Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa
Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Mamkamba. (MB) akitoa Taarifa
kwa Umma kuhusu marufuku ya uzalishaji, uingizaji , usambazaji,na
matumizi ya vifungashio vya plastiki maarufu kama viroba vinavyotumika
kufungashia pombe kali, alipozungumza na waandishi wa habari Ofisini
kwake Mtaa wa Luthuli Jijini Dare es Salaam Leo.
Katikati Waziri wa Nchi Ofisi ya
Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba. (MB) akitoa
Taarifa kwa Umma kuhusu marufuku ya uzalishaji, uingizaji ,
usambazaji,na matumizi ya vifungashio vya plastiki maarufu kama viroba
vinavyotumika kufungashia pombe kali, kulia ni Katibu Mkuu wa Ofisi
hiyo Profesa Faustin Kamuzora na Kulia ni Mkurugenzi Msaidizi wa Idara
ya Mazingira, Waziri Makamba alizungumza na
waandishi wa habari Ofisini
kwake mtaa wa Luthuli Jijini Dare es Salaam Leo.
Mtakumbuka tarehe 20 Februari 2017
Ofisi ya Makamu wa Rais ilitoa tamko la Serikali la utaratibu
utakaotumika kutekeleza agizo la kusitisha utengenezaji, uuzaji na
matumizi ya pombe kali zinazofungashwa kwenye vifungashio vya plastiki
(viroba)kuanzia tarehe 1 Machi 2017. Utekelezaji wa katazo hili
utazingatia Ibara ya 8(1) (b) na 14, Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004
na Kanuni zake zilizotungwa kupitia kifungu 230 (2) (f) cha sheria hiyo,
na Sheria ya Leseni za Vileo Namba 28 ya mwaka 1968 pamoja na
marekebisho yake ya mwaka 2012.
Napenda kusisitiza na kuujulisha
umma wa Tanzania kuwa utekelezaji wa maamuzi haya ya Serikali kuhusu
usitishaji uingizaji, uzalishaji, uuzaji na matumizi ya vifungashio vya
plastiki vya kufungia pombe kali utaanza rasmi tarehe 01 Machi, 2017,
katika Mikoa yote ya Tanzania Bara. Operesheni ya kukagua utekelezaji wa
agizo la serikali la usitishaji utengenezaji, uuzaji na matumizi ya
pombe zinazofungashwa kwenye vifungashio vya plastiki itaendeshwa nchini
kote kuanzia tarehe 2 Machi 2017 kwa kupitia Kamati za Ulinzi na
Usalama na Kamati za Mazingira katika ngazi ya Mkoa, Wilaya, Tarafa,
Kata, Vijiji na Mtaa. Kamati hizi zitawajibika kuwasilisha taarifa za
operesheni wakati na baada ya operesheni hiyo Ofisi ya Rais Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa na nakala Ofisi ya Makamu wa Rais.
Mnamo terehe 24 Februari 2017,
kiliitishwa kikao cha Mawaziri na viongozi wa taasisi za Serikali
kujadili mpango wa utekelezaji wa zuio hili. Katika kikao hicho, Wizara
na taasisi za Serikali zilipewa majukumu mbalimbali, kama ifuatavyo:
- Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwa kuzingatia umuhimu wa ujazo katika utozaji kodi, imeanzisha mfumo wa stempu za Kielektroniki ili kudhibiti ujazo wakati wa uzalishaji kwa ajili ya kupata mapato stahiki. Aidha, Mamlaka itahakikisha kwamba wazalishaji na waingizaji nchini wa malighafi ya pombe kali (ethanol) wamesajiliwa na kwamba mfumo wa ufuatiliaji wa usambazaji malighafi hiyo unawekwa. Wazalishaji na waingizaji wa malighafi hiyo watawauzia wale tu ambao wamepewa kibali na pia watatakiwa kutoa taarifa kila baada ya miezi mitatu (3) ya kiasi cha ujazo kilichouzwa na wateja waliouziwa ambao wamesajiliwa. Uuzaji wa malighafi kwa watengezaji wa pombe kali ambao hawajasajiliwa itakuwa ni kosa la jinai kulingana na Sheria.
- Mkemia Mkuu wa Serikali ambaye ndiye msajili wa kemikali za viwandani na majumbani, atasajili makampuni na taasisi zinazoingiza kemikali za viwandani na majumbani nchini ikiwa ni pamoja na Ethanol. Msajili atawajibika kutoa taarifa sahihi za majina ya makampuni na watu binafsi na taasisi zinazohusika, kiasi kilichoingizwa na kimetumika, pamoja na madhumuni ya matumizi.
- Kulingana na sheria ya Leseni ya Vileo Na 28 ya Mwaka 1968 na marekebisho yake ya mwaka 2012, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa katika operesheni hii itaratibu zoezi hili katika mikoa, wilaya, tarafa, kata, vijiji na mitaa yote Tanzania bara kwa kuhakikisha kuwa wanaofanya biashara ya pombe ya kawaida na pombe kali (spirit) na watumiaji kinyume na masharti ya leseni za vileo wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.
- Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kupitia Shirika la Viwango Tanzania (TBS), katika operesheni hii watakukagua viwanda vyote vinavyojihusisha na uzalishaji wa vileo na vifungashio vya aina mbalimbali vya kufungia pombe kali kama vimekidhi viwango vya kitaifa Ukaguzi katika viwanda vya plastiki utachunguza kama kuna mitambo ya kuzalisha vifungashio vya plastiki kwa ajili ya pombe kali. Mitambo ya kuzalisha vifungashio vya plastiki kama haitumiki kwa kuzalisha bidhaa zingine katika kiwanda husika, mwenye kiwanda atalazimika kutoa ufafanuzi wa hatima ya mitambo hiyo. Mitambo ya kuzalisha vifungashio vya plastiki itakayokutwa inaendelea kuzalisha pombe kali na kufungashia vifungashio vya plastiki itakamatwa na kutaifishwa na wahusika watashtakiwa.
- Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Watoto na Wazee, kupitia Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na mabwana afya katika operesheni hii watatoa elimu kwa umma na kukagua maeneo yote yanayotumika kuhifadhia, kuuza na kusambaza vileo vya aina zote, na kushiriki kukamata vileo ambavyo vipo kinyume cha sheria na kanuni.
- Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, kupitia Idara ya Habari Maelezo, itasaidia kutoa elimu kwa umma kuhusu suala hili.
- Wizara ya Mambo ya Ndani, kupitia Jeshi la Polisi, na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, itashiriki katika operesheni, ikiwemo kwenye masuala ya inteligensia.
- Ofisi ya Makamu wa Rais na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira, wataratibu operesheni.
Kama tangazo letu la tarehe
20/2/2017 lilivyoonesha muda wa nyongeza unaweza kutolewa kwa
wazalishaji halali ambao wataonyesha ushahidi wa kuelekea kuhamia kwenye
teknolojia ya chupa, na kwamba watahitaji muda mchache kufanya hivyo,
na ambao watatimiza masharti kadhaa na kupata kibali maalum kabla ya
tarehe 28/2/2017. Hadi sasa Serikali imepokea maombi ya wazalishaji 9.
Tutangaza kesho iwapo kuna ambao wamekidhi masharti au la. Kanuni za
upigaji marufuku pombe hizi zipo tayari.
Pia tumepokea malalamiko kwa
wazalishaji wengi kwamba zoezi hili limekuja ghafla na wengine wana
malighafi na bidhaa kwenye maghala. Ukweli ni kwamba Serikali ilitoa
taarifa Bungeni, kuanzia mwezi Mei 2016, na mara kadhaa baada ya hapo,
na rekodi zipo, kuhusu hatua hizi. Vilevile, taarifa ya Serikali
iliyotangaza kupiga marufuku pombe za viroba ziliripotiwa kwa ukubwa
stahiki kwenye vyombo vya habari, ikiwemo kwenye ukurasa wa kwanza wa
gazeti la Mwananchi, mwezi Agosti 2016. Katika taarifa zote za nyuma,
Serikali ilitangaza kwamba hatua hiyo itaanza tarehe 1 Januari 2017.
Hatua hizi zimechelewa kwa miezi miwili. Iwapo, baada ya taarifa hizo za
Serikali, kuna mzalishaji ameagiza malighafi au kutengeneza au
kuhifadhi pombe za viroba, au kuchukua mkopo kwa ajili hiyo, atakuwa
amefanya hivyo akijua madhara yake.
Mwisho napenda kutoa wito kwa
wananchi wote kutoa ushirikiano katika utekelezaji wa zoezi hili la
upigaji marufuku matumizi ya pombe zinazofungashwa katika vifungashio
vya plastiki (viroba) kwa kutoa taarifa kwa vyombo husika ili wale
wanaozalisha na kuuza au kuhifadhi waweze kuchukuliwa hatua stahiki.
Zawadi itatolewa kwa watakaotoa taarifa zitakazowezesha kukamatwa kwa
watakaokiuka zuio hili.
OFISI YA MAKAMU WA RAIS
28/02/2017
28/02/2017
No comments :
Post a Comment