
na kila pale anapokwenda kinyume na kiwango hicho, basi anapasa kuzuiwa
na kuadhibiwa.
Hata hivyo utumiaji mabavu na
nguvu hauna nafasi katika hapa. Katika kesi kama hiyo njia ya mazungumzo
sanjari na kumzuia kwa muda, kutumia vitu anavyovipenda mtoto huyo,
inafaa kutumiwa hapa.
Wakati mwingine mtoto hutumia
vyema kompyuta kwa kujinufaisha kielimu na chombo hicho muhimu cha
teknolojia na kwa kweli katika hali kama hii wazazi hawapaswi kumzuia
mtoto kutumia chombo hicho cha kompyuta. Lakini jambo linalopaswa
kuzuiwa ni tabia ya mtoto huyo kutumia wakati wake mwingi katika kichezo
isiyofaa ya kompyuta.
Moja ya nyenzo zingine za
udhibiti ambazo zinaweza kutumiwa na wazazi katika kusimamia mienendo ya
mtoto, ni uwezekano wa kutumia mbinu zinazodhibiti mfumo wa kompyuta.
Kwa utaratibu huo watoto hawawezi kuingiza program mpya au kuweka
windozi tofauti ambazo ni rahisi kuweza kuwaharibu watoto.
Njia nyingine ni pamoja na kuzuia
kuondolewa program zilizopo katika kompyuta au kuzizuia zisifanye kazi,
ni moja ya njia ambazo zinaweza kutumiwa katika kuwadhibiti watoto.
Miongoni mwa njia nyepesi zaidi
kwa wazazi katika kumlinda mtoto wao wakati wa kutumia njia na nyenzo
zinazohusiana na ulimwengu wa intaneti, ni kuweka mfumo wa kompyuta nje
ya chumba chake cha kulala. Njia hiyo itawasaidia wazazi wakati wa
kutumia mtoto chombo hicho nao waweze kushuhudia na kufuatilia kwa
karibu michezo na shughuliza zote za mtoto huyo anapotumia kompyuta.
Kwa hakika vivutio vya kompyuta
na michezo mingine ya kielektroniki kwa watoto havina kikomo, na ikiwa
hakutakuwepo usimamizi madhubuti wa wazazi kwa mtoto wao, basi huenda
mtoto bila kujijua, akatumia wakati mwingi zaidi kuliko inavyotakiwa na
hivyo kuathiri lishe, usingizi na hata masomo yake.
Hapo ndipo wazazi wanapotakiwa
kuwa macho na kuhakikisha wanasimamia vyema malezi ya mtoto wao sanjari
na kumuandalia ratiba nzuri ya maisha yake na kuchunga sheria
watakazomuainishia kila wiki.
Aidha wazazi wanatakiwa kumuweka
mbali mtoto wao na ulimwengu wa elektroniki na michezo ya kompyuta
wakati wa kipindi cha masomo. Watafiti wanasema kuwa, kuna ulazima
mkubwa wa kuzingatiwa wakati wa matumizi ya watoto kwa vyombo vya umeme
kama vile kompyuta, labtop na tablet na kile ambacho kinahusiana na
ulimwengu wa kielektroniki, kwani utafiti unaonyesha kwamba matumizi
mengi ya vyombo hivyo kupita kiasi na kufikia kiwango cha uraibu,
hupunguza uwezo wa kifikra wa mtoto.
Na kukithiri kwa maradhi hayo
kwa watoto ndio mwanzo wa kufeli katika hatua zao za kielimu sanjari na
kushindwa kukabiliana na mikikimikiki mingine ya kimaisha ambayo
anapaswa kukabiliana nayo katika mustakbali wa maisha yake ya mbeleni.
Katika matumizi ya michezo ya
kompyuta au ulimwengu wa intaneti, kuna udharura wa kujitenga na mambo
machafu yasiyofaa. Aidha inaelezwa kuwa, kutumia sana kompyuta na
intaneti, taratibu huibua tatizo la unene, ambalo mara nyingi hupelekea
watoto na hasa vijana wengi kujichukia wenyewe kutokana na tatizo hilo.
Hivyo kuna haja kwa wazazi kuwaepusha watoto wao na unene na uzembe
unaosababishwa na matumizi ya muda mrefu ya vyombo vya umeme hasa
michezo ya kompyuta.
Wataalamu wengi wanaamini kuwa,
ni muhimu kuwatenga watoto walio na umri wa chini ya miaka mitatu na
aina yoyote ya matumizi ya kompyuta. Kwa maana nyingine ni kwamba, umri
huo hauoani na matumizi ya kompyuta au video.
Hata hivyo ikiwa mtoto aliye na
umri wa chini ya miaka mitano ataingia katika ulimwengu wa matumizi ya
vyombo hivyo na kuvizoea, basi lazima awekewe sheria na vidhibiti
maalumu vya kumuwezesha kukabiliana na hatari ya ulimwengu huo. Kwanza
anapasa kufahamishwa ni kwa kipindi gani anatakiwa atumie vyombo hivyo
na kisha baada ya hapo ajishughulishe na kazi nyingine.
Watafiti wanapendekeza kuwa,
mtoto mwenye umri wa kuinukia anatakiwa atazame kwa saa moja au masaa
mawili filamu na katuni, upekuzi katika intaneti na michezo mingine ya
video katika kompyuta. Ikiwa mtoto kwa siku atatumia dakika 45 kucheza
mchezo wa kompyuta na muda mwingine mdogo kutazama televisheni na
mwingine mfupi kujishughulisha na harakati za kifizikia, basi
hakutakuwepo na wasi wasi wa kuathirika afya yake. Lakini ikiwa atatumia
masaa mengi kujishughulisha na michezo ya kompyuta zaidi ya kiwango
kinachotakiwa, basi hatua za haraka zinapaswa kuchukuliwa ili
kukabiliana na hali hiyo.
Madaktari wanashauri kwamba,
watoto wanatakiwa kutumia masaa mawili tu kwa siku kutazama televisheni.
Televisheni ina athari nyingi muhimu kwa watoto wengi wanaosoma na hasa
katika kupumzisha mwili na fikra zao.
Hivyo wazazi na walimu wanatakiwa
kusimamia ni kiasi gani watoto wanapaswa kutazama televisheni. Hii ni
katika hali ambayo katika miaka ya awali watoto wanaosoma shule za
msingi, huwa hawana uwezo wa kupanga vyema ratiba za kutazama
televisheni.
No comments :
Post a Comment