Mkurugenzi wa Divisheni ya
Mashauri ya Madai na Usuluhishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa
Serikali, Obadia Kameya akifungua semina ya elimu ya sheria za kodi
iliyofanyika katika ukumbi wa Benki Kuu ambapo washauri wa masuala ya
kodi walijadili namna ya utekelezaji wa mabadiliko mbalimbali katika
sheria za kodi nchini.
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa
Mlipakodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Richard Kayombo
akizungumza wakati wa semina ya kujadili namna bora ya utekelezaji wa
mabadiliko katika sheria za kodi iliyofanyika katika ukumbi wa Benki Kuu
ya Tanzania.
Washauri wa masuala ya Kodi (Tax
Consultants) walioshiriki katika semina ya kujadili namna bora ya
utekelezaji wa mabadiliko ya sheria za kodi nchini iliyotolewa na
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kushirikiana na kampuni ya ushauri
wa masuala ya kodi ya Hanif Habib & Co.Semina hiyo ilifanyika katika
ukumbi wa Benki Kuu jijini dar es Salaam.
Washauri wa masuala ya Kodi (Tax
Consultants) walioshiriki katika semina ya kujadili namna bora ya
utekelezaji wa mabadiliko ya sheria za kodi nchini iliyotolewa na
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kushirikiana na kampuni ya ushauri
wa masuala ya kodi ya Hanif Habib & Co.Semina hiyo ilifanyika katika
ukumbi wa Benki Kuu jijini dar es Salaam.
………………………………………………………..
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
imeendesha semina ya siku moja kwa washauri wa
masuala ya kodi zaidi ya
100 kutoka taasisi mbalimbali nchini ili waweze kutoa tafsiri fasaha za
sheria za kodi kwa wafanyabiashara wanaowahudumia.
Akifungua semina hiyo Jijini Dar
es Salaam jana kwa niaba ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mkurugenzi wa
Divisheni ya Mashauri ya Madai na Usuluhishi, Bw. Obadia Kameya alisema
semina hiyo imekuja wakati muafaka ambapo Serikali imejipanga kuzuia
mianya ya ukwepaji kodi.
Bw.Kameya alisema ukusanyaji wa
kodi ndio chanzo kikubwa cha mapato ya Serikali hivyo ni wazi kuwa TRA
inategemea ushirikiano mkubwa kutoka kwa wadau wengine wakiwemo washauri
wa masuala ya kodi ambao watasaidia kupeleka elimu fasaha ya tafsiri za
sheria za kodi na kuchochea ulipaji wa kodi kwa hiyari kutoka kwa
wafanyabiashara hivyo kupelekea nchi kuwa na maendeleo.
“Serikali inaamini kuwa semina
kama hizi ni muhimu sana kwa wadau wa kodi kwa kuwa inatoa fursa ya
kujadiliana ili kuongeza utashi na uelewa wa haki na wajibu wa kulipa
kodi hivyo kusaidia kuchochea utamaduni wa kulipa kodi kwa hiyari ambao
kwa kiasi kikubwa kutaongeza makusanyo na hatimaye kukuza uchumi,”
alisema Bw.Kameya.
Aidha Mkurugenzi huyo alisema
Serikali itaendelea kuwathamini na kuwajengea uwezo wadau wa masuala ya
kodi ili waweze kuelimisha wengine na kusimamia vizuri walipa kodi na
wananchi kwa ujumla wajue umuhimu wa kulipa kodi kwa kuwa ni jukumu la
kila mtanzania anayetakiwa kulipa kodi, kulipa kwa hiyari.
Naye Mkurugenzi wa Huduma na
Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Bw. Richard Kayombo alisema vikao vya aina
hiyo ni muhimu kwani vinatoa nafasi kwa wadau kujadiliana kuhusu fursa
na changamoto zinazotokana na ukusanyaji wa kodi kwa nia ya kuimarisha
mahusiano mazuri pamoja na kujenga uchumi wa nchi kwa kuwa kodi ndiyo
msingi wa maendeleo.
“Kwa kupitia semina na mafunzo
mbalimbali tunayoendesha mara kwa mara kwa wadau na wananchi kwa ujumla
tumegundua kuna changamoto ya urasimu katika mchakato wa ulipaji kodi
hivyo Ili kupunguza urasimu, tumejitahidi kuimarisha miundombinu ya
kielektroniki itakayotuwezesha kukabiliana na changamoto mbalimbali za
ulipaji kodi”,alisema Kayombo.
Lengo la Serikali na TRA kwa
ujumla ni kuhakikisha mlipa kodi anatumia mitandao popote alipo kupata
huduma anazozihitaji badala ya kutumia muda mwingi kufika kwenye ofisi
zetu hivyo tumeanzisha baadhi ya programu kwenye mitandao
zitakazorahisisha upatikanaji wa huduma zetu zikiwemo za ulipaji wa
Ankara za Maji, umeme pamoja ving’amuzi, alisisitiza Bw.Kayombo.
“Kwa sasa TRA tunaboresha mifumo
ya mitandao inayorahisisha ulipaji kodi bila mfanyabiashara kutembelea
ofisi za TRA ambapo mlipakodi anaweza kupakua fomu na nyaraka mbalimbali
kutoka katika tovuti na kulipia benki kwa kutumia simu ya kiganjani na
hivyo kupunguza muda na kuepuka urasimu wakati wa kulipia,” alisema Bw.
Kayombo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa
Kampuni Binafsi ya Hanif Habib,Bi. Hanif Habib alisema mafunzo hayo
yamewakutanisha pamoja Maafisa wa Kodi,wataalamu pamoja na jamii ya
wafanyabiashara kutoka mashirika na taasisi mbalimbali za ndani na nje
ya nchi hivyo ni kielelezo cha ushirikiano kati ya Serikali na sekta
binafsi katika masuala ya maendeleo.
“Kukutana kwa wadau mbalimbali wa
kodi katika mafunzo haya hausaidii tu kuchochea ongezeko la mapato bali
kunahakikisha nchi inakuwa na maendeleo endelevu, kuchochea demokrasia
na uwajibikaji nchini, pamoja na kupunguza utegemezi”,alisema Bi.Hanif.
No comments :
Post a Comment