*Amtaka Waziri wa Maji avunje mkataba ifikapo Mei 31
*Ni mkandarasi aliyenyang’anywa pasipoti na Rais Magufuli
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amesema Serikali haitavumilia wakandarasi wasio na uwezo na ambao
wanapewa kazi lakini wanashindwa kuzimaliza katika muda uliopangwa.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo, leo
(Alhamisi, Machi 30, 2017) wakati akizungumza na
watumishi wa
Halmamshauri ya Chalinze na wale wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa
Mazingira (CHALIWASA) katika ofisi zao, karibu na daraja la mto Wami,
wilayani Bagamoyo, mkoani Pwani.
Alikuwa ameenda kukagua mradi wa
upanuzi wa mtambo wa maji Chalinze na ujenzi wa mfumo wa kusafirisha na
kusambaza majisafi pamoja na matenki ya kuhifadhia maji ambao umechukua
muda mrefu lakini haujakamilika. Awamu ya kwanza ilianza mwaka Septemba
mosi 2001 na kukamilika Desemba mosi 2003.
Amemuagiza Waziri wa Maji na
Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge ahakikishe kuwa kazi ya ujenzi wa
mradi huo inaimarika na kufikia asilimia 80 la sivyo, wakamilishe
taratibu za kukatisha mkataba na kutafuta mkandarasi mwingine.
Agizo la Waziri Mkuu linafuatia
taarifa aliyopewa kwamba mkandarasi wa mradi huo, Overseas
Infrastructure Alliance (OIA) Pvt Ltd ya India alipaswa kumaliza kazi
hiyo Februari 22, mwaka huu lakini hadi sasa mradi huo umekamilika kwa
asilimia 23 tu.
“Nimeelezwa kwamba mmempatia
nyongeza ya siku 100 ambayo inaisha tarehe 31 Mei 2017, kama kazi yake
haitakuwa ya kuridhisha na kufikia walau asilimia 80, itabidi Mheshimiwa
Waziri uendelee na taratibu zako za kukatisha mkataba, tuanze kutafuta
mkandarasi mwingine,” amesema.
“Hii kampuni niliikuta Lindi
kwenye mradi mwingine wa maji kama huu. Nilitoa maagizo ya kuharakisha
ujenzi ukamilike lakini hawakufanya hivyo hadi Mheshimiwa Rais alipoenda
na kuagiza mkandarasi anyang’anywe pasi yake ya kusafiria mpaka
atakapomalizia kazi.”
“Kwa kifupi ni kwamba hii kampuni
haina uwezo wa kufanya hizi kazi, na ndiyo maana hadi sasa wamekamilisha
asilimia 23 tu ya mradi wakati walipaswa kuwa wamemaliza hivi sasa,”
amesema Waziri Mkuu na kuongeza: “Mheshimiwa Waziri endelea na utaratibu
wa kuwaondoa kisheria sababu hata tukiwaongezea muda bado
hawatakamilisha kazi.”
“Nimesikitika sana kukuta
mkandarasi hajafikia malengo. Mtu akipewa kazi anapaswa awe na uwezo wa
kifedha wa kuifanya ile kazi ili hata Serikali ikichelewesha malipo
yake, yeye aendelee na kazi,” ameongeza Waziri Mkuu.
Akizungumzia kuhusu ufanisi wa
mradi huo, Waziri Mkuu amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa CHALIWASA, Eng.
Christer Mchomba, ahakikishe kuwa wanapeleka maji hadi majumbani mwa
wateja na kuweka mita ili wananchi waweze kulipa bili zao badala kuishia
kutoa huduma hiyo kwenye vioski (viula).
“Kazi ya kupeleka maji majumbani
ni yenu CHALIWASA na siyo ya Wizara. Pelekeni maji na mfunge mita ili
watumiaji waweze kulipa bili zao. Pia toeni elimu kwa wananchi kupitia
mikutano ya hadhara, waelezeni mipango yenu na wapi mlipofikia. Kazi
yenu siyo kutandika mabomba tu, bali kutekeleza majukumu mliyopewa kwa
niaba ya Serikali,” amesema.
Kuhusu mitambo inayotumika, Waziri
Mkuu amesema mashine zilizopo ni za siku nyingi tangu 2003; hivyo
amemuagiza Waziri Lwenge afuatilie upatikanaji wa mashine za kisasa
kwani hilo suala ni kubwa na haliwezi kubebwa na CHALIWASA. “Bora
mngeanza kuagiza mashine mpya hivi sasa, badala ya kusubiri zichakae
kabisa, ndipo muanze kufikiria kuagiza.”
Mapema, akitoa taarifa ya mradi
huo, Eng. Mchomba alisema awamu ya tatu ya ujenzi wa mradi huo
ilisainiwa Mei 18, 2015 kati ya DAWASA na OIA yenye ubia na kampuni ya
Pratibha Industries kutoka India kwa gharama ya dola za Marekani milioni
41.36 ambazo zilikuwa ni fedha za mkopo nafuu kutoka benki ya Exim ya
India.
“Kazi zilizopangwa kufanyika ni
upanuzi wa mtambo wa maji ili kuongeza uzalishaji wa maji kutoka mita za
ujazo 500 hadi 900 kwa siku; ujenzi wa mfumo wa mabomba ya kusambaza
maji wenye kilometa 1,022; ujenzi wa matenki makubwa 19 ya kuhifadhia
maji; vituo tisa (9) vya kusukumia maji (booster stations) na vioski
(viula) vya kuchotea maji 351.”
Alisema hadi sasa mkandarasi huyo
amekwishalipwa dola za Marekani milioni 15.81 sawa na asilimia 38 na
anaendelea na ulazaji mabomba ambapo hadi sasa amekwishalaza mabomba
yenye urefu wa km.141 sawa na asilimia 12.4.
Alisema mradi huo umelenga
kuvinufaisha vijiji 68 ambavyo 19 kati ya hivyo viko Kaskazini mwa mto
Wami na 49 viko Kusini mwa mto huo.
Akizungumzia utendaji kazi wa
mkandarasi huyo, Eng. Mchomba alisema Serikali imechukua hatua za
kimkataba dhidi yake kwa kumtoza gharama ya kuchelewa kumaliza mradi
(liquidated damages) kuanzia Februari 23, 2017.
“Pia mkandarasi amepewa notisi ya
siku 100 ya kumtaka aongeze kasi ya kazi, vinginevyo tutasitisha mkataba
ifikapo terehe 31 Mei, 2017 kulingana na kipengele namba 8.7 cha
mkataba,” alisema.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMISI, MACHI 30, 2017.
No comments :
Post a Comment