Mhandisi Mshauri wa Kitengo maalum
cha Wahandisi Washauri Wazawa kutoka Wakala wa Barabara Nchini (TECU),
Eng. Mushubira Kamuhabwa (kulia), akitoa taarifa kwa Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (kushoto), kuhusu mradi
wa ujenzi wa barabara ya Kyaka-Bugene KM 59.1 kwa kiwango cha lami,
wilayani Karagwe, mkoa wa Kagera.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akiruka mtaro wa maji uliopo
pembezoni mwa barabara ya Kyaka-Bugene KM 59.1 inayojengwa kwa kiwango
cha lami, wilayani Karagwe, mkoa wa Kagera.
Muonekano wa sehemu ya barabara ya
Kyaka-Bugene KM 59.1 inayojengwa kwa kiwango cha lami, wilayani
Karagwe, mkoa wa Kagera. Barabara hiyo inajengwa na mkadarasi kutoka
Kampuni ya CHICO na imegharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 64.96.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akitoa maelekezo kwa Mhandisi Jumanne
Werema (wa kwanza kulia), kuhusu kukamilisha ujenzi kwa wakati wa Shule
ya Msingi Tumaini iliyopo eneo la Mafumbo, wilayani Bukoba, mkoa wa
Kagera.
Mhandisi Jumanne Werema kutoka
Kampuni ya ujenzi wa CMG akimpa taarifa ya mradi Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa kuhusu hatua iliyofikiwa
ya ujenzi wa Shule ya Msingi Tumaini iliyopo eneo la Mafumbo, wakati
alipokagua, wilayani Bukoba, mkoa wa Kagera.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (katikati), akiongozana na Mhandisi
Salum Chanzi (kushoto), kutoka Wakala wa Majengo nchini (TBA), pamoja na
Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Bw. Deodatus Kinawiro (kulia), kukagua
maendeleo ya ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Ihungo mkoani
Kagera iliyoharibiwa na tetemeko la ardhi takriban miezi sita iliyopita.
Moja ya Jengo la Shule
ya Sekondari ya Wavulana ya Ihungo linalojengwa na Wakala wa Majengo
Nchini (TBA), baada ya Shule hiyo kuathiriwa na tetemeko la ardhi
takriban miezi sita iliyopita, mkoani Kagera.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
………………..
Serikali imesema haitavumilia
wala kusita kumchukulia hatua yeyote anayevamia na kujenga katika
hifadhi za miundombinu ya barabara na reli kwani kufanya hivyo ni kosa
kisheria.
Akizungumza na waandishi wa habari
wilayani Karagwe, mkoani Kagera mara baada ya
kukagua barabara ya Kyaka
hadi Bugene yenye urefu wa kilometa 59.1, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amewataka wananchi kuacha dhana ya
kuingilia miundombinu hiyo kwa imani ya kulipwa fidia na Serikali.
“Najua bado kuna watu wanaendelea
kuvamia miundombinu ya usafirishaji, sasa nasema kuwa Serikali
itaendelea kubomoa pasipo kulipa fidia kwa yeyote anayevunja sheria”,
amesema Profesa Mbarawa.
Kuhusu mradi wa ujenzi wa barabara
hiyo, Waziri Profesa Mbarawa amekipongeza Kitengo maalum cha Wahandisi
Washauri Wazawa (TECU), kinachosimamiwa na Wakala wa Barabara nchini
(TANROADS), kwa kusimamia ujenzi wa barabara hiyo kwa kuzingatia viwango
na kuwataka kuendelea kuimarisha kitengo hicho ili kiweze kufikia
hatua ya kujenga barabara nchini.
Aidha, amewataka viongozi wa
wilaya hiyo kuwahamasisha wananchi wake kuilinda na kuitunza barabara
hiyo ili iweze kudumu kwa muda mrefu kama ilivyokusudiwa.
Kwa upande wake, Mhandisi Mshauri
wa mradi huo Eng. Mushubira Kamuhabwa, amesema kuwa kazi inaendelea
vizuri kwani mpaka sasa mradi huo umefika asilimia 98 ambapo kazi
iliyobaki ni uwekaji wa alama za barabarani.
Eng. Kamuhabwa ameongeza kuwa
kukamilika kwa barabara hiyo kutarahisisha usafirishaji wa mizigo na
abiria kutokana na barabara hiyo kuwa kiungo kati ya Tanzania na nchi
jirani za Uganda, Rwanda na Burundi.
Mradi wa ujenzi wa barabara ya
Kyaka hadi Bugene umejengwa na kampuni ya CHICO kutoka nchini China na
kugharimu kiasi cha shilingi bilioni 64.96.
Katika hatua nyengine Waziri
Mbarawa ametembelea na kujionea maendeleo ya ujenzi wa shule ya
Sekondari ya wavulana ya Ihungo mkoani Kagera iliyoharibiwa na tetemeko
la ardhi takriban miezi sita iliyopita.
Akiwa katika shule hiyo Profesa
Mbarawa ameridhishwa na kasi ya mkandarasi anayejenga shule hiyo na
kusema nia ya Serikali ni kuijenga shule hiyo kwa ubora wa hali ya juu
ili kukabiliana na majanga mbalimbali.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Bukoba,
Bw. Deodatus Kinawiro pamoja na mambo mengine ameishukuru Serikali kwa
kuwajali wananchi wake na kuijenga shule hiyo kwa ubora wa hali ya juu.
Ni takribani miezi sita tangu
kutokea kwa tetemeko la ardhi mkoani Kagera na kuharibu miundombinu
mbalimbali ikiwemo ya barabara, madaraja, hospitali, shule pamoja na
makazi ya watu.
Kutokana na uharibifu huo Serikali pamoja na wadau mbalimbali ilianza juhudi za ukarabati na ujenzi wa miundombinu hiyo.
No comments :
Post a Comment