NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar
kimesema wakati wa kuvumilia baadhi ya Viongozi, watendaji na Wanachama
wanaowachafua na kuwakashfu wenzao kupitia mitandao ya kijamii
umekwisha badala yake kinaandaa taratibu za kuwachukulia hatua kali za
kinidhamu
wanaohusika na vitendo hivyo.
Msimamo huo ameutoa Naibu Katibu
Mkuu wa Chama hicho Zanzibar, Vuai Ali Vuai wakati akizungumza na
viogozi, watendaji na wafuasi wa chama hicho wa Jimbo la Malindi katika
ziara ya Siku 10 ya kuimarisha CCM katika Mkoa Mjini Kichama.
Amesema CCM kwa sasa inaandaa
utaratibu kupitia vikao vyake vya kikanuni kuwahita baadhi ya viongozi
wanaotuhumiwa kuhusika na tabia hizo ili kuwahoji na kuwapa nafasi ya
kujitetea ili vikao vinavyosimamia maadili viweze kuchukua hatua za
kinidhamu kwa watakaokutwa na hatia.
Vuai alieleza kuwa taasisi hiyo
imekuwa ikitoa onyo na tahadhari za mara kwa mara ili watu wenye tabia
hizo waache lakini baadhi yao wamekuwa hawataki kubadilika, hali ambayo
haiwezi kuvumiliwa kwa nia ya kulinda heshima na hadhi ya CCM na
serikali zilizopo madarakani.
Naibu Katibu Mkuu huyo alitoa
ufafanuzi huo kufuatia kusambazwa kwa habari za upotoshaji katika
mitandao ya kijamii zilizokuwa zikidai kuwa Rais wa Zanzibar Dkt.Shein
amevunja Baraza la Wawakilishi, hali iliyosababisha baadhi ya viongozi
na wanachama wa CCM kuandika maneno yasiyofaa kwa kuwashutumu viongozi
wenzao ndani ya chama hicho kinyume na utaratibu.
Alitoa wito kwa wafuasi wa CCM na
Wananchi kwa ujumla kufahamu kuwa Chama na Serikali ni mamlaka Kuu za
nchi hivyo zina utaratibu wake maalum wa kutoa taarifa mbali mbali
ambao ni rasmi na sio kupitia mitandao ya kijamii.
“ CCM ni Chama kinachoongozwa na
Katiba , maadili na taratibu hivyo kila jambo lina utaratibu wake na
hata suala la kukosoana ni lazima tufuate miongozo ya kikanuni lakini
sio kudhalilishana katika mitandao ya kijamii na sehemu zingine
zisizofaa kujadiliwa masuala ya Chama.
Kama hatujawachukulia hatua
stahiki watu wanaokiuka miongozo yetu ya Chama kuna hatari ya kutugawa
na yawezekana wanatumiwa na vyama vya upinzani kutengeneza mpasuko, na
mimi nikiwa ni mtendaji mkuu wa CCM Zanzibar sitowavumilia tena. “,
alifafanua Vuai.
Aidha amewasihi wafuasi wa Chama
hicho kuwa na tahadhari juu taarifa za upotoshwaji zinazotolewa na
vikundi vinavyoandaliwa na vyama vya upinzani kwani zina nia ya kuwagawa
wafuasi wa Chama hicho ili washughulikie propaganda hizo badala ya
kujiandaa na Uchaguzi wa Chama unaotarajia kufanyika mwaka huu.
Alisema kuwa baada ya Chama Cha
Wananchi CUF kususia Uchaguzi wa marudio na kushindwa kurudi serikali
kwa sasa wamekuwa wakitumia njia nyingine ya kuwaaminisha uongo na
kuwahadaa wafuasi wao mambo ambayo sio sahihi kupitia mitandao ya
kijamii.
Alilitaka Jeshi la Polisi Zanzibar
kuwatafuta watu wanaomiliki na kusambaza taarifa za uongo kupitia
mitandao ya kijamii kwa lengo la kuwachukulia hatua za kisheria kabla
hawajaingiza nchi katika machafuko.
Akizungumzia maandalizi ya
Uchaguzi wa Chama hicho na Jumuiya zake na kuwataka wafuasi wa CCM
kujitokeze kwa wingi kuwania nafasi mbali mbali zinazogombewa ili wapate
kuchagua na kuchaguliwa kwa misingi ya kidemokrasia.
Sambamba na hayo amewashauri
wafuasi hao kupokea kwa nia njema mabadiliko yanayofanyika ndani ya CCM
kwani lengo lake ni kutengeneza taasisi imara itakayokuwa na nguvu kubwa
kiuchumi na kisiasa.
Hata hivyo ametoa Rai kwa Viongozi
wa Chama na Jumuiya kujenga mazoea ya kuwatembelea wanachama wao
kuanzia ngazi za chini za taasisi hiyo kwa lengo la kujadili changamoto
zinazowakabili wananchi ili zipatiwe ufumbuzi unaofaa
No comments :
Post a Comment