Na: Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma
Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa
na Michezo Nape Nnauye amesema kuwa wasanii na watu wenye majina makubwa
ndio wanaoonekana zaidi katika athari za madawa ya kulevya ingawa wapo
wengi katika jamii wanayotumia madawa hayo.
Nape Nnauye ameyasema hayo leo
katika ukumbi wa Bunge, Mjini Dodoma alipokuwa akitoa majibu kwa
waandishi wa habari waliotaka kujua namna ambavyo wizara yake imelipokea
sakata la kukamatwa kwa wasanii ambao wanatuhumiwa kutumia madawa ya
kulevya.
“Kama wizara inayosughulikia suala
la wasanii tunaunga mkono juhudi zozote za kupambana na jambo hili kwa
sababu mwisho wa siku sehemu ya wadau wetu wanaathirika, hivyo basi
juhudi za kupambana nalo zinaokoa wadau wetu,” alifafanua Nape Nnauye.
Aliendelea kwa kusema kuwa kama
wizara inayosimamia wasanii wamekuwa wakijadili na kuzungumza juu ya
athari hizo za madawa ya kulevya kwa wasanii, aidha wapo wasanii ambao
Serikali imewasaidiwa kupata matibabu kutokana na athari za madawa hayo,
akiwemo mwanamuziki Rehema Chalamila anayefahamika kama Ray C.
Aidha amesema kuwa Mkuu wa Mkoa wa
Dar es Salaam, Paul Makonda ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na
Usalama wa Mkoa huo hivyo hawajibiki kuuliza Wizara hiyo anapotaka
kuchukua hatua zozote kwa wasanii waliopo ndani ya mkoa anaosimamia,
lakini anapohitaji anaweza kuiuliza wizara hiyo.
Nape Nnauye amesema kuwa ni kazi
kubwa sana kwa mtu kutengeneza jina (brand) lakini ni rahisi sana
kubomoa, hivyo basi ni vyema busara ikatumika katika kuwashughulikia
waathirika, vile vile watu wasihukumiwe kwa tuhuma.
Hivi karibuni Mkuu wa Mkoa wa Dar
es Salaam, Paul Makonda alitangaza majina ya watu wanaotuhumiwa kuuza
ama kutumia madawa ya kulevya wakiwemo wasanii, maaskari na
wafanyabiashara na kuwataka kuripoti Polisi kwa ajili ya mahojiano.
No comments :
Post a Comment