Meneja Mkuu wa kampuni ya
kuzalisha umeme kwa kutumia nishati ya jua ya Rafiki Power, Joanis
Holzigel (kushoto) akibadilishana mawazo na Mtaalam wa Nishati Jadidifu
kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Emillian Nyanda (kulia)
katika ziara ya wataalam wa nishati jadidifu kutoka Wizarani katika
wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara kwa ajili ya ukaguzi wa miradi ya
umeme.
Mmiliki wa kioski kilichonufaika
na huduma ya umeme jua kupitia kampuni ya Rafiki Power, Thadeo Bura
(kushoto) akielezea manufaa ya mradi wake katika ziara ya wataalam wa
nishati jadidifu kutoka Wizara ya Nishati na Madini katika wilaya ya
Simanjiro mkoani Manyara kwa ajili ya ukaguzi wa miradi ya umeme.
Moja ya kioski kilichonufaika na
huduma ya umeme jua kupitia kampuni ya Rafiki Power kilichopo katika
kijiji cha Komolo wilayani Simanjiro mkoani Manyara.
Mmiliki wa mghahawa wa chakula
ambaye ni mmoja wa wanufaika wa huduma ya umeme jua kupitia kampuni ya
Rafiki Power akionesha friji inayotumia nishati hiyo katika ziara ya
wataalam wa nishati jadidifu kutoka Wizara ya Nishati na Madini katika
wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara kwa ajili ya ukaguzi wa miradi ya
umeme.
Mmiliki wa kioski kilichonufaika na huduma ya umeme jua kupitia kampuni ya Rafiki Power, Thadeo Bura akielezea matumizi ya compressor
inayotumia nishati ya jua kwa matumizi mbalimbali, katika ziara ya
wataalam wa nishati jadidifu kutoka Wizara ya Nishati na Madini katika
wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara kwa ajili ya ukaguzi wa miradi ya
umeme.
……………….
- Kampuni yajipanga kupatia kaya 20,000 umeme wa uhakika mwaka 2022
Na Greyson Mwase, Manyara
Februari 14, 2017
Wananchi katika Wilaya ya
Simanjiro mkoani Manyara wamepongeza kampuni ya kuzalisha umeme kwa
kutumia nishati ya jua ya Rafiki Power iliyopo chini ya kampuni tanzu
ya E.ON
ya Ujerumani, kwa kuwapatia huduma ya umeme iliyopelekea kukua
kwa kasi ya maendeleo katika wilaya hiyo.
Waliyasema hayo leo katika ziara
ya wataalam wa nishati jadidifu kutoka Wizara ya Nishati na Madini
katika miradi ya umeme mkoani Manyara yenye lengo la kuangalia
utekelezaji wa miradi ya umeme, changamoto zake na kutoa ushauri wa
kitaalam.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake
katika kijiji cha Komolo kilichopo wilayani Simanjiro mkoani Manyara,
Thadeo Bura ambaye ni mmiliki wa duka la vifaa vidogo vya umeme jua na
bidhaa nyingine, alisema kabla ya kampuni ya Rafiki Power kuwekeza
katika kijiji hicho maisha yalikuwa ni magumu kwa kuwa hakukua na
nishati ya kuwawezesha kuanzisha miradi midogo midogo.
Alisema mara baada ya kupata umeme
kupitia kampuni ya Rafiki Power, ameweza kuanzisha duka kwa ajili ya
vifaa vidogo vya umeme jua, bidhaa nyingine na kutoa huduma nyingine kwa
wanakijiji wenzake.
Alisema huduma ya umeme imewekwa kwenye baadhi ya shule na hospitali hivyo kuboresha huduma za jamii.
Naye Joseph Hango ambaye ni
mmiliki wa saluni ya kunyoa nywele aliongeza kuwa uwepo wa nishati ya
umeme kupitia kampuni ya Rafiki Power umepelekea kuongezeka kwa kipato
kutokana na idadi ya wateja kuongezeka.
Aliiomba kampuni hiyo kuendelea na
juhudi za kusambaza umeme katika maeneo mengi ambayo hayajafikiwa na
huduma ya umeme ili kukuza uchumi wa wilaya na mkoa kwa ujumla.
Wakati huohuo, akizungumza katika
ziara hiyo Meneja Mkuu wa Kampuni ya Rafiki Power, Joanis Holzigel
alisema kuwa kampuni yake inatarajia kuongeza uzalishaji wa umeme ambapo
kaya 20,000 nchi nzima zinatarajiwa kunufaika na huduma ya umeme
ifikapo mwaka 2022.
Alisema kwa kutambua umuhimu wa
nishati ya umeme katika uchumi wa viwanda utakaopelekea nchi ya Tanzania
kuwa kwenye orodha ya nchi za kipato cha kati ifikapo mwaka 2025,
kampuni yake imeweka mipango ya muda mfupi na muda mrefu ambapo
inatarajia kufikia wateja 20,000 ifikapo mwaka 2022.
Akitaja miradi inayotekelezwa na
kampuni yake, Meneja Holzigel alisema katika mkoa wa Arusha kampuni yake
ina miradi minne katika maeneo ya Digodigo, Soitsambu, Ololosokowani,
na Malambo yaliyopo wilayani Ngorongoro na miradi mingine miwili
iliyopo katika maeneo ya Itaswi na Kwamtoro wilayani Kondoa, mkoani
Dodoma.
Aliongeza kuwa, mradi mwingine mmoja unaotekelezwa na kampuni hiyo ni wa Komolo/Temeke, uliopo Simanjiro mkoani Manyara.
No comments :
Post a Comment