Sunday, February 12, 2017

SHARIF-SHIRIKISHO LA VYUO VIKUU (CCM)LISIWE NYUMA KUKIPIGANIA CHAMA NA SERIKALI


tah1
Mlezi wa shirikisho la wanaafunzi wa vyuo vikuu (CCM)mkoani Pwani,,alhaj Abdul Sharif,akifunga mkutano ulioandaliwa na shirikisho hilo,kwa ajili ya kuchagua viongozi nafasi ya katibu,mwenezi na mhamasishaji..(Picha na Mwamvua Mwinyi)
tah2
BAADHI ya wanachama wa shirikisho la wanafunzi wa vyuo vikuu la Chama Cha Mapinduzi (CCM)mkoani Pwani wakipiga kura kuchagua viongozi wa nafasi zilizoachwa wazi ikiwa ni pamoja na katibu,mhamasishaji na mwenezi.(Picha na Mwamvua Mwinyi)
tah3
BAADHI ya wanachama wa shirikisho la wanafunzi wa vyuo vikuu la Chama Cha Mapinduzi (CCM)mkoani Pwani wakifuatilia mkutano wa uchaguzi uliofanyia kwa lengo la kuchagua viongozi wa nafasi zilizoachwa wazi ikiwa ni pamoja na katibu,mhamasishaji na mwenezi.(Picha na Mwamvua Mwinyi)
…………………………………………………………………………
Na Mwamvua Mwinyi,Bagamoyo
SHIRIKISHO la Wanafunzi wa Vyuo Vikuu Tanzania (TAHLISO) la Chama Cha Mapinduzi limetakiwa kuwa moja ya mabalozi wa chama na serikali yake kwa kusema yale
yanayotekelezwa na Rais dk.John Magufuli na watendaji wake.
Aidha wasomi hao wametakiwa kuwa wazalendo wa nchi yao ikiwa ni pamoja na kuacha kutumika kama ngazi ya kupandisha watu wachache kwa maslahi yao.
Hayo yalisemwa Bagamoyo na mlezi wa tahliso,mkoani Pwani,alhaj Abdul Sharifu wakati wa uchaguzi wa kujaza nafasi za baadhi ya viongozi wa shirikisho hilo kimkoa.
Alhaj Sharifu alisema ,shirikisho hilo ni nguzo pekee ndani ya chama ambayo inapaswa kutia nguvu katika kukisemea na serikali yake iliyopo madarakani.
Alieleza kwamba,awamu ya nne ,iliona mbali na kuanza kushirikisha wanafunzi wa vyuo vikuu kujiunga kwenye chama hivyo watumie mwanya huo kueleza na mazuri yanayofanywa pasipo kuwa nyuma.
Alhaj Sharif alisema ,lengo kuu la chama ni mashirikisho hayo kupikwa kisiasa na kuwa viongozi wenye maadili mema baadae na kuwa viongozi bora na si bora kiongozi.
Katika hatua nyingine,alhaj Sharif alisema kuna baadhi ya watu wamekuwa wakilalamika hali ya kiuchumi ni mbaya na kusababisha wananchi kuwa kwenye hali ngumu ya kimaisha.
“Serikali inatambua nini inakifanya,na kudhibiti madudu yaliyokuwa yakifanyika,hivyo wasomi kwa kuwa ni waelewa jaribuni kuwaelewesha wananchi juu hili”alisema.
Alhaj Sharifu ambaye pia ni mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi (CCM) wilaya ya Bagamoyo alisema rais dk Magufuli amefanikisha suala zima la kodi kukusanywa kikamilifu,kuwadhibiti walaji wa fedha za serikali na kuwabana watu waliokuwa wakikwepa kodi .
Alifafanua,hali hiyo ilikuwa ikisababishia nchi hasara kubwa kwa kuikosesha mapato ya ndani ambapo kwasasa kila mmoja anajionea mapato ya serikali yanainuka.
“Nyie ni wasomi na viongozi wa siasa baadae ,waelezeni wananchi faida na malengo ya miaka ijayo “alisema alhaj Sharif.
Aliwataka viongozi waliochaguliwa kuweka mikakati ya kuwapa mafunzo ya itikadi kwa wanachama wao ili waweze kukijua chama na kuiva kisiasa.
Kwa upande wake mwenyekiti wa shirikisho hilo Filemon Mabuga alisema shirikisho limekuwa msaada mkubwa kwa chama na hata kwenye uchaguzi mkuu uliopita wa 2015 walifanya kazi kubwa ya kukipa chama ushindi .
Katika uchaguzi huo Method Mselewa amechaguliwa kuwa katibu wa shirikisho hilo mkoani Pwani na nafasi ya mhamasishaji alipata Magina huku na nafasi ya mwenezi ameshinda Salum Kiguni.

No comments :

Post a Comment