Serikali imetoa ufafanzi kuhusu
masuala mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa mikopo kwa vijana na malipo ya
ada kwa fedha za kigeni. Ufafanuzi huo umetolewa mjini hapa leo wakati
wa kikao cha pili katika Mkutano wa Sita wa Bunge la Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania.
Kuwainua Vijana Kiuchumi
Akijibu hoja kuhusu namna vijana
kutoka sehemu mbalimbali nchini wanavyoweza kufaidika kiuchumi, Naibu
Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira), Anthony Mavunde,
amesema Serikali imetenga fedha za kutosha kupitia mifuko mbalimbali
kuwawezesha vijana kwa mitaji na mafunzo ya ujasiriamali ili kuwainua
kiuchumi.
Ameongeza kuwa vijana wenyewe
ndio wanaopaswa kuchangamkia fursa hizo na pale wanapojiunga katika
vikundi mbalimbali wamekuwa wakipewa mikopo kwa ajili ya mitaji. Alitoa
mfano wa jinsi Serikali ilivyowawezesha vijana waliojiunga na kuwekeza
katika viwanda vidogo vya maziwa na chaki mkoani Simiyu.
Amewataka pia Wabunge na
Halmashauri zote nchini kuendelea kupigania kutengwa maeneo maalum
katika sekta mbalimbali kwa ajili ya kuwapatia vijana na kutengwa kwa
asilimia 5 ya mapato ya Halmashauri kwa maendeleo ya vijana
Ada kwa Fedha za Kigeni
Serikali imesema, ingawa
haijapokea malalamiko yoyote kuhusu wananchi wasioridhihwa na mtindo wa
kutakiwa kulipa malipo ya ada kwa fedha za kigeni katika baadhi ya shule
na vyuo, lakini imesisitiza kuwa wale wanaotoza ada kwa fedha za kigeni
wanakiuka Sheria.
Akitoa ufafanuzi huo, Naibu
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhandisi Stella Manyanya amesema
kwa mujibu wa kifungu cha 28 cha Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania (BOT),
2006, fedha inayopaswa kutumika kwa malipo ya huduma nchini ni Shilingi
ya Tanzania. Ameviagiza vyuo na shule nchini kuacha kutoza ada kwa
fedha za kigeni na kuhimiza wananchi watakaobainika kufanya hivyo kutoa
taarifa Serikalini.
Si Tatizo Kutumia Majengo UDOM
Serikali imesisitiza kuwa baadhi
ya Wizara zilizoanza kutekeleza agizo la kuhamia Dodoma kutumia baadhi
ya majengo kwa muda kwenye Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) hakutaathiri
shughuli za chuo.
Hayo yameelezwa na Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama. Waziri Jenista amesisitiza
kuwa baadhi ya Wizara zitatumia majengo ya UDOM kwa sababu mengi ya
majengo hayo yalikuwa hayatumiki kwa sasa kwa shughuli za chuo hicho na
hakutakuwa na muingiliano na shughuli za chuo.
Mradi wa Mabilioni Maji Dar
Serikali kwa kushirikiana na
Mamlaka ya Maji Dar es Salaam imeanza kutekeleza mradi wa usambazaji wa
maji utakaogharimu Dola za Marekani milioni 32.772 ambazo ni mkopo
kutoka Benki ya Exim ya China. Mradi huo utahusisha sehemu yote ya jimbo
la Kawe, Dar es Salaam. Mradi huo utachukua miezi 15.
Imetolewa na:
Idara ya Habari-MAELEZO.
No comments :
Post a Comment