Katibu
Mkuu Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Profesa Elisante
ole Gabriel (wa nne kutoka kushoto) na Naibu Waziri wa Masuala ya
Utangazaji, Filamu na Habari wa China, Tong Gong (katikati), wakikata
utepe kuzindua maonyesho ya kwanza ya tamthiliya ya China ya ‘Mfalme
Kima’ iliyotafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili. Uzinduzi huo umefanyika leo
jijini Dar es Salaam. Wa pili kutoka kushoto ni Jiang Almin, ambaye ni
Mkurgenzi wa Radio China Kimataifa, wa pili kutoka kulia ni Suzan Mungy
(Mkurugenzi Mtendaji wa Huduma na Matukio wa Shirika la Utangazaji
Tanzania – TBC) na wa nne kulia ni Ma Li (Mkurugenzi wa Idara ya
Mawasiliano ya Kimataifa wa China).
Katibu
Mkuu Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Profesa Elisante
ole Gabriel, akizungumza wakati wa uzinduzi wa maonyesho ya kwanza ya
tamthiliya ya China ya ‘Mfalme Kima’ iliyotafsiriwa kwa lugha ya
Kiswahili.
Ma
Li, Mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano ya Kimataifa wa China,
akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika leo hii jijini Dar es
Salaam.
Mkurugenzi
Mtendaji wa StarTimes, Guo Zingi, akizungumza wakati wa uzinduzi wa
tamthiliya ya ‘Mfalme Kima’ ambayo ni ya Kichina iliyotafsiriwa kwa
Kiswahili.
Suzana
Mungy, Mkurugenzi Mtendaji wa Huduma na Matukio wa Shirika la
Utangazaji Tanzania (TBC) akizungumza wakati wa uzinduzi wa tamthiliya
ya Kichina ya ‘Mfalme Kima’ iliyotafsiriwa Kiswahili. Uzinduzi huo
umefanyika leo jijini Dar es Salaam.
Mkurgenzi wa Radio China Kimataifa, Jiang Almin, akizungumza wakati wa uzinduzi huo.
Meza kuu ya wageni wa heshima katika uzinduzi huo.
Akinadada
wa StarTimes wakiwa wamejiandaa kabla ya kukatwa kwa utepe kuashiria
uzinduzi wa maonyesho ya kwanza ya Tamthiliya ya China ya Mfalme Kima
iliyotafsiriwa kwa Lugha ya Kiswahili.
Wageni waalikwa wakifuatilia mambo yaliyokuwa yakiendelea.
Wasanii wakitumbuiza kwenye uzinduzi huo.
Wageni mbalimbali wakifuatilia.
Picha ya pamoja ya wafanyakazi wa StarTimes, wasanii wa wageni wa heshima.
Na Dotto Mwaibale
SERIKALI
ya China kupitia Wizara ya Utamaduni ya nchi hiyo imeombwa kutangaza
filamu za Tanzania nchini humo ili kuutangaza utamaduni wa Watanzania.
Wito huo
umetolewa jijini Dar es Salaam leo hii na Mkurugenzi Mtendaji wa Huduma
na Matukio wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Suzana Mungy, wakati
akitoa hotuba kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TBC katika hafla ya
uzinduzi wa maonesho ya kwanza ya Tamthiliya ya China ya (Mfalme Kima)
ya lugha ya Kiswahili uliofanyika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa
Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam leo.
“Ni vema
sasa na wenzetu wa China wakawa wanaonesha filamu zetu huko kwao kwa
lugha ya Kichina ili kusaidia kutangaza utamaduni wetu,” alisema Mungy.
Mungy
alisema Wachina wamekuwa wakionesha filamu zao hapa nchini ambazo
zimeingizwa sauti kwa lugha ya Kiswahili na Watanzania hivyo ili kupanua
wigo wa mahusiano katika tasnia hiyo ni vema pande zote mbili
zishirikiane kuandaa tamthiliya ya pamoja ya lugha ya Kiswahili.
Mkurugenzi
Mtendaji wa StarTimes, Guo Zingi, alisema kwamba kampuni yake
imejizolea mashabiki wengi nchini Tanzania kutokana na kuonesha filamu
na tamthiliya nyingi za Kichina zilizotafsiriwa Kiswahili, lugha ambayo
inaeleweka.
Alitolea
mfano tamthiliya ya Maudodo, kama mojawapo ya tamthiliya hizo ambayo
ilijizolea umaarufu kwa watu wa rika zote nchini Tanzania.
Aidha,
amekiri kwamba, kwa sasa ziko tamthiliya na filamu nyingi za Kichina
zinazotazamwa nchini Tanzania ambazo zimetafsiriwa Kiswahili.
Alisema
mapema mwaka 2016 kampuni hiyo ilifanya mashindano ya kuwapata vijana 10
wa Kitanzania waliopelekwa China kwa lengo la kwenda kuingiza sauti za
Kiswahili katika filamu na tamthiliya mbalimbali za Kichina, hatua
ambayo imesaidia kuzifanya tamthiliya hizo zipendwe na kukubalika nchini
Tanzania.
Naibu
Waziri wa Masuala ya Utangazaji, Filamu na Habari wa China, Tong Gong,
alisema uhusiano huo baina ya Tanzania na China utaendelea kudumishwa
katika masuala ya utamaduni kama iliyo katika maeneo mengine maendeleo.
Kupitia tamthiliya mbalimbali, watakuwa wakibadilisha utamaduni baina ya nchi hizo mbili.
Naye
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Profesa
Elisante ole Gabriel, alisema Tanzania na China wataendelea kushirikiana
na kudumisha uhusiano ulioasisiwa na waasisi wa mataifa hayo – Mwalimu
Julius Nyerere na Mao Tsetung.
“Kwa kuwa
wenzetu China mko juu katika teknolojia ya utangazaji na mawasiliano,
ninawaomba muangalie namna ya kuisaidia Tanzania katika tasnia ya sanaa
na utamaduni ili na wasanii wetu nao kazi zao ziweze kupata masoko
huko,” alisema Profesa Ole Gabriel.
No comments :
Post a Comment