Katibu Mkuu Wizara ya Afya Bi.
Asha Abdalla akifungua Mkutano wa siku tatu wa matayarisho ya Mpango wa
kupambana na maradhi ya Polio Tanzania katika Ukumbi wa Zanzibar Beach
Resourt Mbweni.
Baadhi ya washiriki wa mkutano wa matayarisho ya Mpango wa kupambana na Polio wakifuatilia ufunguzi wa mkutano huo.
Mwakilishi wa Shirika la Afya
Ulimwenguni (WHO) kutoka Afrika Kusini Dkt. Mercy Kamupira akiwasilisha
mada katika mkutano unaozungumzia maradhi ya Polio unaofanyika Zanzibar
Beach Resourt Mbweni.
Washiriki wa mkutano unaojadili
ugonjwa wa Polio wakiwa katika picha ya pamoja na mgeni rasmi, Katibu
Mkuu Wizara ya Afya Bi. Asha Abdalla.
Picha na Makame Mshenga-Maelezo.
…………..
Na Ramadhani Ali/Maelezo Zanzibar
Wadau wa chanjo wa Tanzania na
nchi jirani wapo Zanzibar kwa ajili ya mkutano wa kutathmini maradhi ya
polio na matayarisho ya kuandaa mpango wa kukabiliana na maradhi hayo
iwapo yatajitokeza.
Akizungumza katika mkutano huo
unaofanyika Zanzibar Beach Hotel Mbweni, Mkurugenzi Kinga na Elimu ya
Afya Zanzibar Dkt. Fadhil Mohd Suleiman amesema maradhi ya polio sio
tatizao Tanzania kwa sasa, lakini bado hatupo salama kutokana na nchi
jirani kuendelea kusumbuliwa na maradhi hayo.
Amesema Tanzania mara ya mwisho
kuwa na mgonjwa wa polio ni mwaka 1997 lakini nchi ya Somalia, Jamhuri
ya Watu wa Kongo na Nigeria bado wanakabiliwa na maradhi hayo na watu
wake wanakuja kwa shughuli mbali mbali za maisha hivyo matayarisho ya
kujiandaa ni jambo muhimu.
Amewashauri wazazi kuendelea na
utaratibu wa kuwapeleka watoto wao katika vituo vya afya mara baada ya
kuzaliwa kupatiwa chanjo zote ili kuhakikisha maradhi hayo na mengine
yanayowasumbua hayarejei tena.
Meneja wa Kitengo cha chanjo
Zanzibar Dkt. Yussuf Haji Makame amesema hali ya chanjo iko vizuri baada
ya asilimia 95 ya watoto wanaostahiki kupatiwa chanjo kupatiwa chanjo
hizo.
Amesema kitengo hivi sasa
kinaendelea kufuatialia kwa karibu watoto wenye umri kuanzia miaka 15
wanapopata ulemavu wa ghafla ili kujua chanzo chake na amewataka wazee
wanapobaini kijana wao kupata tatizo hilo kumpeleka hospitali mapema.
Mwakilishi wa WHO Zanzibar Dkt.
Andemichael Ghirmay ameipongeza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa
juhudi kubwa za kupambana na polio na kufanikiwa kupewa cheti maalumu
mwaka 2015.
Amesema Shirika hilo litaendelea
kuunga mkono juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na serikali na ametaka
juhudi za pamoja za wadau na jumuiya za kimataifa kuhakikisha polio na
maradhi mengine yanayozuilika kwa chanjo sio tatizo tena Zanzibar.
Akifungua mkutano huo Katibu Mkuu
Wizara ya Afya Bi. Asha Abdalla amewataka wadau wa chanjo kutoridhika na
hatua iliyofikiwa ya kutokomeza Polio bali waendelee kuweka mikakati
bora zaidi itakayo hakikisha maradhi hayo hayarejei.
Mkutano huo wa siku tatu
unaowashirikisha wataalamu wa chanjo kutoka Shirika la Afya ulimwengu
(WHO) na Shirika la kuhudumia watoto (UNICEF) utaundaa Kamati ya Maafa
ya polio ya kujiweka tayari wakati wote kukabiliana nayo yatakapo
tokea.
No comments :
Post a Comment