Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
akimsikiliza Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo
alipokuwa akifafanua jambo katika kikao kilichoitishwa na Waziri Mkuu
kwenye Makazi yake Oysterbay jijini Dar es salaam Februari 27, 2017, kwa
ajili ya kujadili masuala ya madini. Watatu kushoto ni Waziri wa Fedha
na Mipango Dkt. Philip Mpango na ni Mkuu wa Mkoa wa Manyara Dkt. Joel
Bendera.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akisisitiza jambo katika kikao alichokiitisha kuhusu masuala ya
madini kati yake na viongozi wa Serikali, viongozi wa kampuni ya
uchimbaji madini ya Tanzanite One na baadhi ya wachimbaji wadogo ,kwenye
Makazi yake Oysterbay jijini Dar es salaam jana Februari 27, 2017.
.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akizungumza katika kikao alichokiitisha kuhusu masuala ya madini kati
yake na viongozi wa Serikali, viongozi wa kampuni ya uchimbaji madini ya
Tanzanite One na baadhi ya wachimbaji wadogo,kwenye makazi yake,
Oysterbay jijini Dar es salaam jana Februari 27, 2017.(Picha na Ofisi
ya Waziri Mkuu)
………………………………………………………………………
*Amuagiza Kamishna wa Madini aende Mererani
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amesema anafuatilia kwa makini minada ya madini
inayofanyika nchini kwa
sababu anazo taarifa za kukiukwa utaratibu kwenye minada hiyo.
Amesema ukiukwaji huo unachangia
kutobadilika kwa mapato ya mauzo yatokanayo na mnada hata kama kuna vito
viliyokakatwa au havijakatwa.
Ametoa kauli hiyo jana jioni
(Jumatatu, Februari 27, 2017) wakati akihitimisha kikao alichokiitisha
kwenye makazi yake Oysterbay jijini Dar es Salaam kilichojumuisha
Mawaziri wa Fedha pamoja na Nishati, Mkuu wa Mkoa wa Manyara na
watendaji wake, Mbunge wa Simanjiro, wamiliki wa mgodi wa Tanzanite One,
watumishi waliofukuzwa kazi na wachimbaji wadogo.
Alisema licha ya kuwa Kitengo cha
Uthaminishaji wa Madini ya Almasi na Vito cha Wizara ya Nishati na
Madini (TANSORT) kinasifiwa kwa kuongeza mapato ya madini, bado kuna
kazi ya ziada inabidi ifanyike kwenye minada hiyo ili Serikali iweze
kunufainika na madini hayo.
“Uzoefu wa kwenye minada ya
korosho unaonyesha kuwa wanaushirika ndiyo wanaiba fedha za wakulima.
Nimekuwa ninafuatilia kwa muda sasa uendeshaji wa hii minada na
sijaridhishwa na uendeshaji wake. Hakuna tofauti ya bei madini ya Tanzanite yanapokuwa yamekatwa au la,” alisema.
Kwa mujibu wa wataalamu wa madini
na vito, inapotokea kuna madini yamekatwa bei inapaswa kuwa juu
ikilinganishwa na madini ghafi yanapouzwa moja kwa moja.
Amemuagiza Kaimu Kamishna wa
Madini, Bw. Benjamini Mchwampaka (ambaye alihudhuria kikao hicho kwa
niaba ya Kamishna wa Madini) aende Mererani na kufuatilia utendaji kazi
wa mgodi wa Tanzanite One na suala zima la teknolojia zinazotumika
kiwandani hapo.
Waziri mkuu aliitisha kikao hicho
kufuatia ahadi aliyoitoa kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika
Mererani, wilayani Simanjiro, mkoani Manyara Februari 16, 2017 kwamba
akimaliza ziara ya mkoa huo ataitisha kikao na wawekezaji wa Tanzanite
One baada ya kupokea malalamiko kwamba hali ya watumishi ilikuwa nafuu
wakati kampuni hiyo ilipokuwa inamilikiwa na wazungu kuliko ilivyo hivi
sasa.
Ili kuhakikisha ukusanyaji wa
mapato katika sekta ya madini unaongezeka, Waziri Mkuu amemwagiza
Kamishna wa Mamlaka ya Mapato (TRA) aimarishe ukaguzi kwenye viwanja wa
ndege vya Arusha na Kilimanjaro (KIA),
“Kamishna wa TRA na watu wako
inabidi mjipange kwa sababu kuna njia nyingi za ukwepaji kodi
zinafanyika kwenye sekta ya madini wakiwemo hata hawa wachimbaji wadogo.
Simamieni utaratibu wa kufuatilia kodi, nendeni kule walipo, msisubiri
waje kuwaletea malipo ofisini. Wasipokuja je? Au wakija wakakuta mmetoka
ofisini je?” Alihoji Waziri Mkuu.
Akizungumzia kuhusu uelewa wa
sheria miongoni mwa wachimbaji wadogo, Waziri Mkuu alisema Wizara ya
Nishati na Madini kupitia kwa Kamishna wa Madini wanapaswa kutoa elimu
na uelewa wa kisheria kwa wachimbaji hao ili kupunguza migogoro ambayo
imekuwa ikijitokeza kwenye maeneo mengi nchini.
“STAMICO na Kamishna wa Madini
fanyeni kazi pamoja, waelewesheni wachimbaji wadogo kuwa uwepo wa vitalu
maana yake kuna mipaka ambayo pia inajumisha utoaji wa leseni kwa wenye
vitalu hivyo. Kwa hiyo, waelimisheni kuwa mtu hapaswi kwenda upande wa
pili wa mtu mwenye leseni, akifanya hivyo atakuwa anavunja sheria.”
“Ninyi ni wadau wakubwa wa sekta
hii kwa hiyo mnapaswa kushiriki katika zoezi la kutoa elimu. Mnayo
maeneo mengi ya uchimbaji lakini yana migogoro, mfano ni kule Ngaka na
Kiwira. Maeneo yote haya yanahitaji usimamizi mzuri. Mnayo Bodi,
Mwenyekiti yupo kwa hiyo mnatosha kuifanya kazi hii,” alisisitiza.
Katika hatua nyingine, Waziri
Mkuu amewataka wamiliki wa mgodi wa Tanzanite One waboreshe mahusiano
yao na vijiji vilivyo jirani na mgodi huo. “Kuweni karibu na wananchi
ili wajue umuhimu wenu na uwepo wenu na waweze kusaidia kulinda mali
zenu. Shirikianeni na Halmashauri na Baraza la Madiwani, tangazeni kazi
zenu za CSR ili wananchi wajue mmechangia nini katika kusaidia maendeleo
yao,” alisema.
Kuhusu suala la watumishi
waliofukuzwa kazi kwenye mgodi huo, Waziri Mkuu amemwagiza Katibu Mkuu
(OWM-Kazi, Ajira na Vijana), Bw. Erick Shitindi asimamie suala lao na
kuwapatia majibu kuhusu hatma ya suala hilo.
Watumishi hao walikuwa
wanawakilisha wenzao 201 ambao walifukuzwa kazi Februari 8, 2016 kwa
sababu ya kufuatilia maslahi yao vikiwemo malipo ya saa za kazi za ziada
(overtime), mishahara ya miezi miwili, malipo ya NSSF, vitendea kazi na
usalama wa kazi migodini
No comments :
Post a Comment