Wednesday, March 29, 2017

DC WETE PEMBA AFANYA ZIARA YA KUSHTUKIZA NA KUBAINI MADUDU


821d2a9f-5576-4652-9691-7f0862ab788e
Na Masanja Mabula –Pemba ..
 
ZIARA za kushtukiza zinazofanywa na Mkuu wa Wilaya ya Wete Rashid Hadid Rashid bado zinaendelea na mara hii  zimebaini madudu kwa wafanyabiashara ya vyakula katika Mji wa Wete .
 
Akiwa eneo la Chasasa Mjini Wete ,Mkuu wa Wilaya  amebaini mazingira machafu ya biashara kwa muuza supu Suleiman Nassor (Ngamia ) ambaye amebainika kutozingatia masharti yanayotakiwa kisheria .
 
Wafanyabiashara wengine ambao Mkuu huyo wa Wilaya amewabainisha kwamba hawazingatii usafi wa mazingira ni wauza maandazi , chipsi pamoja na wauzaji wa vyakula kwenye migahawa
 
Akizungumza katika eneo hilo Mkuu huyo wa Wilaya ambaye pia  alikuwa amefuatana na maofisa mbali mbali wa Serikali , ametoa muda wa siku moja kwa mfanyabiashara huyo kuboresha mazingira ya biashara yake kinyume chake atafungiwa kufanya biashara.
 
Amesema mazingira ya biashara katika eneo hilo hayandani na sheria pamoja na kanuni za afya , hivyo mfanyabiashara huyo anatakiwa kuhakikisha mandhari ya eneo analouzia biashara yanaboreshwa na yakuwa safi ili kulinda afya za walaji .
 
“Nakupa muda wa siku moja uhakikishe mazingira katika eneo lako hili la biashara unayaboresha , huwezi kuuza chakula (supu) katika sehemu zilizochafu namna hii , baada ya siku moja maofisa wa afya watakuja kuangalia na ikiwa hali bado ni hii tutakufungia ”alisema  Mkuu wa Wilaya.
 
Aidha Mkuu huyo wa Wilaya ametumia fursa hiyo kuwaasa wafanyabiashara na wananchi wa Wilaya hiyo kila mmoja kuhakikisha anaweka safi mandhari  inayomzunguka ili kujiepusha na magonjwa ya mripuko ikiwemo matumbo ya kuharisha na kipindupindu .
 
Naye Afisa wa Afya Wilaya hiyo Mwarabu Nuhu Mwarabu amewataka wananchi kuondoa kasumba kwamba usafi wa maziningira utafanywa na  watendaji wa baraza la Mji pamoja na taasisi nyingine , bali wanapaswa kufahamu kamba maradhi yanapotokea hayachagui .
 
Amesema Wilaya ya Wete imekuwa ikikumbwa na maradhi ya mripuko hususani kipindupindu , na kuwatanabaisha kuchukua hatua za haraka na mapema kuimarisha usafi ili kujiepusha na maradhi hayo ambayo yanachangiwa na uchafu .
 
“Ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha maeneo yanayomzunguka anayaweka katika hali ya kupendeza , na ondoeni kusumba ya kwamba usafi utafanywa na baraza la Mji na taasisi za Serikali pekee kwani maradhi yanapotokea hayachagui ”alisisitiza Mwarabu .
 
Mmoja wa fanyabiashara Suleiman Juma Suleiman amewaomba wafanyabiashara wenzake kushiriki katika usafi wa mazingira maeneo yao ya biashara ili kufanya biashara zao ziweze kuwavutia wateja .
 
Ameeleza kwamba usafi sehemu za kazi  ni moja ya kivutio kwa wateja na kuwasisitiza wananchi kulifanya zoezi la usafi ni la kudumu na kuacha kushuhulika wakati wa mvua  tu kwani maradhi yanayotaka kuja hayasubiri msimu wa mvua .
 
Katika eneo la mfanyabiashara huyo miongoni mwa mapungufu yaliyobainika ni vyombo kutosafishwa , mavazi yake  hayakubaliki pamoja na kuuza supu sehemu isiyokuwa na kibanda (juani) jambo ambalo ni hatari kwa afya za walaji

No comments :

Post a Comment