Saturday, March 25, 2017

HATUTAKI KUFANYWA MATEJA TENA-DK. HARISSON MWAKYEMBE


mwakyembe
WAZIRI Mpya wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe  wa pili kutoka kulia na  mtangulizi wake Nape Nnauye Mbunge wa jimbo la Mtama wakishangilia timu ya Taifa Stars pamoja na viongozi wengine wakati timu hiyo ilipocheza mchezo wa kirafiki na timu ya Botswana kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam leo.
………………………………………………………………………………………………………………
Aahidi kupambana hadi kombe la Dunia
Ampongeza Nape kwa kuunda Kamati ya ushindi
WAZIRI Mpya wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe ameanza
kazi katika Wizara mpya kwa pongezi kwa TFF kuasisi mageuzi ya Kandanda nchini.
 “Watanzania tumechoka na huu uteja, kusukumwa sukumwa tu kwenye soka. Ni hamu ya watanzania sasa tuonekane katika ulimwengu wa soka”, alisema
Waziri alienda mbali kwa kuiagiza Wizara yake yote ijikite kuhakikisha maandalizi ya Serengeti Boys yanakamilika kwa wakati.
“Nataka Wizara yangu yote sasa wimbo wetu uwe Serengeti Boys,” alisema Dk Mwakyembe jijini Dar Es Salaam leo, alipokutana na Kamati ya kuhamasisha ushindi wa Serengeti Boys.
Katika hafla hiyo, Dk Mwakyembe amempongeza mtangulizi wake Nape Nnauye kwa kuunda Kamati ya Serengeti Boys ili kutoa hamasa ya watanzania kwa timu yao.
Alisema Serengeti Boys ni nyota wanaoinukia (upcoming stars) na wanampa sababu ya kuanza kwenda mpirani tena.
Waziri Dk Mwakyembe aliendelea kusema kuwa michezo ya leo inahitaji uwekezaji hivyo Wizara yake itahakikisha kuwa jukumu hilo analibeba.
“Naona kama imechelewa, lakini bado muda upo, tukimbie, nataka Wizara nzima wimbo wetu uwe Serengeti Boys”, alisema kwa hamasa kubwa.
Dk Mwakyembe amempongeza Rais wa TFF Jamal Malinzi na Mwenyekiti wa Kamati ya Serengeti Boys Charles Hilary kwa mafanikio ya program ya mageuzi ya soka nchini.
Naye Mkurugenzi wa michezo katika Wizara ya Habati, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Yusuf Dingo alisema sasa imechoka kuwa kichwa cha mwenda wazimu na hivyo Taifa limeazimia kucheza Kombe la Dunia kupitia vijana wa Serengeti Boys.
Rais wa Shirikisho la Kandanda Tanzania, Jamal Malinzi alisema kufuzu kwa Serengeti Boys kucheza fainali za AFCON mi sifa pekee na mwanzo mpya wa mageuzi makubwa ya soka la Tanzania.
Alisema maandalizi ya ushiriki wa fainali za AFCON zitahitaji takriban Shilingi bilioni moja.
Alisema mikakati mbalimbali imeandaliwa kuchangisha kiasi hicho cha fedha, ikiwa ni pamoja na kuandaa chakula cha hisani.
Waziri Mwakyembe amesema atahakikisha fedha hiyo inapatikana ili vijana wa Serengeti Boys waweze kufuzu kucheza kombe la dunia huko India mwishoni mwa mwaka huu.

No comments :

Post a Comment