*Ni kutoka Karatu-Mbulu-Haydom-Sibiti-Lalago hadi Meatu
*Nyingine ni ya kutoka Haydom hadi Katesh
*Limo pia daraja la Magara linalounganisha Mbulu na Babati
SERIKALI imepanga kujenga
barabara mbili kuu za lami ambazo zikikamilika zitasaidia
kuunganisha
mikoa mitano ya Arusha, Singida, Simiyu, Shinyanga na Manyara.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
ametoa kauli hiyo jana (Jumatatu, Februari 20, 2017) kwa nyakati tofauti
wakati akizungumza na wananchi wa kata ya Haydom na Mbulu Mjini kwenye
mikutano wa hadhara iliyofanyika wilayani Mbulu, mkoani Manyara.
Waziri Mkuu amezitaja barabara
hizo kuwa ni ya kutoka Karatu-Mbulu-Haydom-Sibiti-Lalago- Meatu hadi
Maswa yenye urefu wa km. 389 (maarufu kama Serengeti Southern Bypass) na
nyingine ni ya kutoka Haydom hadi Katesh yenye urefu wa km. 74. Pia
limo daraja la Magara linalounganisha Mbulu na Babati.
Amesema anatambua umuhimu wa
barabara hizo na kwamba kukamilika kwake kutaharakisha kuufungua mkoa
huo na kuongeza fursa za kiuchumi kwa wakazi wake.
“Fedha kwa ajili ya upembuzi wa
awali imeshatolewa na kazi imeshaanza kwa ajili ya barabara ya kutoka
Karatu-Mbulu-Haydom-Sibiti-Lalago hadi Meatu na Maswa lakini hii ya
Katesh hadi Haydom itaombewa fedha kwenye bajeti tunayoiandaa hivi
sasa.”
“Lengo letu ni kuona hospitali ya
rufaa ya Haydom inafikiwa kwa urahisi zaidi.La sivyo wagonjwa
watakaoletwa hapa watafika wakiwa hoi zaidi,” ameongeza.
Akizungumzia kuhusu hoja ya
ujenzi wa daraja la Maraga ambayo iligusiwa na wabunge wote wa mkoa huo,
Waziri Mkuu alisema: “Waheshimiwa wabunge wasemea vikali kuhusu daraja
la Maraga. Napenda kuwathibitishia kwamba Serikali imeshatoa kiasi cha
sh. milioni 950 kwa ajili ya ujezi wa daraja hili muhimu ambalo
linaunganisha wilaya zetu za Mbulu na Babati.”
Akizungumzia ahadi ya Mheshimiwa
Rais Dk. John Pombe Magufuli kuhusu ujenzi wa barabara ya lami wa km. 5
Haydom, km. 6 Dongobesh na km. 5 mji wa Mbulu, Waziri Mkuu alisema
analibeba suala na kulipekea kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa ili alifuatilie.
Kuhusu tatizo la maji, Waziri
Mkuu alisema Serikali imeshatoa kiasi cha milioni 200 kwa ajili ya
Mamlaka ya Maji ya Mji wa Mbulu ili wafanye utafiti wa vyanzo vya maji
vya uhakika na pia imetoa sh. milioni 300 kwa ajili ya Halmashauri ya
Wilaya ya Mbulu ili watafute maeneo ya uhakika ya kuchimba visima.
“Huku kwenye Halmashauri vijiji
ni vingi. Kwa hiyo tumetoa sh. Milioni 300 ili watafute ni wapi wanaweza
kuchimba visima virefu na vya kati ili kuondoa tatizo hili kwa wananchi
wetu. Mkurugenzi wa Halmashauri sisitiza wataalamu wako watafute vyanzo
hivina watumie fedha hizi vizuri,” alisisitiza.
Waziri Mkuu leo anaendelea na
ziara yake ya kikazi ya siku sita mkoani Manyara kwa kutembelea wilaya
ya Hanang ambako atapokea taarifa ya wilaya hiyo atazungumza na
watumishi wa umma, na kuzungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara.
No comments :
Post a Comment