Na Ismail Ngayonga -MAELEZO-Morogoro
SERIKALI Maafisa Habari na
Mawasiliano katika Wizara, Taasisi, Idara na Mamlaka za Mikoa na Wilaya
nchini wametakiwa kutangaza mafanikio ya miradi mbalimbali ya
maendeleo
iliyotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano
inayoongoozwa na Rais Dkt John Pombe Magufuli.
Hayo yamesemwa leo Mjini Morogoro
na Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt.
Hassan Abbas wakati alipokuwa akizungumza na Maafisa Habari na Maafisa
TEHAMA katika mafunzo ya uwekaji wa taarifa katika tovuti za Mikoa na
Halmashauri yanayofadhiliwa na Shirika la Misaada la Marekani (USAID) na
kusimamiwa na Ofisi ya Rais- TAMISEMI na Wakala ya Serikali Mtandao
(EGA).
Kwa mujibu wa Dkt. Abbas alisema
Serikali ya Awamu ya Tano inatekeleza miradi mikubwa ya maendeleo katika
Mikoa na Halmashauri zake, hivyo ni wajibu wa Maafisa Habari
kuhakikisha kuwa taarifa zinazowekwa katika tovuti hizo zinaonyesha
mafanikio ya Serikali katika utekelezaji wa miradi hiyo.
“Ipo miradi mikubwa
inayotekelezwa na Serikali ikiwemo miradi ya umeme vijiji, ambapo
Serikali imekuwa ikitoa fedha nyingi kwa ajili ya miradi hiyo, hivyo ni
wajibu wa Maafisa Habari kuhakikisha kuwa taarifa za utekelezaji wa
miradi inawafikia wananchi” alisema Dkt. Abbas
Aliongeza kuwa lengo la Serikali
ya Awamu ya Tano inayooongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magaufuli ni
kuleta matokeo ya haraka kwa wananchi wake, hivyo ni wajibu wa Maafisa
Habari kuhakikisha taarifa mbalimbali za mafaniko katika maeneo yao ya
kazi zinatangazwa kwa kuzingatia muda na wakati.
Dkt. Abbas alisema kuwa Serikali
ipo mbioni kuanza utaratibu wa kupima utendaji kazi wa Maafisa Habari na
Mawasiliano katika Wizara, Taasisi, Idara na Mamlaka za Mikoa na Wilaya
ili kuangalia ni kiasi gani wameweza kutangaza mafanikio ya Serikali
katika maeneo yao ya kazi.
Kwa mujibu wa Dkt. Abbas alisema
utaratibu huo wa upimaji utaweza kuainisha Wizara, Idara, Taasisi na
Mamlaka za Mikoa na Wilaya zinatoa na zisizotoa taarifa zake kwa umma,
ambapo taarifa hiyo itaweza kuwasilishwa katika Mamlaka za juu
Serikalini kwa ajili ya utekelezaji.
Aidha alisema kwa sasa suala la
utoaji wa taarifa kwa umma si suala la utashi badala yake ni matakwa ya
kisheria, hivyo Serikali inaandaa barua zitazoelezwa kwa Watendaji wakuu
katika mamlaka za Serikali Kuu na Serikali za Mitaa kuhusu umuhimu wa
utoaji wa taarifa kwa umma.
“Kwa sasa tuna sheria ya huduma
za habari na sheria ya haki ya kupata taarifa, ambazo zote zinasisitiza
na kutoa maelekezo kwa taasisi zote za umma kutoa taarifa kwa wananchi”
alisema Dkt Abbas.
Alisema kuwa ili kutekeleza vyema
majukumu yao msingi ni wajibu wa Maafisa Habari na Mawasiliano
Serikalini kuhakikisha kuwa wanatumia vyema mitandao ya kijamii katika
utoaji wa taarifa za Serikali, kwani kwa sasa ulimwengu upo katika
mabadiliko makubwa ya teknolojia ya habari na mawasiliano.
“Wananchi kwa sasa hawasubiri
tena kusoma gazeti linalotoka siku ya pili asubuhi au taarifa ya habari
katika redio na televisheni, badala yake wengi wao wamekuwa wakitumia
mitandao ya kijamii kupata taarifa za matukio ya moja kwa moja yanatokea
katika maeneo mbalimbali nchini, hivyo ni wajibu wetu kutumia mitandao
hiyo” alisem Dkt. Abbas.
Mafunzo hayo ya uwekaji wa
taarifa katika tovuti yamehusisha Mikoa 5 na halmashauri 33 zilizopo
katika mikoa ya Morogoro, Tanga, Simiyu, Kilimanjaro na Arusha.
No comments :
Post a Comment