- “Asema wasithubutu kuingia huko mtafungwa
NA MWANDISHI WETU
DAWA za kulevya ni moja kati
ya vitu vyenye madhara makubwa ambavyo vinachangia kuporomosha uchumi wa
Taifa kwa sababu yanaathiri vijana wengi ambao ndiyo nguvu kazi.
Hata hivyo dawa za kulevya
zimekua zikiigharimu Serikali kwa kutumia fedha nyingi katika
kupambana
na athari zitokanazo na matumizi dawa hizo, hivyo imewataka wananchi na
jamii kiujumla kutojihusisha na biashara hiyo haramu.
Mbali na dawa hizo
kulisababishia Taifa madhara ya kiuchumi na kiafya, pia biashara hiyo ya
dawa za kulevya inachafua na kushusha hadhi ya Tanzania kimataifa.
Madhara ya kiafya
yanayosababishwa na matumizi ya dawa za kulevya ni pamoja na kuathirika
kwa mfumo wa fahamu kwa mtumiaji ikiwa ni pamoja na kuchanganyikiwa,
kuwa na ulevi uliopindukia na hatimaye kusababisha kifo kama mtumiaji
atazidisha matumizi.
Katika kuhakikisha biashara
hiyo inakomeshwa Serikali imeunda Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa
za Kulevya nchini ambayo ndiyo inayoongoza mapambano hayo.
Jumatano ya Machi 22, mwaka
huu akiwa nchini Mauritius, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alizungumza na
Watanzania waishio nchini huko katika mkutano alioutisha kwenye hoteli
ya Meridien mjini Port Louis.
Akizungumza na Watanzania hao
aliwataka wajiepushe na masuala yahusuyo dawa za kulevya. Aliwataka
Watanzania wote wanaoishi nje ya nchi wazingatie sheria za Taifa husika
na kamwe wasijihusishe na biashara haramu ya dawa za kulevya.
“Vita ya dawa za kulevya ni
kubwa, hata hivyo Serikali tunaendelea kupambana nayo. Nchi ilikuwa
inapoteza vijana ambao walikuwa wamejiingiza katika biashara haramu ya
dawa za kulevya. Nawaomba msithubutu kuingia huko mtafungwa,” alisema.
Alisema katika kudhibiti
biashara hiyo haramu ya dawa za kulevya Serikali iliamua kuunda Mamlaka
ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) na inafanya kazi
vizuri. “Na tutakamata kila mtu anayejihusisha na biashara hiyo bila
kujali cheo, uwezo na mamlaka aliyonayo,”.
Aliongeza kuwa mamlaka hiyo
inafanya kazi ya kutafuta wazalishaji, watumiaji na wafanyabiashara,
lengo likiwa ni kuokoa vijana ambao wameshindwa kutimiza ndoto zao
kutokana na madhara waliyoyapata baada ya kutumia dawa za kulevya.
Waziri Mkuu alisema kuna
Watanzania wengi wamefungwa katika magereza mbalimbali duniani na
wengine wamehukumiwa kunyongwa baada ya kuthibitika kuwa wanajihusisha
na matumizi, usafirishaji na uuzaji wa dawa za kulevya, hivyo aliwataka
wawe mabalozi wazuri wa Tanzania kwa kujiepusha na dawa za kulevya.
Akizungumzia idadi ya watu
ambao hadi sasa wamekwishakamatwa katika nchi mbalimbali, Waziri Mkuu
alisema takwimu za jumla zinaonyesha kuwa Watanzania 515 wamekamatwa na
kufungwa gerezani kwa makosa ya kujihusisha na biashara ya dawa ya
kulevya.
“Nchini China Watanzania
walioko magerezani ni zaidi ya 200; Brazili kuna Watanzania 12; Iran
wako Watanzania 63; Ethiopia Watanzania saba na Afrika Kusini wako
Watanzania 296,” alisema.
Waziri Mkuu aliongeza kwamba
“Dawa za kulevya ni hatari sana kwa usalama na ustawi wa Taifa letu.
Vita hii inayopiganwa sasa dhidi ya uagizaji, uzalishaji, usambazaji na
matumizi ya dawa za kulevya ni kubwa. Sote kwa pamoja tunapaswa kuunga
mkono jitihada hizo,” alisisitiza.
Kwa mujibu wa taarifa
zililizopatikana ndani ya Jeshi la Magereza Tanzania hadi Machi 26,
mwaka huu kulikuwa na wafungwa 512 wanaotumikia vifungo vyao katika
magereza mbalimbali kutokana na makosa yanayohusiana na dawa za kulevya,
ambapo kati yake wanaume ni 491 na wanawake 21.
Mbali na wafungwa pia kuna
mahabusu 1,284 wanaoshikiliwa kwa tuhuma za kujihusisha na utumiaji,
usafirishaji na uuzaji wa dawa za kulevya, ambapo kati yao wanaume
ni1,166 na wanawake ni 118.
Katika hatua nyinngine, Waziri
Mkuu aliwataka Watanzania hao walioko nchini Mauritius kujenga
mshikamano wa pamoja na wawe na uzalendo na nchi yao. Pia wawe mabalozi
wazuri wa kutangaza vivutio vya Taifa.
Alisema ni vema wakatumia
fursa walizonazo katika kutafuta wawekezaji na kuwashawishi waje nchini
na kuwekeza kwenye sekta mbalimbali zikiwemo za viwanda, uvuvi, nishati
na utalii.
Kwa upande wake, Waziri wa
Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Khalid Salum
Mohammed aliwaomba Watanzania hao wazidishe mshikamano miongoni mwao kwa
kuwa umoja wao ndiyo nguzo yao.
“Mko hapa kwa ajili ya kutafuta
elimu na wengine mnafanya kazi, shughuli ambazo zitawasaidia kuboresha
maendeleo yenu na Taifa kwa ujumla, hivyo nawaomba mzingatie
kilichowaleta,” amesema.
Dkt. Khalid aliwahakikishia
Wanzania hao walioko nje ya nchi kuwa Tanzania iko salama na
wanaendelea kudumisha amani na utulivu kama walivyoiacha wakati
walipondoka.
Naye Mwenyekiti wa muda wa Umoja
wa Watanzania waishio nchini Mauritius, Bw. Donald Kongwa ambaye ni
Ofisa wa benki ya Standard Chartered nchini Mauritius alimuhakikishia
Waziri Mkuu kwamba kipato wanachokipata watakitumia kwa kuwekeza
Tanzania kwa lengo la kukuza uchumi wa Taifa.
Alisema wanaunga mkono na
kupongeza jitihada zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano katika
kujenga uchumi wa viwanda, mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi, ujenzi
wa miundombinu ya kisasa, ununuzi wa ndege pamoja na kuimarisha
uwajibikaji na nidhamu kwa watumishi wa umma.
Bw. Kongwa alisema Tanzania
ina nafasi kubwa ya kujifunza mambo mbalimbali nchini Mauritius kama
namna bora ya kuendesha kilimo cha miwa kwa sababu nchi hiyo inazalisha
zaidi ya tani 600,000 za sukari kwa mwaka na tani 530,000 inauzwa nje ya
nchi.”Tutumie fursa hii kujifunza zaidi ili tuweze kukuza uchumi
wetu,”.
Aliongeza kuwa mbali na
kujifunza kilimo cha miwa pia Tanzania inaweza kutangaza vivutio vyake
vya utalii nchini Mauritius ili kuwawezesha watalii wengi wanaoingia
nchini humo kuweza kuvifahamu na hatimaye kuwa nchini. Kwa mwaka
Mauritius inapata watalii zaidi ya milioni moja.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S.L.P 980, DODOMA
IJUMAA, MACHI 31, 2017
No comments :
Post a Comment