Na Lydia Churi- Mahakama, Tanga
Mahakama Kuu Kanda ya Tanga
inakusudia kuwanunulia Mahakimu wake 67 kompyuta Mpakato (Laptops) ili
kurahisisha kazi zao na kuondosha mashauri kwa wakati katika Mahakama
mbambali za mkoa wa Tanga.
Akizungumza kwa niaba ya Mtendaji
wa Mahakama Kuu kanda ya Tanga, Afisa Utumishi wa Kanda hiyo, Bwana
Farid Mnyamike amesema kompyuta hizo zitawasaidia waheshimiwa
Mahakimu
katika kuandika hukumu ili wananchi waweze kupati haki kwa wakati.
Alisema katika kanda yake, baadhi
ya Mahakama zina uhaba wa watumishi hasa Makatibu Muhtasi pamoja na
vitendea kazi jambo ambalo limekuwa likichelewesha utolewaji wa hukumu
pamoja na upatikanaji wa nakala za hukumu kwa wakati. Aliongeza kuwa kwa
Mahakimu kupatiwa kompyuta hizo kutarahisisha upatikanaji wa haki.
Aidha, Afisa Utumishi huyo
alisema hivi sasa Mahakama Kuu kanda ya Tanga inao mpango wa kuhakikisha
inazipatia umeme baadhi ya Mahakama za Mwanzo kupitia Mradi wa Umeme
vijijini (REA) ili kurahisisha upatikanaji wa nakala za hukumu kwa
wakati.
Mahakama ya Tanzania ilimwekea
malengo kila Hakimu nchini ya kuhakikisha anasikiliza kesi zaidi ya 250
kwa mwaka ili kuondosha mrundikano wa mashauri yaliyoko kwenye
Mahakama mbalimbali nchini.
Bwana Mnyamike aliitaja mipango
mingine iliyowekwa na Kanda yake katika kuitekeleza nguzo ya pili ya
Mpango Mkakati wa Miaka Mitano wa Mahakama ya Tanzania kuwa ni
kuwapeleka Mahakimu wenye mashauri machache kwenye Mahakama zenye
mashauri mengi ili kuhakikisha mashauri yote ya muda mrefu yanaondoshwa
na yaliyofunguliwa yanamalizika kwa wakati.
Ili kuleta mabadiliko ndani ya Mahakama, Mahakama ya Tanzania iliandaa Mpango Mkakati wa Miaka mitano 2015-2020
unaotekelezwa kupitia nguzo tatu ambazo ni Utawala bora, Upatikanaji wa
Haki kwa Wakati na pamoja na kurudisha na kujenga imani ya wananchi kwa
Mahakama.
No comments :
Post a Comment