Mkurugenzi Msaidizi Huduma za
Ajira kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu
Bw. Robert Masingiri akiwaeleza waandishi wa habari leo jijini Dar es
Salaam kuhusu Programu ya Kukuza Ujuzi Nchini inayoratibiwa na Ofisi
hiyo. Kushoto ni Afisa Habari wa Ofisi hiyo Bw. Ridhiwani Wema.
Afisa Habari Ofisi ya Waziri Mkuu
Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Bw. Ridhiwani Wema akiongea na
waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa Programu ya Kukuza Ujuzi
Nchini. Kulia ni Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Ajira kutoka Ofisi hiyo
Bw. Robert Masingiri
(Picha na Fatma Salum-MAELEZO)
………………………………………………………………………
Na Fatma Salum – MAELEZO
Serikali imetoa wito kwa vijana
kote nchini kuchangamkia fursa ya kupata ujuzi wa fani
mbalimbali
kupitia Programu ya Kukuza Ujuzi Nchini inayoratibiwa na Ofisi ya Waziri
Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi
Msaidizi Huduma za Ajira kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira
na Wenye Ulemavu Bw. Robert Masingiri wakati akizungumza na waandishi
wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu programu hiyo.
Masingiri alibainisha kuwa
programu hiyo ni muhimu kwa vijana kwani itawawezesha kupata ujuzi na
stadi stahiki ili kumudu ushindani katika soko la ajira ndani na nje ya
nchi.
“Utekelezaji wa programu hii ni
hatua za makusudi za Serikali za kukabiliana na kiwango kidogo cha ujuzi
miongoni mwa nguvu kazi ya Taifa.” Alisema Masingiri.
Aliongeza kuwa kiwango cha ujuzi
hakijafikia hatua nzuri ya kuiwezesha nchi kufikia uchumi wa kati hivyo
Serikali imetenga shilingi bilioni 15 kwa ajili ya programu hiyo na
utekelezaji wake umeanza mwaka wa fedha 2015/2016 hadi 2020/2021
“Programu hii inalenga kuziba
pengo kubwa lililopo la ukosefu wa ujuzi katika sekta za utalii, ujenzi,
viwanda, nishati na madini ambapo utawawezesha vijana wengi kuajirika
na kujiajiri.” Alisema Masingiri.
Akifafanua kuhusu mfumo wa
utekelezaji wa programu hiyo, Afisa Habari kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu
Bw. Ridhiwani Wema alisema kuwa programu hiyo inatekelezwa kwa
ushirikiano na wadau mbalimbali kwa njia ya uanagenzi (apprenticeship)
ambapo lengo ni kuwafunza vijana 3000 katika viwanda vya nguo na vijana
1000 katika sekta ya ngozi.
Wema aliongeza kuwa program hiyo
pia inatekelezwa kupitia urasimishaji wa ujuzi uliopatikana nje ya mfumo
rasmi (Recognition of Prior Learning) na vijana 3900 watarasimishwa
kupitia sekta ya ujenzi, utalii na ukarimu.
Aidha kupitia program hiyo
wahitimu 4000 watapata mafunzo kwa vitendo mahali pa kazi na wafanyakazi
13400 watapatiwa mafunzo ya kuongeza ujuzi.
“Ofisi ya Waziri Mkuu imesaini
mikataba na VETA na Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT) ili
watoe ujuzi kwa vijana kote nchini na kupitia programu hiyo mafunzo hayo
yanagharamiwa na Serikali , hakuna malipo.” Alieleza Wema.
Serikali imejipanga kuendelea
kukamilisha miongozo ya ukuzaji ujuzi kwa njia mbalimbali itakayowezesha
wadau kushiriki katika utekelezaji wa Programu ya Kukuza Ujuzi Nchini
ili kufikia sera ya kukuza viwanda na kujenga uchumi wa kati.
No comments :
Post a Comment