Na: Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma
Serikali haina mamlaka ya kuweka ukomo wa riba au riba elekezi itakayotumiwa na mabenki katika kutoa mikopo.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango
Dkt. Ashatu Kijaji ameeleza hayo leo Bungeni, Mjini Dodoma alipokuwa
akijibu swali la Mbunge wa Baraza la Wawakilishi Machano Othman Said juu
ya lini Serikali itaweka utaratibu wa kupunguza riba ya mikopo walau
kufikia asilimia 10 – 12 badala ya sasa ambayo ni asilimia 17 – 20.
“Mabadiliko ya Sekta ya Fedha ya
mwaka 1991 yalipelekea Serikali kujitoa katika uendeshaji wa moja kwa
moja wa shughuli za kibenki nchini ili kuruhusu mfumo wa soko huria,
hususan nguvu ya soko kuamua viwango vya riba za mikopo, riba za amana
na gharama nyingine za huduma za kibenki,” alifafanua Dkt. Ashatu
Kijaji.
Aliendelea kwa kusema kuwa viwango
vya riba za mikopo na riba za amana pamoja na riba za mikopo kati ya
benki na benki hupangwa kwa kuzingatia gharama za upatikanaji wa fedha,
gharama za uendeshaji, riba za dhamana za Serikali, sifa za mkopaji na
hatari ya mkopaji kutolipa mkopo pamoja na kasi ya mfumuko wa bei.
Aidha Dkt. Ashatu Kijaji amesema
kuwa kutoa maelekezo kwa mabenki kutumia viwango fulani vya riba katika
biashara zao, kutaifanya Benki Kuu kukosa nguvu na mamlaka ya
kuyachukulia mabenki hatua endapo yatapata hasara kwa kutumia riba
ambayo Benki Kuu imeelekeza.
Vile vile amesema kuwa kiwango cha
hatari ya kutolipa mkopo ni miongoni mwa vigezo vinavyotumiwa na
mabenki katika kupanga viwango vya riba za mikopo, ambapo kwa sehemu
kubwa gharama za riba za mikopo hutegemea zaidi gharama za upatikanaji
wa fedha pamoja na gharama za uendeshaji.
Pia amesema kuwa, ni muhimu
kutambua kwamba kadri riba za mikopo zinapokuwa juu, ndivyo riba za
amana zinapokuwa juu pia, ambapo wastani wa riba za kukopa kwa mwaka
mmoja mwezi Juni, 2016 ulikuwa asilimia 13.67 wakati wastani wa riba za
amana za mwaka mmoja ulikuwa asilimia 11.52 ikiwa ni tofauti ya asilimia
2.25.
No comments :
Post a Comment