Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Ni jambo lisilopingika kuwa
matumizi makubwa ya fedha za Serikali yanatumika katika ujenzi wa
miundombinu ya Umma ambapo matumizi hayo yanahusisha karibu asilimia 53
ya Bajeti nzima ya nchi.
Tunaishukuru Serikali kwa kuweka
kipaumbele katika suala hilo kwani ni muhimu kuwa na miundombinu mizuri
na bora ili kutoa huduma bora kwa wananchi na kurahisisha ufanyaji kazi
hivyo kuharakisha maendeleo ya nchi katika Nyanja zote muhimu zikiwemo
za biashara, utalii na mawasiliano.
Miradi ya ujenzi ya miundombinu ya
Umma inayoelezewa hapa ni ile ambayo inajengwa kwa fedha za Serikali
kwa ajili ya matumizi ya wananchi wote ikiwemo ya barabara, hospitali na
vituo vya afya,shule,vyuo,nyumba za kuishi pamoja na ofisi mbalimbali.
Jitihada hizo za Serikali
kuhakikisha miundombinu ya Umma inaleta maendeleo imekuwa ikikwamishwa
na changamoto mbalimbali zinazojitokeza pindi mradi husika unavyoanza
kwani wahusika wanakuwa wanajiamulia jinsi ya kufanya ili mradi ujenzi
husika umalizike.
Hali hiyo inapelekea Serikali
kupata hasara kwa kupoteza fedha nyingi na kuambulia kubaki na majengo
yasiyo na viwango ambayo mwisho wake hushindwa kutumika na kuilazimu
Serikali kuanza upya ujenzi husika baada ya kubomoa.
Kwa kuwa Serikali hii ni sikivu na
imejipanga kuhakikisha nchi inafika katika uchumi wa kati basi
tunaamini mambo hayo hayana nafasi na hayawezi kutokea tena katika nchi
hii watu kuachiwa uhuru wa kutumia vibaya fedha za Umma zinazotolewa kwa
ajili ya ujenzi wa miundombinu.
Tunaamini kuwa maendeleo ya nchi
yanachangiwa na wananchi wenyewe kwa njia ya ukusanyaji wa kodi na
ushuru mbalimbali hivyo hata miundombinu ya umma inajengwa kwa kutumia
fedha za wananchi zinazopatikana kwa njia ya ukusanyaji mapato.
Hivyo, ili kuifanya Serikali kuwa
na taswira nzuri kwa wananchi wao pamoja na kuwafanya wananchi kuiamini
Serikali yao ni vizuri kuwapa taarifa juu ya matumizi ya fedha hizo
wanazozikusanya.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano,(Ujenzi), Mhandisi. Joseph Nyamuhanga amewahi
kusema kuwa Sekta ya Ujenzi ni sekta moja wapo inayoonekana imekithiri
kwa rushwa duniani kwa sababu takribani asilimia 10 hadi 30 ya Bajeti
yake inapotea kwa njia ya rushwa na usimamizi mbaya hivyo ili kuondoa
dhima hii ni lazima kukusanya na kutoa taarifa kwa wananchi juu ya
ujenzi wa miundombinu hiyo.
Kuwapa taarifa wananchi juu ya
miradi mbalimbali haswa ya ujenzi wa miundombinu kutaamsha ile hali ya
watu kuona umuhimu wa kulipa kodi kwa sababu wanaona matumizi ya fedha
wanazozikusanya.
Taarifa hizo pia zitaendeleza
uwajibikaji na uwazi katika ujenzi wa miundombinu hiyo hivyo kupunguza
vitendo vya rushwa,kujenga miundombinu inayoendana na thamani ya fedha
zilizotolewa kwa ajili ya ujenzi husika pamoja na kujenga miundo mbinu
bora na imara.
Ni muhimu kwa Serikali kupitia
miradi yote iliyojengwa na inayoendelea kujengwa kwa kutumia fedha za
Umma ili kugundua thamani halisi ya majengo hayo na kutoa taarifa kwa
wananchi.
Jambo hili pia litasaidia vyombo
husika vya kisheria kuwachukulia hatua watu wote walioshiriki kutumia
vibaya fedha za wananchi kwa kujenga miundombinu iliyo chini ya kiwango
au isiyoendana na thamani ya fedha iliyotolewa kwa ajili ya ujenzi
husika.
Rai inatolewa kwa wizara na idara
zinazohusika na ujenzi wa mioundombinu ya umma kutoa elimu ya kutosha
kwa wananchi juu ya mradi upi uko wapi na unathamani gani ili wananchi
waweze kupima kama kiasi walichoambiwa kimetumika kina thamani ya fedha
waliyoambiwa?
Pia ni muhimu wananchi
wakaelimishwa juu ya umuhimu wa kuwa walinzi katika miundombinu hiyo ili
isitokee watu wachache wakuihujumu kwani fedha nyingi za walipa kodi
zimetumika.
No comments :
Post a Comment