Mkemia Mkuu wa Serikali, Prof.
Samwel Manyele (katikati) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo
pichani) leo Jijini Dar es Salaam kuhusu mafunzo ya wasafirishaji na
watumiaji wa Kemikali nchini, kutoka kulia ni Kaimu Meneja wa Maabara ya
Kanda ya Mashariki, Everlight Matinga na Mkurugenzi wa Idara ya
Usimamizi na Udhibiti wa Kemikali nchini,Sabanitho Mtega, (kutoka
kushoto), Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi Jinai na
Huduma za
Vinasaba, David Elias pamoja na Mkurugenzi wa Idara ya Biashara,George
Kasinga.
………………………………………………………………………
Na jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu
wa Serikali (GCLA) wamejipanga kuendelea kuendesha mafunzo kwa wadau wa
Kanda ya Mashariki wanaohusika na kemikali ili kuhakikisha kemikali
zinatumika vema na kwa njia salama.
Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es
Salaam na Mkemia Mkuu wa Serikali, Prof. Samwel Manyele alipokuwa
akizungumza na waandishi wa habari kuhusu wasafirishaji na watumiaji wa
kemikali nchini.
Prof. Manyele amesema kuwa wakala
hufanya usajili na ukaguzi kwa wadau wote wanaohusika na kemikali
wakiwemo waagizaji, watengenezaji, wasafirishaji, watumiaji,
wanaosafirisha nje ya nchi au yeyote yule anayehusika na kemikali kwa
njia moja au nyingine.
Pia ukaguzi huo unahusisha mahali ambapo kemikali zinatumika, zinatunzwa au kuhifadhiwa.
“Kuanzia mwaka 2012 hadi sasa,
wadau wa Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani waliopatiwa mafunzo ni 642
wakiwemo Askari wa Jeshi la Polisi Usalama Barabarani Tanzania Bara,
wasimamizi wa shughuli za uzalishaji kwenye viwanda, wasambazaji,
wasafirishaji wa kemikali pamoja na madereva wanaosafirisha kemikali.,
hivyo baada ya kuona umuhimu wake tumeamua kuendelea na mafunzo haya kwa
wadau wetu wengine,” alisema Prof.Manyele.
Prof. Manyele ameongeza kuwa
mafunzo hayo yatatolewa kwa siku mbili kwa kila kundi katika makundi
matatu yakiwemo ya wasimamizi wa shughuli zinazohusisha kemikali
watakaoanza tarehe 21- 22/02/2017, Mawakala wa Forodha watakaoanza
tarehe 23-24/02/2017 pamoja na madereva wanaosafirisha kemikali kuanzia
tarehe 10-11/03/2017.
Aidha, Wakala Mkuu wa Serikali
amefafanua kuwa Wakala hautaruhusu mdau ambaye hajapitia mafunzo hayo
kuhusika katika shughuli yoyote ya kemikali kwa kutumia, kuhifadhi,
kusafirisha, kutoa bandarini na hata kuagiza kutoka nje ya nchi hivyo
akasisistiza umuhimu wa wahusika kuhudhuria mafunzo hayo.
Ametoa rai kwa wadau hao kuwahi
kuhudhuria mafunzo haya ili kutekeleza matakwa ya Sheria Na. 3 ya mwaka
2003 ya Udhibiti na Usimamizi wa kemikali pamoja na kuepuka usumbufu
utakaoweza kujitokeza kwa sababu ya kukosa mafunzo.
No comments :
Post a Comment