Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Mkuu wa Wilaya ya Kilombero
mkoani Morogoro, James Ihunyo amewataka vijana wenye ulemavu
kuchangamkia fursa zitolewazo na Serikali pamoja na wadau mbalimbali ili
ziwasaidie kuboresha maisha yao.
Mkuu huyo wa Wilaya ya Kilombero
ameyasema hayo leo wakati alipokuwa akizungumza na
mwandishi wa habari
hii juu ya ushiriki wa walemavu katika Mradi wa Uwezeshaji Vijana
Kiuchumi (YEE) unaoratibiwa na shirika la Plan International.
Mhe. Ihunyo amesema asilimia
kubwa ya vijana wenye ulemavu wamekosa nafasi ya kupata elimu na wengine
wameishia njiani hivyo ili kuwafanya wawe sawa na vijana wengine
Halmashauri ina wajibu wa kuwapatia mafunzo ya ufundi ili waweze
kujiajiri na kujipatia vipato vitakavyowawezesha kujitegemea na
kupunguza utegemezi kwa kiasi kikubwa.
“Katika maeneo mbalimbali nchini
walemavu wamekuwa wakitengwa na wengine kufichwa ndani ikiaminika kuwa
hawawezi kufanya shughuli yoyote, kwa kupitia mradi wa YEE unaoratibiwa
na shirika la Plan International ninawaomba vijana walemavu kujitokeza
kwa wingi kuchangamkia fursa hiyo,”alisema Mhe. Ihunyo.
Ameongeza kuwa tangu mwaka 2015
mradi ulivyoanzishwa jumla ya vijana 1376 wameshapatiwa mafunzo chini ya
mradi huo lakini vijana wenye ulemavu ni 13 tu ambayo ni sawa na
asilimia 3 kati ya asilimia kumi iliyopangwa katika mradi huo hivyo
vijana walemavu wanatakiwa kujitokeza kwa wingi kwani mradi huo una
manufaa katika maisha yao.
Aidha, Mhe. Ihunyo ametoa wito
kwa watendaji wa Serikali za Vijiji, Kata na Vitongoji kujitahidi
kuwaibua vijana walemavu ili waweze kupatiwa mafunzo yatakayowasaidia
kuimarisha maisha yao pamoja na Taifa kiujumla.
Amefafanua kuwa Serikali
inashirikiana na Shirika hilo katika kutoa maeneo ya kufundishia pamoja
na kutoa mikopo inayotumika kama mitaji ya kuanzishia shughuli
mbalimbali kwa vijana wanaohitimu mafunzo hayo.
Kwa upande wake mzazi wa kijana
mwenye ulemavu, Menhad Limota amelishkuru shirika hilo kwa kuweza
kuwapatia vijana hao mafunzo ya ufundi pamoja na ushauri wa kitaalamu
ambao umewawezesha kufanya shughuli zao zinazowasaidia kupata fedha za
kujikimu.
“Miaka ya nyuma kabla mwanangu
hajapatiwa mafunzo alikuwa akinitegemea mimi kwa kila kitu lakini baada
ya mafunzo hayo ameweza kujiunga na walemavu wenzie na kuanzisha
shughuli mbalimbali ambazo kwa namna moja au nyingine zinamsaidia yeye
pamoja na sisi wazazi wake,”alisema Limota.
Mradi huo wa miaka mitatu 2015
hadi 2018 unatekelezwa kwa ushirikiano wa mashirika ya VSO, CCBRT, VETA,
UHIKI, CODERT pamoja na Serikali ya Tanzania huku ukiratibiwa na
Shirika la Plan International chini ya ufadhili wa Umoja wa Nchi za
Ulaya (EU)
No comments :
Post a Comment